August 11, 2013

IMANI YAKO INAAKISI FEDHA UNAZOMILIKI


 Na: Albert Sanga, Iringa

Nafahamu kuwa wengi kama sio wote tunakubaliana kuwa fedha zina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya mtu, tunachotofautiana ni imani kuhusu fedha. Mitazamo kuhusu fedha ndio inayoamua kiwango cha fedha alichonacho kila mmoja. Hii ina maana kuwa kila mtu anamiliki kiwango cha pesa sawa sawa na imani ama mtazamo wake kuhusu fedha.

Kimsingi ni kwamba zipo imani zinazosapoti watu kuwa na fedha za kutosha na zipo imani na mitazamo inayozuia watu kuwa na fedha ama inawafanya waishi maisha ya kupungukiwa nyakati zote! Imani na mitazamo hii kimsingi huzalishwa kutokana na  malezi, utamaduni na mazingira. Mtazamo wa mtu kuhusu fedha tunaita, “Money blue print” (Kila nitakapotumia neno hili la kimombo litakua limebeba maana hii)

Mathalani, ukiwa mikoa ya Nyanda za juu kusini kuna mivumo, ‘myths’ kuhusu kabila la Wakinga (bahati nzuri na mimi ni Mkinga). Watu wengi kutoka kabila hili wanasifika sana kwa kufanya biashara na matajiri wengi katika mikoa hii ni Wakinga. Pamoja na sifa hii, Wakinga wanatajwa kuwa ni mabingwa wa kutumia ushirikina katika biashara zao.
Hivyo utabaini kuwa kwa mtu anaewatazama wakinga na utajiri wao, akiamua kuchukua ‘myth’ hii; basi ataunganisha fedha na uchawi. Hii itakuwa kichwani kwake kwamba, ili uwe na fedha nyingi (tajiri) ni lazima uwe mchawi na hii ndio itakuwa, ‘Money blueprint’ yake.

Mfano mwingine unawahusu rafiki zangu Wachaga. Wapo watanzania wengi ambao wanaamini mchaga yeyote anayetajirika ni lazima awe ametumia wizi ama udhulumaji. Kwa watanzania wenye  mtazamo kama huu, ni wazi kuwa wanapoitazama fedha wanaiunganisha na wizi ama udhulumaji. Kwao hawa hii ni ‘blue print’ yao.

Ukiiangalia mifano hiyo yote miwili utabaini kuwa  ni mitazamo inayozuia mtu kuwa na fedha nyingi (hata kama mwenye mtazamo huo akiwa hajijui). Na hii ni kwa sababu watu wengi hawapendi uchawi, hawapendi wizi na wanauchukia ujambazi. Kwa kuwa wameunganisha fedha na uchawi, wizi na ujambazi, ‘automatically’ wataichukia fedha bila hata kujijua ikiwa wanaichukia fedha! Matokeo ya chuki zao dhidi ya fedha yanadhihirika katika kiwango cha fedha wanazomiliki. (Nakuthibitishia eidha wanakuwa ni masikini ama ni watu wenye kuhangaika milele kwa kupata fedha isiyowatosha-hata kama wawe ni wenye vyeo vikubwa!).

Ingawa mtu kuwa na fedha nyingi sio kipimo cha utajiri  lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu aweza kusema ni tajiri ikiwa hana fedha (hata kama iwe katika maumbo mengine). Kwa maana hii tukiongelea fedha kwa namna moja ama nyingine tunakuwa tukiiunganisha na utajiri (ingawa kuna watu hawataki kabisa kuwa matajiri-hawa nao blueprint zao ndivyo zinavyowaelekeza!).

Kiuhalisia ni kuwa utajiri ama umasikini wa mtu haupo katika wingi ama uchache wa mali au fedha anayomiliki. Tofauti kubwa iliyopo kati ya masikini na matajiri  ni ile ya kifikra. Masikini huwaza kimasikini, tajiri huwaza kitajiri. Utajiri ama umasikini wa mtu huanzia katika fikra na mitazamo yake.

Kwa mfano, fikra za kitajiri  huamini kuwa ukiwa na fedha ya kutosha utaishi kwa furaha, amani na upendo kwa wengine hivyo utatimiza agizo la Mungu kuwa mpende jirani yako kabla ya kumpenda Mungu. Fikra za kimasikini zitajinenea hivi, “sio vizuri kuwa na fedha nyingi, kwa sababu hautampendeza Mungu”

Kama alivyosema, Mchungaji Pepe Minambo kutoka Kenya ndivyo na mimi ninavyoamini kuwa ni vigumu kwa masikini kuingia mbinguni. Sababu za uwezekano wa masikini kuikosa Mbingu zipo wazi; kwanza masikini ni mlalamikaji na mnung’unikaji (na Mungu hapendi walalamishi na wanung’unikaji), masikini ana wivu na masikini hajiamini.

