Markus Mpangala |
IWAPO Raila
Odinga wa Muungano wa CORD atashindwa kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi
mkuu wa Kenya, basi Uhuru Kenyatta ataapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo. Bahati
mbaya zaidi, suala linalojitokeza sasa ni namna diplomasia ya Kenya
itakavyokuwa hapo baadaye.
Kuna nchi zimempongeza Uhuru
Kenyatta kwa kupata ushindi; Tanzania, Zimbabwe, Afrika Kusini, Rwanda na
Uganda, huku Marekani ikikwepa kutaja jina lake. Si hoja kuu kujadili uamuzi wa
serikali ya Barrack Obama kukwepa kumtaja Uhuru Kenyatta.
Pamoja na hayo Uhuru Kenyatta
na William Ruto wamefunguliwa mashtaka katika Mahakama Kimataifa ya
Uhalifu(ICC). Hata hivyo, kesi yao itaendeshwa mjini Arusha hapa nchini baada
ya serikali kukubali maombi ya ICC kuwa nchi mwenyeji. Mjadala mkubwa uliopo ni juu ya
diplomasia ya Kenya chini ya Uhuru
Kenyatta na William Ruto ambao walikuwa wakiungwa mkono na Mwai Kibaki, huku
Daniel Arap Moi akimuunga mkono Musalia Mudavadi.
Kote Afrika kuna mazungumzo
kila kona wakihoji jinsi Uhuru Kenyatta anavyoweza kuwaumiza wananchi wa Kenya
ikiwemo suala la kuwekewa vikwazo. Kwanza tunatakiwa kutambua
Uhuru Kenyatta alipigiwa kura kihalali na aliingia kwenye mchakato wa kugombea
urais kwa njia halali kabisa baada ya Mahakama Kuu nchini Kenya, chini ya Jaji
Willy Mutunga kutupilia mbali madai ya kuzuiwa kwa wanasiasa hao kugombea
urais.
Uhuru Kenyatta |
Tangu wakati huo kuliibua hofu,
lakini kulingana na siasa za Kenya, ukabila umeshika kasi hivyo makabila ya
Kalenjin na Kikuyu yanaonekana kushinda uchaguzi huu baada ya William Ruto (mkalenjin)
na Uhuru Kenyatta (mkikuyu) kushika madaraka. Hivyo hadi leo diplomasia ya
Kenya inaelekea kuleta mjadala na kudhaniwa kunaweza kutokea mgogoro na nchi za
kigeni hivyo kuhatarisha maisha ya wakenya.
Lakini muhimu ni kufahamu kuwa
Kenyatta alipigiwa kura na wakenya, hivyo ulikuwa uamuzi wao juu ya kumchagua
au kumwacha. Jambo la kuelewa hapa ni kwamba Uhuru Kenyatta anaingia kwenye
nafasi ya urais (iwapo Mahakama haitabatilisha matokeo) akiwa na swahiba wake
William Ruto.
UMOJA
WA AFRIKA vs ICC
Umoja wa Afrika utalazimika kufikiria
zaidi juu ya suala la Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. AU inaendesha Mahakama ya
Haki za Binadamu ya Afrika (African Court on Human and People’s Right), yenye
makao makuu mjini Arusha. Mahakama hii iliidhinishwa
nchini Ethiopia na kugharamiwa na serikali ya Tanzania. Dhumuni la Mahakama ya
ACHPR ni kuwa na Mamlaka ya kusikiliza na kuzitolea uamuzi kesi za makosa ya
Jinai sawa na Mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (uhalifu wa
vita na haki za binadamu) yaani ICC (International Criminal Court) yenye makao
makuu The Hague, Uholanzi.
Mahakama ya Haki za Binadamu ya
Afrika (ACHPR) inaongozwa na Jaji Gerald Niyungeko (Rais wa Majaji), Jaji
Sophia Akuffo (Makamu) Jaji Elsie Nwanuri na Jaji Robert Eno (Msajili wa
Mahakama hiyo). Kwa mujibu wa AU, Mahakama ya
ACHPR itakuwa na mamlaka kamili ya kutolea uamuzi wa; (i). Makosa dhidi ya
Ubinadamu (Crimes against Humanity), (ii). Makosa ya kivita (War Crimes) na
mamlaka yote ya kusikiliza makosa ya Jina.
Aidha, kulingana na uanzishwaji
wa ICC, kuna kesi ambazo zinatolewa uamuzi The Hague, Uholanzi, lakini zinaweza
kufanyiwa uamuzi na Mahakama ya Haki za Binadamu inayofanya kazi barani Afrika
mjini Arusha, Tanzania. Madhumuni ya ICC ni; (i).
kusikiliza makosa ya ukandamizaji (Crime of Genocide), (ii). Makosa dhidi ya
Ubinadamu (Crimes against Humanity), (iii). Makosa ya Kivita (War Crimes),
(iv). Makosa ya Uchokozi (Crime of Aggression), (v). Makosa ya uvunjaji wa
Sheria za Kimataifa.
Mahakama ya ICC ilianzishwa
rasmi mwaka 2002 baada ya makubaliano yaliyofanyika mwaka 1998 kwa kazi
tulizoainisha hapo juu. Kuundwa kwa ICC ni zao la Mkataba wa Roma (Rome Statue)
wa Julai 1, 2002. Kumekuwa na shutuma nyingi dhidi ya Mahakama ya ICC, lakini
sasa bara la Afrika limeamua kujibu mapigo kwa kufanya kweli na kuanzisha Mahakama yao. Mwaka 2009, Mahakama ya ICC
ilianzisha mchakato wa uchunguzi wa uhalifu wa kivita katika nchi za DRC,
Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kenya, Afghanistan, Colombia, Ivory Coast,
Chad na Georgia. ICC iliamua kutoa hati ya mashtaka dhidi ya Rais Omar Al
Bashir kwa madai anahusika na mauaji ya yanayofanyika katika jimbo la Darfur,
Sudan.
Aidha, ICC ilimhusisha Rais
Bashir na wanamgambo wa Janjaweed. Kwa mujibu wa Ripoti yake, ICC ilisema Sudan
siyo sehemu ya Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC kulingana na Mkataba
uliounda Mahakama hiyo), hivyo kiongozi wake (Bashir) hawezi kukamatwa kwa
mfumo wa Mahakama hiyo. Lakini ICC ikasema inachukua
jukumu la kumtia mbaroni Rais Bashir kulingana na uamuzi wa Baraza la Usalama
(United Nation Security Council) Namba.1593 la Machi 31, 2005, kutokana na hali
ya maafa ya jimbo la Darfur. Azimio hilo linalofanya kazi chini ya Sura ya VII
ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) ndilo lilitumiwa na ICC kutaka kumkamata
Rais Bashir kulingana na hali mbaya ya Jimbo la Darfur.
Jean Ping, Mkuu wa zamani wa Tume ya Umoja wa Afrika |
Wanachama 11 waliounga mkono
azimio hilo, halafu China, Algeria na Brazil zikapinga. Hata hivyo, uamuzi wa
ICC unadaiwa kuchochewa zaidi na Marekani ambayo siyo mwanachama wa Mahakama
hiyo, bali ilitumia nafasi yake ya mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama,
na mvuto wa ICC katika hatua zake za kulinda haki za Binadamu. Hivyo kikao cha 111 cha ICC
kikaidhinishwa kukamatwa kwa Rais Bashir. Lakini kwa upande wa nchi za Afrika
kupitia Umoja wa Afrika zilipingana na ICC, huku zikishutumua ICC kuchukua
mkondo wa nchi za kibeberu kuingilia kadhia ya Darfur.
Hati ya kukamatwa Rais Bashir
ilitolewa Machi 4, 2009 haiwezi kutekelezwa kwa namna yoyote kwa mujibu wa AU
hali ambayo ilileta malumbano makali. Malumbano yalichochewa zaidi baada ya serikali
ya Marekani kutangaza kuunga mkono Rais wa Sudan kufikishwa The Hague. Taarifa za serikali ya Marekani
zilitolewa na Robert Wood, Hilary Clinton na mwakilishi wa Marekani nchini
Sudan, Jenerali Scot Gration ambao waliwakilisha maoni ya serikali yao kuhusu
Hati ya kukamatwa kwa Rais Bashir. Awali mwaka 2007, ICC ilitoa Hati ya kukamatwa kwa waziri mmoja wa
zamani wa serikali ya Sudan.
UMOJA
WA AFRIKA ULIVYOMTETEA RAIS BASHIR
Ripoti ya Januari 9, 2012 ilieleza
waziwazi hatua ya ICC kumkamata Rais Omar al Bashir ni batili. AU ilipinga hatua ya ICC kuzishinikiza
nchi za Malawi na Chad kutoa “maelezo” kwanini ziliruhusu Rais wa Sudan, Omar al Bashir kuzitembelea
huku zikifahamu kuwa ICC imetoa Hati ya kukamatwa kwao. AU ilikosoa kwa vipengele vya
sheria iliyotumika na ICC kuzishinikiza kutoa “maelezo” kwa nchi za Chad na Malawi. Taarifa ya AU
yenye Kumb. Namba. 002/2012, iliyojibu taarifa mbili za ICC;- Mosi ni taarifa
yenye Kumb. Na.
CC-02/05-01/09-139, pili; yenye
Kumb. ICC-02/05-01/09-140 Desemba 12 na 13, 2011, inaeleza kwanini
haikubaliani na uamuzi wa ICC.
Lakini ICC ilieleza kuwa hatua za Malawi na
Chad kumkaribisha Rais Bashir ni kukiuka Ibara ya 87(7) ya ICC, pamoja na Baraza la nchi
wanachama pamoja na Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa. Aidha, ICC ilisema Malawi na
Chad zilikiuka Ibara ya 27(2) na 98(1) zilizounda Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu kwa Mamlaka ya Kiongozi wa nchi kutekeleza agizo la ushirikiano na
Mamlaka ya ICC.
Kwa hiyo ICC, ilikuwa ikimshutumu marehemu Bingu wa
Mutharika wa Malawi (Joyce Banda alibadilisha baadaye) na Idrissa Derby wa Chad
wanadaiwa kukiuka Ibara ya 98(1) kwa kutotimiza “agizo la ushirikiano” kwa
mamlaka yao mbele ya ICC. Hata hivyo, Umoja wa Afrika
haukuweza ulisema Malawi na Chad ni wanachama wa AU wapo chini ya Ibara ya 23
(2) ya Sheria (Constitutive Act) ambayo inawataka nchi wanachama kuheshimu na
kuzingatia Sera zinazounda Umoja wa Afrika.
AU ikasema kulingana na Ibara
ya 27(2) ambayo inaelezea taratibu maalumu za uundwaji wa ICC;- kwamba hatua
zozote za kisheria zinazochukuliwa lazima zizingatie nafasi ya mhusika iwe
kitaifa au kimataifa, hivyo mahakama haitakiwa kuingilia suala hilo. Ibara hiyo inajieleza kuwa ni
‘taratibu za jumla za Jinai’ lakini hatua zozote za kisheria hazichukuliwi kama
kigezo cha kumkamata mhusika, vinginevyo kulingana na uhusiano baina ya ICC
dhidi ya mtuhumiwa (Rais Bashir/Uhuru Kenyatta) kama inavyoelezwa kwenye Ibara
ya 98(1).
Ibara hiyo inasema mamlaka ya
jumla, hatuwezi kusema Mahakama za ndani hazijumuishwi, hivyo lazima ICC
inatakiwa kuwa na adabu mbele ya sheria za Kimataifa (Interanational Law
Helsinki Final Act) na sheria za Mahakama ya ndani. Kwa mantiki hiyo, hapa
tunajikuta tukimleta Uhuru Kenyatta ambaye ni mshtakiwa wa ICC, je, atalindwa
na Constitutive Act kama ilivyokuwa kwa Rais Bashir? Labda tofauti iliyopo Kenya ni
mwanachama wa ICC na Sudan sio mwanachama wa mahakama hiyo. Pia Uhuru Kenyatta
ameshtakiwa akiwa mwanasiasa wa kawaida sio mkuu wa nchi kama sheria za Umoja
wa Afrika zinavyoagiza. Ni mtihani kwa diplomasia ya Kenya na Afrika.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako