Na Salvatory Mkami, Dar es salaam
Mheshimiwa rais Kikwete mkatika hotuba yake mheshimiwa
alieleza kuwa matokeo hayo ni ishara kwamba ifikapo mwaka 2016 kuna uwezekano
wa idadi hiyo kufikia milioni 51 jambo ambalo linaweza kuwa ni mzigo kwa taifa,
jamii na hata katika masuala ya uchumi.
Mheshimiwa Rais alizidi kufafanua kuwa jamii inapaswa
kuyachukulia kwa uzito matokeo hayo hasa katika masuala ya kupanga uzazi pamoja
na kuongeza bidii ya kufanya kazi.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, inaonesha kuwa kwa wastani,
kila sekunde moja wanazaliwa watoto watano hapa duniani, na wakati huo huo watu
wawili wanafariki dunia, achilia mbali zile mimba zinazoharibika.
Maana ya tofauti hiyo kati ya vizazi na vifo ni kwamba watu
watatu wanaongezeka duniani kila sekunde moja. Ukizidisha idadi hiyo utagundua
kwamba kuna ongezeko la watu 11,000 kwa saa na watu 265,000 kwa siku na hii
inafanya dunia kuwa ongezeko la watu milioni 100 kwa mwaka.
Hivi sasa dunia ina watu wapatao bilioni 7. Mwaka 1750
kulikuwa na watu milioni 800 tu duniani. Kufikia mwaka 1850 idadi iliongeka na
kufikia watu bilioni 1.8.
Mwaka 1950 idadi ya watu ikawa bilioni 2.5. Ilichukuwa miaka
50 idadi ya watu kufikia bilioni 6 yaani mwaka 2000. Ilikisiwa kwamba mpaka
kufikia mwaka 2010 idadi ya watu hapa duniani itafikia watu bilioni 7, ikiwa ni
ongezeko la watu bilioni 1 kwa muda wa miaka 10.
Lakini pia Ukiangalia mtiririko wa takwimu hizo utagundua
kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa kasi hapa duniani kuanzia karne ya
19. Kwa mfano nchi yetu ya Tanzania iko chini ya kiwango cha
ongezeko la watu hapa duniani ukilinganisha na nchi nyingine zilizoko dunia ya
tatu. Tanzania ina ukubwa wa eneo la mita za mraba zipatazo 342,100, karibu
sawa na Misri ambayo ina ukubwa wa mita za mraba zinazofikia 384,300.
Pamoja na kwamba tofauti ya ukubwa kati ya nchi hizi mbili
ni ndogo sana lakini Tanzania imezidiwa kwa idadi ya watu karibu mara mbili na
Misri. Kwani wakati Tanzania ikiwa na idadi ya watu wapatao milioni 44, Misri
ina idadi ya watu wapatao milioni 83 kwa mujibu wa sensa iliyofanyika Julai
2012.
Ikiwa utaiunganisha Tanzania na nchi ya Benin iliyoko Afrika
Magharibi ukubwa wake utalingana na nchi ya Misri, kukiwa na tofauti ndogo
sana. Ukijumlisha idadi ya watu wa nchi ya Benin wanaokadiriwa kufikia watu
milioni 9 (kwa mujibu wa sensa iliyofanyika Julai 2012) na idadi ya watu wa
Tanzania unapata idadi ya watu wapatao milioni 53, ikiwa bado ni chini ya idadi
ya watu wa nchi ya Misri.
Hii inaonesha bado nchi hii ina kiwango kidogo sana cha
idadi ya watu ukilinganisha na nchi nyingine zilizo katika dunia ya tatu. Kwa
hiyo sioni sababu ya serikali yetu kupiga kelele sana kuzuia watu wasizaane.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, imekadiriwa
kwamba watoto milioni 1.6 huzaliwa kila mwaka hapa nchini. Na kwa mujibu wa
takwimu zilizotolewa hivi karibuni na wizara ya afya zinaonesha kwamba watoto
wanaosajiliwa ni 140,000 kila mwaka ikiwa ni asilimia 10 tu ya watoto
wanaozaliwa, hii inaonesha kwamba kuna idadi kubwa ya watoto wanaofia tumboni,
na wale wanaofariki baada ya kuzaliwa inakuwa haijachukuliwa na kuingizwa
kwenye takwimu za serikali.
Hata hivyo inakadiriwa kwamba watoto wapatao 51,000 hufariki
baada ya kuzaliwa hapa nchini, na wakati huo huo 43,000 hufia tumboni kila
mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu hizo inaonesha kwamba bado tunayo
safari ndefu ya kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa hapa nchini,
kabla hatujaanza kupiga kelele ya watu kuzaa kwa mpango.
Hata hivyo chapisho hilo linabainisha kwamba mataifa makubwa
yameanza kuonesha wasiwasi juu ya ongezeko la watu hapa duniani. Mataifa hayo
yanadai kuwa ongezeko la watu linasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, na
hivyo kutishia dunia isiwe salama.
Kwani kumekuwa hakuna udhibiti wa kutosha kiasi kwamba watu
wamekuwa wakitawanyika kwa ajili ya kutafuta makazi na hivyo kuvamia maeneo ya
misitu ya asili na vyanzo vya maji na kufanya uharibifu mkubwa mkubwa wa
mazingira.
Imebainika kwamba iwapo watu hao watasogezewa miundo mbinu
kama vile Barabara, shule, hospitali, na huduma mbali mbali za kijamii katika
maeneo hayo ya hifadhi waliyoyavamia, itakuwa na maana ya kuhalalisha uharibifu
wa mazingira.
Pia wataalamu hao wanadai kwamba ongezeko la watu haliendi
sambamba na ujenzi wa miundo mbinu ambayo itasaidia kulinda uharibifu wa
mazingira.
Labda niwaulize ndugu wasomaji, hivi nchi masikini na zile
nchi tajiri zenye viwanda ni zipi hasa zinazoifanya dunia hii isiwe salama?
Wao wana viwanda wanazalisha sumu kila uchao huku
wakitulisha vyakula na madawa yenye sumu ili kujikusanyia utajiri, halafu leo
wanasema kuwa nchi masikini ndizo zinazochangia uharibifu wa mazingira na
kuifanya dunia isiwe salama, huu ni uonevu wa hali ya juu.
HEBU TUANGALIE UPANDE MWINGINE WA SHILINGI WA KADHIA HII:
Kuzungumzia ongezeko la watu, unazungumzia ongezeko la soko,
kwa maana ukuaji wa biashara, nguvu kazi, na ongezeko la viwanda, na hivyo
ukuaji wa uchumi kuongezeka.
Kwani kwa jinsi idadi ya watu inavyozidi kuongezeka na
ndivyo uchumi unavyozidi kukua, hebu angalia nchi kama ya China, India,
Marekani na iliyokuwa Urusi kabla haijasambaratika, ukuaji wa uchumi katika
nchi hizo ulitokana na kuwa na idadi kubwa ya watu.
Ila naomba nitahadharishe kidogo hapa, ninapozungumzia
ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi nazungumzia nchi kutumia nguvu kazi katika
kuzalisha na kuwa na serikali makini inayowawezesha wananchi wake kufikia
malengo yao.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako