Na Albert Sanga, Iringa |
Mwishoni mwa
mwezi Februari nilikuwa nikisafiri kutoka wilaya ya Mvomero kuelekea Kilombero
mkoani Morogoro. Nilipofika Morogoro mjini niliingia kwenye basi moja ambalo
linafanya safari zake kati ya Morogoro mjini na Ifakara.
Muda niliokata
tiketi katika basi hilo ilikuwa ni saa tisa na nusu jioni, lakini ndani ya hilo
basi nilikutana na abiria ambao walikata tiketi majira ya saa tatu asubuhi!
Kila abiria aliyekuwa anakata tiketi pale alikuwa akidanganywa muda wa kuondoka
kwa basi husika. Wale waliokata
tiketi saa tatu asubuhi waliambiwa basi lingeondoka saa nne na mimi wakati
ninakata tiketi saa tisa na nusu niliambiwa kuwa basi linaondoka saa kumi
kamili!
Kilomita mbili
baada ya kuondoka stendi kuu ya Morogoro majira ya saa kumi na moja jioni;
kondakta akatutangazia abiria ya kwamba basi hilo halitaendelea na safari ya
Ifakara kwa sababu idadi ya abiria ni wachache. Kondakta akadai kuwa kutokana
na uchache wa abiria tuliomo “haitawalipa” kulipeleka basi huko.
Walichofanya
wakakodi basi dogo na kuamuru abiria tuingie humo. Kwa bahati mbaya sana idadi
ya abiria tuliokuwemo kwenye basi la awali tulikuwa ni wengi kushinda idadi ya
siti za hili basi dogo. Abiria wengi waliokosa siti wakalazimika kusimama
wakati tiketi zao zilikuwa zinaonesha nambari ya siti kwa basi la awali.
Abiria tusio na
makuu ndio tulioingia kwenye basi lile dogo lakini kuna ambao waliwasha moto
kuhusu “uhuni” wa basi lile na wakakataa katakata kubadilishiwa gari eti kwa
sababu ya kusema “hailipi”. Nilimsikia abiria mmoja akisema maneno yafuatayo
kwa hasira na ukali mwingi;
“Kama ingekuwa
basi limeharibika ningekubali, lakini mnaleta uhuni wa kusema eti haitawalipa,
kwani mnavyoomba leseni SUMATRA si mlijua kuna siku mtapata abiria na siku
nyingine mtakosa? Imeandikwa wapi katika leseni ya kuwa abiria wakiwa wachache
katika basi, safari iahirishwe? Nitakufa na ninyi ili niwafundishe adabu muache
kutuonea. Mnadhani watanzania wa siku hizi ndio wale wa zamani wa kuwapelekesha
kama maboga?”
Baada ya kuona
pamekuwa pa moto, wafanyakazi wa lile basi kubwa ilibidi wawavute pembeni wale
abiria waliowasha moto na kuzungumza nao. Sielewi walifikia muafaka gani lakini
abiria wale walishikilia msimamo wa kutoingia kwenye basi lile dogo. Tuliondoka
Morogoro mida ya saa moja kasoro jioni huku abiria wote wakiwa wanalalamika,
kujiapiza na kupiga sana kelele.
Katika siti
niliyokaa ndani ya lile basi dogo kulikuwa na mama mmoja ambae baada ya
kumsalimia alinieleza kuwa anaona sura yangu kama sio ngeni. Nilipomueleza kuwa
huenda aliniona kwenye gazeti la Jamhuri, alishtuka mno na kusema, “Hee, kumbe
wewe ndio Sanga? Wawoo!”
“Kila wiki
nazisoma makala zako” Kisha akauliza kwa hisia kali, “Kwa nini hujawapigia
kelele hawa wahuni (wenye basi) wakati wewe ni mwandishi? Hivi unajua
ungejitambulisha kwao na kuwapiga mkwara, wangeogopa sana na wasingefanya uhuni
waliotufanyia?”
Yule mama
niliendelea kuongea nae njia nzima, lakini kwa swali lake la hisia nilimjibu
hivi, “Wakati abiria wote mlikuwa mkipiga kelele na kulilaani hili basi, mimi
fikra zangu zilikuwa kwa mmiliki wa hili basi. Huko aliko nina uhakika hafahamu
kuwa vijana wake wanamuharibia biashara. Katika masuala kama haya huwa
ninafunga kinywa changu na kusali nikimuombea mjasiriamali mwenye biashara
husika.”
“Kwa sababu ninafahamu
kama mwenye basi hili angekuwepo hapa; asingetumia lugha ya kibabe,
asingeonesha ukaidi na asingekubali kuona jina la basi lake linachafuliwa”.
Nikaendelea kumueleza, “Siwezi kutumia uwezo wangu wa kuandika kwa ajili ya
kuchafua biashara ama makampuni ya wengine hata kama wawe wamekosea vipi.”
“ Ninaamini kuwa
kuwalinda wajasiriamali wenzangu ni eidha kuandika mema yao ama kukaa kimya kwa
makosa yao. Msimamo wa kukaa kimya inapotokea uvurundaji kama wa lile basi
lililotushusha unaweza kuonekana ni kutokuwajibika; lakini sikufichi mamangu;
kabla sijaandika chochote kuhusu biashara ama kampuni yeyote; huwa kwanza
najiuliza hivi:
“Je, hiki
ninachoandika kama ningekuwa ni mimi, biashara yangu ama kampuni yangu
inaandikwa hivi, ningejisikiaje? Majibu ya swali hili ndiyo hutengeneza makala
zangu zote za biashara na uchumi unazozisoma. Nafahamu kuwa viatu vya
ujasiriamali ni vizito; mtu anaweza kukurupuka kukusema vibaya pasipo kufahamu
ikiwa wewe unahusika moja kwa moja ama laa. Nipo makini sana na kalamu yangu”
Mimi nilishuka
Kilombero na yule mama aliendelea na safari yake ya Ifakara, lakini safari ile
ilinipa kutafakari na kuwahurumia wajasiriamali wengi. Nikaikumbuka kampuni
nyingine ya mabasi ambayo siku hizi siioni tena. Wafanyakazi wa kampuni ile
enzi zile ikiwa kileleni iking’aa walikuwa na nyodo kupindukia.
Siku moja
nilikuwa nilikuwa na ndugu yangu mmoja mfanyabiashara aliyepo Tunduma na
tukafika katika ofisi zao kukata tiketi za kwenda Dar es Salaam. Mkatisha
tiketi akatuambia kuwa tiketi zimeisha.
Siku za baadae
nilikuja kuambiwa kuwa wafanyakazi wa mabasi yale walikuwa na mtindo wa
kumtazama mtu mavazi na mwonekano wake kabla ya kumpa tiketi. Ukivaa rafu rafu
hupewi tiketi! Kitendo hiki kilisababisha atu wengi kuhisi wanadharauliwa na
hivyo wakaanza kusambaza maneno mabaya kuhusu mabasi yale.
Kilichotokea?
Kuna wakati basi la watu sabini lilikuwa likiondoka stendi likiwa na abiria
saba tu! Katika mazingira kama haya ambayo unaendesha kampuni ama biashara kwa
hasara haiwezekani ukastahimili katika soko.
Kwenye
ujasiriamali wafanyakazi ni pasua kichwa kweli kweli. Uzembe, ujinga na
upumbavu wa wafanyakazi wengi umesababisha wajasiriamali wengi kutoendelea,
kuyumba ama kufilisika kabisa.
Unaweza kutafuta
mtaji kwa jasho jingi sana na ukaanzisha duka, unamuweka mfanyakazi auze hapo
lakini wengi hawawi waaminifu. Kama ni duka anaweza kuanza kufuja mali ama
kuiba. Shemeji zangu wahehe huwa wanamsemo huu, “Mtu anakuja kuomba kazi akiwa
ananyenyekea na kuweka mikono nyuma, lakini akishapata anaanza kuiweka mikono
mbele na anaweza kukufokea hata wewe bosi wake”!
Kwa hawa
wafanyakazi wazembe jambo baya
kuliko yote ni pale inapotokea hawaheshimu, kuwathamini wala kuwajali wateja.
Wafanyakazi vimeo huwa hawana uchungu na biashara yako, iwe unauza ama hauuzi,
iwe unapata hasara ama faida, hawajali! Wanachojali wao ni mshahara wao
unaowalipa, basiii!
Usiombe biashara
yako ikaingia kwenye tanuri la kusemwa vibya, utajuta. Mathalani, lile basi
liliotufanyia uhuni pale Morogoro kila abiria alikuwa akijiapiza kuwa hatakaa
apande tena lile basi na wengine wakaweka nadhiri ya kuwajulisha ndugu,
marafiki na jamaa zao kuhusu hatari ya basi lile kwamba halifai kupandwa.
Unategemea nini kwa majaliwa ya kampuni ile kama sio kushuhudia kupungua kwa
abiria wanaopanda mabasi yao?
Kama hili
tumeshalifahamu ya kuwa wajasiriamali tuna hatari ya wafanyakazi wazembe
kutufilisi, Je, tufanyaje? Kulalamika haitatusaidia! Kusema tumuachie Mungu ni
uzembe! Kuendelea kuvumilia ni kujirudisha nyuma! Tupende ama tusipende wajasiriamali tunalazimika kuchukua
hatua za makusudi za kutuwezesha kuwa na wafanyakazi bora watakaojenga biashara
pamoja nasi na sio wale wanaobomoa.
Nilichogundua ni
kuwa wajasiriamali wengi hatujui namna ya kuajiri pamoja na namna ya
kuwafundisha wafanyakazi. Wengi wetu huwa tunazoazoa bora wafanyakazi. Na
kinachotuponza ni kupenda vya dezo. Tunapenda kuwabeba ndugu zetu wa karibu
bila kujali ubora wao, ili mradi tu tuwe tunawalipa kidogo ama kutowalipa kabisa.
Fikiria wewe
unamiliki basi ama duka halafu unamuweka ndugu yako asiye na uwezo wala vigezo
vya kufanya kazi kwa ustadi, unategemea nini? Sana sana ataanza kujitukuza na
kujiona yeye ndie kila kitu katika biashara husika. Hata majigambo yake kwa
wengine itakuwa ni cheo chake cha undugu kwako.
Inabidi ufike
wakati ambapo mjasiriamali unapiga hesabu za biashara yako halafu unatafuta
wafanyakazi wa kiwango na vigezo kuhimili biashara yako. Hakuna maana ya kusema
eti unabana matumizi ya kuwalipa watu mishahara ilhali unaelekea kufilisika.
Nimewahi kueleza
namna ya kuwatendea wafanyakazi tunaowaajiri katika makala iliyokuwa na kichwa,
“Mjasiriamali na Sayansi ya kuajiri”. Mara zote nimekuwa nikiwatahadharisha
wafanyabiashara na wajasiriamali kuepuka mtego wa kuwa wadhulumaji kwa
wafanyakazi wao.
Mara zote
mfanyakazi unaemuajiri katika biashara zako huwa anafahamu kiwango cha faida
unayozalisha. Kitendo cha wewe kumlipa kiduchu kinazalisha sumu mbaya sana.
Matokeo yake ni kukuibia, kupoteza morali wa kazi na hatimaye kuwavuruga wateja
wako.
Nihitimishe kwa
kuwasihi wajasiriamali kuwa makini tunapoajiri watu katika biashara zetu kwa
sababu wengine wanaweza kugeuka mawakala wa shetani kutufilisi. Niwatakie kila
raheri katika mapambano makali ya kiujasiriamali
stepwiseexpert@gmail.com , 0719 127
901
No comments:
Post a Comment
Maoni yako