Msomaji usisahau kuwa hapa siongelea masikini wa roho aliowasema Yesu Kristo, ila naongelea masikini wa fikra chanya. Ni vema tukafahamu kwamba, tajiri huwa tajiri kabla hajamiliki kitu na masikini huwa masikini kabla ya kudhihirika kwa hali yake; kwa vile umasikini na utajiri vyote ni matokeo ya kuwaza.

Vile vile nigusie kundi maarufu sana la uchumi wa kati “middle class”. Hawa ni watu ambao hawana fedha nyingi na wala sio masikini kabisa. Kundi hili ni sumbufu sana kifikra na ndilo ambalo husambaza fikra hasi kuhusu fedha. Kundi hili, hupenda kuridhika mapema na hupendelea sana usalama “comfort zone”.

Kinachosikitisha zaidi  ni kwamba kuna wanasiasa wanadai kupigania uwepo wa watanzania wengi katika kada hii ya watu wa kati; wakati mfumo na uchumi wa dunia unawafuta kwa kasi kubwa. Mfumo wa uchumi wa dunia uliopo (na utakaoendelea kuwepo kwa  mamia ya miaka ijayo) unawabeba watu wa aina mbili tu, masikini na matajiri.

Ni ama uchague kuwa masikini au uchague kuwa tajiri. Kazi ni kwako msomaji kama unaamini na kutamani kuwa mtu wa kada ya kati. Kwa wanaofuatilia duru za kiuchumi kwa umakini hawashangazwi na hali iliyopo ya matajiri kuendelea kuwa matajiri na masikini kuzidi kuwa mafukara, sio Tanzania tu lakini ni katika dunia nzima.

Kwa  kuwa ninaongelea kuhusu imani kuhusu fedha ni vema nikagusia imani iliyochimbika miongoni mwa baadhi ya wakristo. Katika Biblia kumekuwa na maandiko ambayo, tafsiri (nasisitiza kuwa ni tafsiri kwa sababu Biblia ipo ‘perfect’) zake zimekuwa na ‘Money blue print’ ambazo hazisapoti mtu kutafuta na kunia kumiliki fedha. Nitataja maandiko mawili; la kwanza ni lile lisemalo, “Huwezi kumtumikia Mungu na mali” na la pili ni lile lisemalo, “Kupenda fedha ni shina la maovu yote duniani”.

Si kusudio langu kuhubiri (ingawa nina karama ya kuhubiri pia) lakini nifafanue kidogo kuhusu maandiko hayo. Neno mali (ama Biblia zingine zimeandika fedha) limetafsiriwa kutoka katika neno ‘Mamos’ linalomaanisha ‘roho inayotawala mali’. Kwa maana hii, kimantiki ilitakiwa kueleweka kuwa, “Huwezi kumtumikia Mungu na roho inayotawala mali”.

Kuhusu fedha na maovu ninachoamini ni kuwa ikiwa pesa itatumika vibaya itazalisha maovu na ikiwa itatumika vema inaleta tija. Ni kama kisu kilichopo jikoni, kinaweza kukata mboga na kinaweza kutumika kuua ama kumdhuru mtu. Kusema kisu ni chanzo cha ‘mauji yote ya jikoni’ itategemea umeangalia upande upi wa matumizi!

Kwa upande wa malezi na utamaduni wetu nako kumezalisha imani na mitazamo mingi iliyo hasi kuhusu fedha. Kwa mfano; jamii zetu zinaamini kuwa wanaume ndio wanastahili kuwa na fedha kuliko wanawake. Ndio maana mwanamke anapotajirika migogoro hutokea ikilinganisha na mwanaume anapotajirika.

Wanawake wengi waliomatajiri utasikia habari kuwa  ama hajapata kuolewa, ama aliolewa akaachika ama ndoa aliyonayo ina mgogoro mkubwa. Unajua tatizo linapoanzia? Nitaeleza hapa chini, lakini kabla nataka niseme jambo hili; imani  ya jamii kuhusu fedha ndio husababisha wanawake wanaotajirika kuonekana kuwa hawapo sawa.

