December 20, 2012

SERIKALI YATENGA SH. BILIONI MOJA KUJENGA DARAJA LA KAVUU

mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi.

SERIKALI imetenga kiasi cha sh. bilioni moja kwa ajili ya kazi za awali za ujenzi wa daraja la mto Kavuu linalounganisha kata za Mamba, Kasansa, Majimoto, na kijiji cha Inyonga yalipo makao makuu ya wilaya mpya ya Mlele. 

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana jioni (Jumatano, Desemba 19, 2012) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mamba kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya saba ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi. 
Waziri Mkuu alisema Serikali ina nia ya kufungua mawasiliano kati ya bonde la Rukwa na mikoa ya kaskazini ambako kuna uhaba wa chakula. “Bonde hili linasifika kwa uzalishaji mkubwa wa nafaka kwa hiyo kujengwa kwa daraja hilo ni ukombozi mkubwa wa kufungua soko kwa mazao mnayozalisha huku,” alisema. 
Alisema katika mwaka huu wa fedha, barabara ya kutoka Sitalike kupitia Kibaoni, Majimoto, Mamba hadi Kasansa yenye urefu wa kilomita 33.5 imetengewa sh. milioni 837/- na kwamba wakandarasi wawili wamekwishapatikana ili kuifanyia ukarabati barabara hiyo.
Kuhusu barabara ya Majimoto hadi Inyonga yenye urefu wa kilometa 135, Waziri Mkuu alisema zimetengwa sh. milioni 943/- kwa ajili ya ujenzi wa madaraja katika barabara hiyo. 
Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa fedha hizo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Katavi, Mhandisi Isaack Kamwelwe alimthibitishia Waziri Mkuu kuwepo kwa fedha hizo. 
“Fedha zimeshatengwa na leo nimepokea kibali cha kutangaza zabuni za ujenzi wa daraja hilo. Zabuni zitatangazwa kuanzia Januari 2013,” alisema. 
Kutokuwepo kwa daraja la Kavuu kunawafanya wakazi waishia bonde la Rukwa (maeneo ya Majimoto na Mamba) kila wanapotaka kwenda Inyonga, walazimike kupitia Mpanda yaliko makao makuu ya wilaya yao ambako ni zaidi ya kilometa 350. 
Kesho (Ijumaa, Desemba 21, 2012) Waziri Mkuu atakwenda kata ya Usevya ambako atazindua mradi wa umemejua kwenye sekondari ya kata ya Usevya na kuhutubia wananchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 20, 2012.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako