January 21, 2013

NINI SABABU YA UMASIKINI AU UTAJIRI WA NCHI?Na Dkt. Hamisi Kigwangalla
Mnamo mwaka 1945 wakati vita kuu ya pili ya dunia ilipokuwa inaelekea kuisha, Korea ambayo ilikuwa iko chini ya utawala wa kikoloni wa Japan toka mwaka 1910 ilipata uhuru wake. Kabla ya hapo majeshi ya ukombozi ya Korea (Korean liberation army) yalikuwa na mpango wa kupigana na japan ili kudai uhuru wao. Kama bahati haikufikia kwenye kudai uhuru kwa vita lakini anguko la Japan kwenye vita kuu ya pili ya dunia ilifanya Korea ipewe uhuru wake bila mtutu wa bunduki. 
Ndani ya mwezi mmoja tu baada ya Japan kunyoosha mikono juu, Korea ilijikuta ikigawanywa mara mbili kwenye mstari unaojulikana kama ‘the 38th parallel north’ (nyuzi 38 kaskazini na sambamba na ikweta) na kuwa mamlaka mbili tofauti zenye ushawishi tofauti. Kusini ikiwa chini ya usimamizi wa Marekani na Kaskazini chini ya Urusi.
Amani ya kipindi cha vita baridi kati ya mamlaka hizi mbili iliisha katikati ya mwaka 1950 pale Korea ya Kaskazini ilipoamua kuivamia Korea ya Kusini na kufikia hadi kuuteka mji mkuu wa Korea ya Kusini, Seoul.
Leo hii nchi hizi zimekuwa dunia mbili tofauti kabisa. Korea ya Kaskazini ikiwa na mfumo tofauti kabisa wa kiuchumi na ile ya kusini. Pengine sababu pekee inayozitofautisha hizi Korea mbili, ambazo zamani zilikuwa moja na sawia kabisa katika kila Nyanja. Leo hii Korea ya Kaskazini hakuna ruhusa kuwa na simu ya mkononi inayotoa mawasiliano nje ya mipaka ya nchi, kuna watu wanaishi chini ya dola moja, kuna ugumu wa namna ya kusafiri kutoka sehemu moja mpaka nyingine, wakati ndugu zao wa Korea ya Kusini wanaishi maisha ya utajiri, ya uhuru wa kuwasiliana kwa simu za kiganjani, kwa mitandao na uhuru hata wa kusafiri na kufanya biashara na yeyote yule wa popote pale duniani – tunu ambazo zimewafanya leo hii wawe kwenye nchi ambazo zinahesabika kama ni za dunia ya kwanza.

Wakati Korea ya Kaskazini ikiishi kwa kutegemea misaada ya chakula na fedha kutoka nchi nyingine, Korea ya Kusini imejenga uchumi imara unaotokana na matumizi ya teknolojia na sayansi ya zama za sasa na imekuwa ni mfadhili wa nchi zinazoendelea kama Tanzania na hata Korea ya Kaskazini.

Ukiangalia kwa undani sana utabaini kuwa kinachotofautisha nchi hizi, zenye historia ya kufanana, zenye jiografia ya kunana, zenye watu wenye kuongea lugha moja, zenye dini, utamaduni na mila na desturi za kufanana, mienendo ya kufanana, kila kitu kinafanana, leo hii kinachowatofautisha si kingine zaidi ya ule mpaka uliowekwa kati yao (the 38th parallel north). Ni nini haswa kinachowafanya wa Kusini wawe matajiri na wa Kaskazini wawe maskini? Maisha ya watu wa Korea ya Kaskazini na yale ya watanzania hayana tofauti sana leo hii wakati yale ya ndugu zao wa Korea ya Kusini yanafanana kabisa na ya wazungu wa Ureno ama wa Hispania. Miaka ya kuishi ya mtu wa Korea ya Kaskazini ni kumi nyuma ya ile ya ndugu zao wa Korea ya Kusini, upande wa pili tu wa ule mstari.

Hizi tofauti zinazoonekana leo siyo za kihistoria. Na kwa hakika hazikuwepo kabla ya ile vita kuu ya pili ya dunia. Kilichotokea baada ya mwaka 1945 ni kwamba hizi serikali mbili, ya Kusini na ile ya Kaskazini zilifuata mifumo miwili tofauti ya kiuchumi, moja ilijenga mfumo wake kufuatia mfano wa kiliberali wa soko huria lililoruhusu uhuru wa masoko na mitaji kama ule unaofuatwa na nchi za magharibi na marekani, na nyingine, Korea ya Kaskazini, ilifuata mfumo wa kikomunisti.

