April 04, 2013

DARASA HURU: CCM KAENI CHONJO NA JULIANA SHONZA NA MTELA MWAMPAMBA

Daniel Gingo

Kuna wakati ukiangalia siasa wanazofanya Juliana Shonza na Mwampamba (na hasa Mwampamba) wanachofanya sio siasa, wanachokifanya ni utoto! Tena unaweza kudhani kwamba inawezekana CHADEMA walipumua baada ya hawa jamaa kuondoka huko.

Niliwahi kusema kwamba utoto wanaoufanya sasa hivi utakitokea puani CCM, kama baadhi yenu hamtaki kuniamini kwa kudhani kwamba nina chuki na CCM basi mimi na ninyi tunyamaze kwa sasa, tusubiri wakati ukifika utasema.

Kwa Juliana mpaka kesho sijui kilichomtokea, namfahamu kama dada aliyekuwa akimpenda na kumtumikia Mungu kule Mabibo, kilichotokea kwake sikijui, BWANA AJUA!

KWA MFANO WAULIZENI MASWALI HAYA:
1. Kama wakiwa CHADEMA walikuwa wakijua njama zote za mauaji zilizokuwa zikipangwa au kutekelezwa na CHADEMA nini kiliwafanya washindwe kuinuka na kusema kama kweli walikuwa wazalendo kwa Taifa hili? Kwa nini waje waanze kutoa tuhuma hizo leo magazetini na mitandao kama humu?

2. Kama walijua njama za uhalifu zilizokuwa zikifanywa na CHADEMA na wakaficha ‘uovu’ huo ni vipi leo watashindwa kuficha uovu wa CCM pindi utakapofanywa? Nini kitawazuia kuficha madudu ya CCM dhidi ya wananchi wa Tanzania?

3. Katika njama na mikakati ya ‘uovu’ ya CHADEMA wao walishiriki kiasi gani na kwa kiwango gani? Je, ni kweli hawakushiriki mipango iliyotelekezwa? Nini kiliwafanya wajiondoe huko huku wakijua kuwa walishiriki kupanga njama hizo? Je, walikosa walichoahidiwa?

4. Kama waliweza kuwasiliti wenzao wa CHADEMA na leo wanakuja kuwaanika hadharani, watuambie kwa nini tusiionye na kuitahadharisha CCM kukaa chonjo na vijana hawa? Kama waliwasaliti CHADEMA na leo wanafichua siri ambazo walishiriki wote Nape Nnaye ana uhakika gani kwamba nay eye hatakuja kuumbuliwa siku za mbeleni?

MWISHO
a. Narudia leo kuionya CCM, iwe macho na vijana hawa, na sio CCM tu, hata vyama vingine kwa ajili ustawi wa Demokrasia nchini, viache kushabikia watu wanapoacha vyama vyao na kuja kuwa mavuvuzela kwenye vyama vipya!
b. Sina uhakika kama CHADEMA haijawatuma vijana hawa kuivuruga CCM, lakini mashaka yangu ni makubwa juu ya hilo.

MANABII MNAO, LAKINI HAMUWASIKILIZI!!!!

No comments:

Post a Comment

Maoni yako