Katika familia nyingi watoto wanapokua, huwa kuna mazoea ya kuomba fedha kwa mama. Mama zetu mara nyingi tukiwaomba fedha huwa wanasema kauli kama hii, “Msubiri baba yako, akija ndio atakupa fedha”. Kinachojengeka katika akili ya mtoto ni kuamini kuwa, wanawake hawana na hawastahili kuwa na fedha! Hii ni ‘Money blueprint’ hatari sana na imechangia sana wanawake wengi kuwa nyuma kujitafutia fedha na pengine kutajirika.

Kutoakana na ‘blueprint’ hii ndio maana huwa sishangai ninapoona mabinti wakijiorodheshea vigezo vya wanaume wanaowataka; katika vigezo hivyo hawaachi kuweka, ‘mwenye kazi nzuri (moja kwa moja atakuwa na fedha)’, ‘mwenye fedha za kutosha’, ‘aliye maarufu (umaarufu kwa kiasi fulani huleta fedha)’ na vigezo vya kufanana na hivyo.

Zipo imani na mitazamo mingine mingi ambayo imewaathiri watu wengi bila kujijua na imesababisha kuishi katika maisha ya uchache badala ya utele wa kifedha. Kwa mfano wapo watu ambao wanaamini kuwa haiwezekani watu wote tukawa matajiri. Wanachosahau kujiuliza ni hiki, “Ni wapi imeandikwa kwamba wewe fulani, bin fulani utakua masikini?” Kama dunia inaendelea kuzalisha matajiri, kwa nini usiwe mmoja wao na badala yake unajivisha haki ya umasikini?

Wapo watu wengine ambao wanaamini kuwa matajiri ni mabahiri; kwao hawa utajiri ni ubahili na wengine wanajiridhisha kuwa fedha haiwezi kununua furaha. Ukweli ni kwamba matajiri wengi wana nidhamu ya matumizi ya fedha (ndio maana wanazidi kutajirika) na uhalisia ni kwamba ingawa fedha sio kigezo pekee cha mtu kuwa na furaha lakini siku za masikini hutawaliwa na huzuni kutokana na kutopata anavyovitaka. Kupata unachokitaka ni moja ya mihimili ya furaha. Na mtu una uwezekano wa kupata unachokitaka kwa sehemu kubwa ikiwa utakuwa na fedha

Msingi mwingine wa kupata fedha (na mafanikio mengine yeyote) ni kuzingatia kile unachokipenda na sio kile usichokipenda (focus on what you want and not on what you don’t want). Hii inatokana na kanuni mbili za kiubongo na kiasili; ambazo ni hizi(Nitatumia kiombo kidogo).

Kanuni ya kwanza inasema“What you focus expands-yaani unachozingatia hukua” na ya pili inasema “Your eyes will see what your mind has prepared to see-macho yako yataona kile ambacho fikra zake zimejiandaa kukiona”. Iko hivi, ukitaka fedha zingatia utele (namna ya kuongeza fedha) na usizingatie uchache (kuishiwa, kufilisika)!

Nihitimishe makala haya kwa kudurufu mambo machache.  Mosi ni kuwa kila mtu anayo nafasi  sawa (equal channce) ya kuwa na fedha za kutosha kumpa uhuru wa kiuchumi. Pili hakuna raha wala sifa ya kuendelea kuwa masikini, kwa sababu masikini ni mzigo kwa dunia. Masikini na umasikini wake hata awe ni mtakatifu na mwema kiasi gani ni kwamba anaitesa dunia (kwa sababu anahitaji kusaidiwa). Tajiri (ama niseme mwenye fedha za kutosha) hata kama ni mchoyo ama bahiri bado ni msaada kwa dunia (kwa sababu anajisaidia).

Pamoja na haya yote, sio kusudio langu kuwabeza masikini na tena sio kusudio langu kuwataka watanzania wote wawe matajiri (japo ikiwa hivyo nitafurahi pia-manake nami nitakuwa mmoja wa matajiri); lakini ninataka kila mmoja apokee changamoto  ya kutamani kuwa na uhuru wa kifedha na kiuchumi. Na hili linawezekana ikiwa mitazamo na imani za wengi kuhusu fedha zitabadilika na kuwa zinazosapoti badala ya kuvuruga nafasi ya mtu kupata fedha.

Kila mtanzania anastahili ushindi wa kifedha!

0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com


No comments:

Post a Comment

Maoni yako