Japokuwa marais wa kwanza wa Korea ya Kusini hawakuweka mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia, wengine wanasema kwa kuhofia kuvamiwa na mfumo wa kitawala wa kikomunisti uliokuwa unasambaa kwa kasi sana maeneo ya Asia wakati huo, walisimamia mfumo wa soko huria. Marais hao, Syngman Rhee, ambaye alisomea vyuo mashuhuri duniani vya Harvard na Princeton, na mwenzake Jenerali Park Chung-Hee, ambaye ni baba mzazi wa Rais wa kwanza wa kike wa nchi hiyo aliyeshinda uchaguzi mkuu juzi tu hapa, wameingia kwenye historia za marais waliotumia nguvu kuongoza nchi yao na ikafanikiwa.
Rais wa pili wa Korea ya Kusini atakumbukwa daima na watu wa Korea ya Kusini kwa kusukuma ruzuku na mikopo kwenye makampuni yaliyoonesha mwelekeo wa kufanikiwa. Kwa upande wa Korea ya Kaskazini, Kim Il-Sung, ambaye alikuwa kiongozi aliyeendesha harakati za kikomunisti za kupinga utawala wa kijapan alitawazwa kuwa Rais wa Korea ya Kaskazini mwaka 1947, na moja kwa moja aliwekeza nguvu zake katika kujenga mfumo wa kiuchumi ambao uliweka chini ya serikali kuu mamlaka yote ya kuandaa mipango ya kukuza na kuendesha uchumi wa nchi chini ya mfumo wa kikomunisti wa ‘Juche’. Rais Kim Il-Sung alizuia mfumo wa soko huria na hakukuwa na ruhusa ya kumiliki mali binafsi.

Hakuna jiografia, wala utamaduni, wala historia ya nchi inayoweza kuelezea tofauti ya kiuchumi kati ya nchi hizi mbili, ambazo si zaidi ya miaka 60 iliyopita zilikuwa nchi moja. Tukichukulia haya ‘maajabu ya Korea ya Kusini’ (the south Korean miracle) kama somo, tunapaswa tujifunze kitu, kwanza tuangalie ni nini chanzo cha kuendelea kwa Korea hii moja na kushidwa kwa nyingine? Majibu yake yanapatikana, kwa vyovyote vile kwenye mfumo wa kisiasa na kiuchumi uliofuatwa baada ya uhuru wa Korea kutoka chini ya utawala wa kikoloni wa Japan. 
Moja ilifuata mfumo wa soko huria na nyingine mfumo wa kikomunisti, je tofauti hizi za kimfumo zinaweza kutumika pia kuelezea utofauti wa kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya? Na je sababu hizi zinaweza kutumika kuelezea spidi ya ukuaji wa Uchumi wa nchi ya Rwanda? Sina jibu sahihi la maswali haya. Watanzania tuendelee kujipanga, pengine tusijidai sana na nafasi yetu kijiografia, kihistoria na hata kiutamaduni, maana jibu la umaskini wetu halipo huko, lipo kwenye mfumo wa kisiasa na kiuchumi tunaoufuata.
Mafanikio baina ya nchi kiuchumi yanatofautiana kwa sababu za tofauti ya aina za taasisi walizoweka kwenye nchi husika, sheria, kanuni na taratibu zinazoathiri uchumi walizotunga na namna ya motisha walizoweka kwa ajili ya watu wao. Angalia tofauti ya mtoto wa Korea ya Kaskazini na yule wa Korea ya Kusini, mmoja anakua huku akipata elimu ya uhakika na itakayomwezesha kushindana, anapata motisha ya kushindana kuingia kwenye ujasiriamali na anakuta kuna mazingira ya kumwezesha kufikia ndoto yake wakati mwingine hapati elimu stahiki na hana fursa ya kuanzisha, kumiliki mali na kuendesha biashara; ni yupi kati yao atakuwa na motisha ya kufanya ubunifu na kutafuta pesa?

Dkt. Hamisi Kigwangalla ni Mbunge wa Jimbo la Nzega, Mkoani Tabora. Amesoma shahada ya kwanza ya udaktari wa tiba, na ana shahada mbili za uzamili, moja kwenye afya ya jamii na nyingine kwenye uongozi. Na sasa anaandika tasnifu ya shahada yake ya uzamivu (Ph.D.) kwenye usawa, haki na uchumi, pia anamalizia kuandika kitabu chake kwenye sera za maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako