April 04, 2013

MGODI UNAOTEMBEA: WAMEAMUA KUIWEKA TANZANIA KIKAANGONI.

Kambi Mbwana, Dar es salaam

KABLA ya kuanza kufikiria labda kuna mkono wa mtu au Taifa kutoka nje ya nchi yetu, vyema tukaelewa kuwa siku zote mvunja nchi ni mwananchi mwenyewe, hasa kwa kuangalia jinsi baadhi yao wanavyokosa uzalendo kwa kutenda vitu visivyokuwa vya kiungwana.

Watu hao wamekuwa wakiendeleza kufanya vitendo vya kushangaza na kuogopesha kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni njia moja wapo inayolitangaza Taifa letu vibaya nje ya nchi.

Tangu kupata Uhuru uliopatikana kwa harakati za viongozi wetu, akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wapambanaji wengine, Tanzania ilijipambanua kuwa ni kisima cha amani.
Katika kulinda msingi huo, wananchi walielimishwa au kupewa kauli mbiu ya namna gani wanavyotakiwa waishi kwa ajili ya kuishi kwa amani na upendo ili kukuza uchumi wa nchi yetu.
Ni kweli kabisa. Kiu hiyo ilidumu kwa miaka mingi, ingawa sasa naanza kuona kuwa hali hiyo imekwisha. Anayesema kuwa nchi hii bado ni kisiwa cha amani, hakika anatumia lugha nzuri kwa kuhofu anayewaeleza hivyo wataondoa woga kwa sababu moja ama nyingine.
Kwanini nasema hayo? Taifa letu sasa lipo kwenye matatizo makubwa ya vurugu za kidini, siasa na mambo mengine ambayo yote kwa pamoja yanawaweka wananchi kwenye wasiwasi mkubwa.

Kumekuwa na matukio mengi ya kutisha. Katika kulielezea jambo hilo la machafuko ya Tanzania, wengi watawataja watu maarufu au wale ambao matukio yao yamegusa watu wengi. Lakini ukweli ni kwamba hao wanaotajwa ni wachache kati ya wengi ambao labda kwa kutokuwa maarufu kwao, au kutojulikana kwa madhira yaliyowakuta, kunawafanya wasionekane yale yaliyowatendewa.

Ingawa watu watawataja watu kama vile Mwandishi Daudi Mwangosi, mtu aliyepoteza maisha kwa staili ya kutisha kupita kiasi. Mbali na Mwangosi, bado wapo watu kama vile Daktari Stephen Ulimboka, Mhariri wa Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006 (Ltd), Absalom Kibanda ambao matukio yao ya kutekwa na kuteswa yamewagusa watu wengi na kuendeleza msemo kuwa Tanzania sasa si kisiwa cha amani.

Mbali na watu hao, ambao kwa mapenzi ya Mungu wameendelea kubarikiwa uhai, wapo ambao wamepoteza maisha, akiwamo Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Visiwani Zanzibar. Padri huyu aliuagwa na kuibua hisia nzito sambamba na kuzidi kueneza chuki kwa miongoni mwa jamii ya Kitanzania. Pamoja na yote hayo, bado wapo wananchi ambao wamekuwa wakiishi bila kuvumiliana kwa sababu za ajabu, hasa huu wimbo wa kuchinja unaoendelea kuimbwa kwa lugha za chuki na kukiathiri kizazi cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tangu kuzaliwa kwa Taifa hili, likipita katika vipindi tofauti kwa viongozi tofauti waliokuwa na mapenzi makubwa kwa wananchi wao, watu waliishi kwa upendo na kuvumiliana kupita kiasi. Si kama ukatili haukuwapo, huenda ulikuwapo, ila si kama ulivyokuwa sasa kiasi cha watu kushikwa na mihemko na kutenda bila hata kuogopa vyombo vya Dola katika mazingira wanayotaka wao.

Hii si njia nzuri ya kuzalisha amani kwa Watanzania. Zaidi tunaendeleza chuki, fitina, majungu na kusababisha sumu mbaya ya vurugu ambazo kuna siku zitashindwa kumalizwa.
Katika kutafuta nufumbuzi juu ya machafuko ambayo mengi huibuka kwa kupita mgongo wa dini na siasa, baadhi ya watendaji wa serikali, wanashindwa kutumia busara, hekima na utu juu ya kumaliza migogoro hiyo.

Kuna siku tutashuhudia watu wakiingia barabarani kufanya uhalifu, maana tayari walishazoea na kuona kuwa hakuna wa kuwazuia kwa namna moja ama nyingine.
Katika kuliangalia Taifa lenye amani, hatupaswi kuchekea kauli za uchochezi zinazotoka kwa mtu yoyote, iwe ni mwanasiasa au kiongozi wa dini ambaye hana uzalendo na wananchi wake. Huo ndio ukweli. Mihemko yako haiwezi kutufanya tuone upo sahihi hata pale utakaposimama kwa kupitia cheo chako cha kidini au kisiasa kuhamasisha vurugu hatari kwa Taifa hili.

Hatuwezi kwenda hivyo. Bado hatuna uchumi unaotufanya tulinge kuwa tutakuwa pazuri hata kama baadhi ya watu watafanya vurugu, wataharibu miundo mbinu yao kwasababu ya kuhamasisha ujinga kutoka kwa mtu mmoja asiyekuwa mzalendo. Kwa mfano, wapo watu ambao wanabishana juu ya nani yupo sahihi katika suala zima la kuchinja. Sakata hili lilibuliwa na Waziri Stephen Wasira, alipokuwa anazungumza jijini Mwanza.

Mengi yaliendelea kuibuka hasa pale Wasira alipojikuta akitoa ufafanuzi kuwa mwenye mamlaka ya kuchinja ni Waislamu. Kauli ya Wasira isingeleta matatizo kama watu watatumia akili na uzalendo kufuatilia suala hili. Kuna uwezekano mkubwa kuwa huenda Wasira amezungumza hivyo kwasababu ndio utaratibu uliozoeleka kwa Watanzania wengi. Hata wachungaji, mapadri walikuwa wakitaka kufanya shughuli inayoshirikisha watu wa jamii tofauti, vitoweo vyao vilikuwa lazima vichinjwe na Waislamu.

Pamoja na yote hayo, watu ambao ni jamii ya Wakristo hawakulazimishwa pia wachinjiwe na Waislamu kama hawajaona hilo linafaa, ingawa tatizo litakuwa pale wanapochinja wao na kuwalisha wengine. Kumbe leo wapo watu wanaotaka wachinje, basi sakata hilo linastahili viongozi wakae na kushirikisha makundi ya kijamii hasa kwa viongozi wao wa dini, Mashekhe, Mapadri na wengineo.

Wakati hayo yakiendelea, watu wanahoji. Je, vurugu hizo mwisho wake ni wapi? Ingawa wapo wanaosema kuwa vurugu hizi zina mkono wa mtu, wakimaanisha watu wanaotumiwa na wengine kutoka nje ya nchi, lakini bado hainifanyi nishindwe kuwataja watu hao kama majuha na wasiokuwa na uzalendo katika Taifa lao.

Watu hao ambao lengo lao kubwa ni kuiweka nchi katika mtihani mzito, hasa katika kiu ya kuilinda amani yake, hawastahili kuchekewa hata mara moja, maana wanavyoendelea kuchekewa, ndivyo sumu hiyo inavyozidi kuenea na kuota mizizi hata kwa wale wasiokuwa na tabia hiyo.

Kila mtu wakiwamo viongozi wa serikali, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa upande wa Bara na Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wa Visiwani kuendelea kuwa wakali kwa kundi lolote, mtu yoyote anayefanya uvunjifu wa amani kwa makusudi kwa faida anayoijua mwenyewe.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe kuwa vinakuwa mstari wa mbele, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kulinda amani na mustakabali wa Tanzania.

Leo tunaona ni kawaida, lakini ikiendelea hivi, kila mmoja ataona ana uhuru wa kufanya kila analotaka, hivyo kusababisha machafuko, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, hasa tatizo hilo linapopitia kwa mlango wa dini au vyama vya siasa, kama vile Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine vya siasa vilivyosajiliwa katika nchi yetu.

Huu ndio ukweli wa mambo. Tusipokuwa makini, kujua nini cha kufanya kwa ajili ya nchi yetu, hakika hatutakuwa na kizazi chenye uzalendo, kinachoithamini amani kwa ajili ya kulinda utu na heshima za watu.

Tuna wajibu wa kulijua hili, maana inapotokea machafuko makubwa, wanaoathirika ni akina mama na watoto, hivyo ni wazi hawa wanaofanya vitendo vya unyama kwa wenzao, wale wananaokesha kubuni namna ya kufanya vurugu za kidini na kisiasa wafikie wakati waone imetosha kwa ajili ya kuendeleza wimbo wetu wa Tanzania kisiwa cha amani.

MAONI: kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment

Maoni yako