December 29, 2012

'KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE: MRADI MGUMU KULIKO YOTE"

Mimi na mzee Kamara Kusupa, hii leo Ofisini, mambo ya kuhariri kitabu chake kipya.

Kwa muda mrefu tumeshuhudia maandiko mengi kuhusiana na sisi waafrika. Yapo maandishi kama ya akina Cheikh Anta Diop, Dk. Elly Kamugisha, Franz Fanon, Julius Nyerere, Leopold Senghor na wengineo. Lakini jambo kubwa lililokuwa likijadiliwa ni nani hasa huyu MWAFRIKA. Mathalani wengi wanakubaliana kwamba mwafrika ni mtu mweusi, hivyo kuwatenga waarabu, wahindi, wazungu na wabarbaig ambao kimsingi nao wamejikuta wakiwa wamezaliwa katika bara ya Afrika. Msomi Dk Harrith Ghassany yeye alihoji nini asili ya Afrika na akaelezea kuwa ni kutoka kule Tunisia.
Dk Harrith alisema hayo kwenye kitabu chake cha KWAHERI UHURU, KWAHERI UKOLONI: ZANZIBAR NA MAPINDUZI YA AFRABIA. Ni moja ya changamoto alizotoa ambao kila mwenye udadisi atajikuta akishughulisha ubongo wake. Wapo wachambuzi makini kama Joseph Mihangwa ambaye kwa sasa maandiko yake yanapatikana katika gazeti la RAIA MWEMA, amekuwa akihojia mara kwa mara juu ya asili ya afrika na kuelezea mambo kadhaa yaliyowahi kutokea huko nyuma. Yote haya yanatuletea swali la msingi MWAFRIKA huyu ni nani?
Hata hivyo dunia imebadilika sana na kila kona inatusaidia kujua nini hasa kinachopaswa kusemwa kwa dhati na moyo safi kwa nyakati za sasa. Kuna wazungu wamezaliwa Afrika Kusini, Tanzania na wengine nchi nyingine za Afrika. Je hawa watakwenda wapi ikiwa hawajui asili zao zilikuwa namna gani. Ni kama ambavyo Waafrika wanavyojiuliza ni namna gani wataweza kurudi Afrika ambako hawajui waanzie wapi.

Ni vigumu leo kumwelezea Cliford Harris au T.I arudi afrika kutoka Marekani. Ni vigumu vilevile kumweleza Lennox Lewis arudi barani afrika. Ni vigumu kumwambia Danny Jordan wa Afrika Kusini kwamba uchotara wake sio kitu arudi kwenye asili ya makaburu. Au ni vigumu kumwambia Hellen Zille mwenyekiti wa chama cha upinzani cha D.A pale Afrika Kusini na gavana wa jimbo la Cape Town, kwamba arudi kwa wazungu wenzake. Hii ni moja ya mabadiliko makubwa ya mipaka ya nchi ambayo imeshindwa kuzuia mahusiano ya wanadamu kutoka nchi moja hadi nyingine au kutoka jamii ya nchi moja kwenda jamii ya nchi nyingine. Leo mwafrika anaweza kuzaa na mchina au Mkorea hivyo ni vigumu mtoto atakayezaliwa kutotambuliwa kuwa mwafrika, na kuangalia asili. 
Lakini wapo watu wanaojaribu kujiuliza ni namna gani wanaweza kuwakumbusha waafrika wenzeo kuwa Mwafrika alikuwa na asili yake. Ni mwafrika alikuwa wa kwanza kuwasilia Marekani kabla ya christopher Columbus, ambapo ushahidi mwingine uliandikwa na Profesa Ivan Sertima kwenye kitabu chake "THEY CAME BEFORE COLUMBUS". 
Nikiwa na mzee Kusupa. Duh anahamu mpaka amevunja meza.
Hata ukisoma 'voyage' mbalimbali za Columbus kumejaa mengi ya kushangaza na kwanini yanachukuliwa kuwa kama yalivyo?. Tukiacha hilo tunajikuta tunaangalia sisi Waafrika ni nani na asili yetu ikoje. Dhana ya uhai inakuwa kubwa na inachukua mkondo mkubwa sana, hivyo basi kitabu cha KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE; MRADI MGUMU KULIKO YOTE hakika kinakuletea baadhi ya majibu ya maswali ambayo kila mara watu wanajiuliza. 
Hii inaonekana kuanzia kwenye DINI, SIASA, UTAMADUNI, na mengine mengi kuhusu Afrika yetu. Mwandishi wa kitabu hicho MWINJILISTI KAMARA KUSUPA anatuelezea mengi kwamba kuna makosa kadhaa yanafanyika, na amekuwa akisogea mbele kidogo zaidi ya anapoishia mwanazuoni kama Ali Mazrui. 
Kila jamii imekuwa kwenye asili yake, na inakuwa vigumu kurudi kwenye asili yake. Nini ambacho Kamara Kusupa anatuelezea kwenye kitabu hicho, hakika tunapaswa kuwa watulivu na kuvuta subira kwamba ni moja ya kitabu chenye mafunzo mengi kwa watu wa Afrika. Je, dini za waafrika ni zipi? Mfumo wa utawala wa waafrika ni upi? Msingi wao na dhana ya uhai vikoje? Uhusiano wao na jamii za nje ukoje? Je, mwafrika ataepuka dhahama ya mabadiliko ya kijamii duniani? Je, mwafrika ataweza kurudi katika asili yake? 
Nadhani ni moja ya mambo ya kusisimua na hakika yatakuwa na hamasa kwa wasomi na wananchi wengine. Ikumbukwe hicho kitakuwa kitabu cha tatu kutoka kwake, kwani alishaandika vitabu viwili; MAISHA YANGU GEREZANI, na kingine HII NDIYO TANZANIA TUNAYOITAKA. Kitabu cha pili nilishiriki kwa kiasi kikubwa, na sasa nashiriki pia kuhariri na kuweka lugha bora yenye hadhi kwa wasomaji makini. Ninadhani wasomaji watafurahia zaidi. Na tuseme basi kama kweli tutaweza kurudi kwenye asili yetu au ni mradi mgumu?    MWINJILISTI KAMARA KUSUPA atatujibu hilo, usikose kukisoma kitabu hicho.

1 comment:

Maoni yako