Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba, Angellah Kairuki amewataka
wanachama wa kikundi cha waandishi wa habari cha kujikomboa kiuchumi (Habari
Group) kupendana na kuaminiana ili kukifikisha kikundi hicho mbali.
Kairuki ambaye pia ni mlezi wa Habari Group, alikitaka
kikundi hicho kutokuwa wachoyo wa kusaidia waandishi wa habari wengine wenye
nia ya kuungana na kufanikiwa kimaisha.
Akizungumza na kikundi hicho Dar es Salaam juzi, alisema ili
mtu afanikiwe ni lazima awe mwenye upendo na kusaidia wengine pale penye mwanya
wa kufanya hivyo na kuwataka wanachama wote kuwa na moyo wa kujitolea kwa ajili
ya kikundi. "Sitopenda
kusikia kikundi hiki kimekufa kwa sababu ya mifarakano na chuki miongoni mwenu
kwani kwa kufanya hivyo hamtofikia malengo mliyokusudia," alisema Kairuki.
Aliongeza kuwa
wakati anaingia madarakani aliweka vipaumbele kwa wafanyakazi wa majumbani,
madereva wa aina zote, wafanyakazi wa mashambani, wahudumu wa baa na nyumba za
wageni, walinzi na waandishi wa habari.
Na kwamba ameanza kushughulikia haki mbalimbali za makundi hayo, ambapo
kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kuishinikiza serikali kusaini mkataba wa
kuridhia haki za wasichana wa majumbani.
Aliwapongeza waandishi wa habari kwamba pamoja na changamoto
nyingi wanazokutana nazo, lakini hawakati tamaa na wamekuwa wakifanya kazi yao
kwa moyo mmoja na kwa bidii.
Kama mkakati wake wa kuwasaidia waandishi wa
habari, alisema atasimamia Habari Group ili wawe mabalozi wazuri kwenye mambo
mbalimbali kwa jamii, ikiwemo kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali, kuwapa elimu
ya umuhimu wa cheti cha kuzaliwa, sambamba na kushirikiana nao bega kwa bega
kwenye mambo muhimu ya kijamii.
"Kuwasidia kwenu ni miongoni mwa malengo yangu
niliyojiwekea ya kupigania haki ya baadhi ya makundi ambyo nimeona haki zao
kama wafanyakazi hazitekelezwi,"aliongeza.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako