August 11, 2013

UNAWEZAJE KUZALISHA FEDHA ZA KUTOSHA?


Na, Albert Sanga, Iringa
Wiki iliyopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa, “Imani yako inasadifu fedha zako”. Kama ilivyo ada nimepokea mirejesho mingi kwa baruapepe, simu za miito na jumbefupi. Wasomaji wamekuwa na mitazamo tofauti tofauti wengine wakiipongeza makala ile na wengine wakionesha dukuduku.
Pia wapo  wachache wamepinga kabisa uthubutu wangu wa kuchambua fedha katika sura ambayo wanadai nahamasisha watu kutafuta fedha. Hawa ni wale ambao wanaamini “fedha si nzuri kwa sababu inaharibu tabia za watu”
Nilivutiwa sana na mchango wa msomaji mmoja kutoka Arusha aliyeniandikia baruapepe ifuatayo, “Bw. Sanga nakupongeza sana kwa makala zako. Unaandika ujasiriamali na mambo ya kujitambua in unique style kiasi kwamba kila ninaposoma makala zako napata ladha na impact kubwa mno. Kwenye makala yako ya leo umeeleza vizuri mno kuhusu imani za fedha”
“Loo! Makala hii imenisaidia na kuniokoa mno kwa sababu nimekuwa na kawaida ya kushiriki gossiping kuhusu wenye fedha. Mfano hili la kuamini kuwa kuna makabila yanafanikiwa kwa sababu ya wizi ama ushirikina nimekuwa ninaamini pasipo kujua kuwa ninaathiriwa na imani hizo”.
“Hata hivyo Bw. Sanga ninaomba unisaidie nawezaje kuzalisha fedha za kunitosha? Kwa sababu mimi ni mwajiriwa lakini kadiri siku zinavyoenda ninaona majukumu yanaongezeka na mshahara naona hautatui mahitaji yangu vizuri, maisha ni magumu, nikitafiti naona biashara karibia zote zimeshafanyika, Je, nitafanya kitu gani ama namna gani ili niweze kuzalisha fedha? Narudia tena kukupongeza na ninaamini utanisaidia katika hili” Mwisho wa kunukuu.
Katika makala haya leo ninajibu swali la msomaji huyu aliyeniuliza, “Nawezaje kuzalisha fedha za kunitosha?” Hata hivyo kabla sijaeleza namna gani mtu unaweza kuzalisha fedha za kukutosha, ninapenda kueleza kidogo kuhusu dukuduku walilokuwa nalo baadhi ya wasomaji kuwa fedha siyo nzuri kwa sababu zinaharibu tabia za watu.
Kimsingi fedha imebeba chembechembe nyingi za kisaikolojia zenye uwezo mkubwa wa kuamsha tabia za mtu hata zile ambazo hazijapata kuonekana. Mtu mchoyo akipata fedha uchoyo wake unaongezeka na unakuwa dhahiri. Mtu mwema na mtoaji akipata fedha wema wake huongezeka na ataonekana akitoa zaidi na zaidi.
Kwa jinsi hii tunaona kuwa kimsingi fedha haibadilishi wala kutengeneza tabia ya mtu isipokuwa fedha hudhihirisha tabia na hulka aliyonayo mtu ambayo alishakuwa nayo hata kabla hajaipata fedha. Fedha naweza kuifananisha na mfumo wa mashine za sauti “Amplifier”.
Kwenye “Amplifier” ukitoa sauti yako kama ni sauti mbaya ubaya huo utakuzwa na kama sauti yako ni nzuri basi uzuri wa sauti yako utakuzwa vile vile. Kwa kuwa fedha zina mfumo wa kukuza tabia, ni vema sana mtu akatumia muda na rasirimali maarifa kujenga tabia na hulka zake ili fedha inapokuja isilete mushkeli.
Na ninapotaja habari ya mtu kuwa na fedha isidhaniwe kuwa ninagusia fedha nyingi sana, la hasha! Watu tunatofautiana sana linapokuja suala la mitazamo na hulka zetu katika fedha. Wapo watu ambao akiwa na elfu kumi tu mfukoni lazima ujue kwa maana ataleta vurugu na maujiko kibao.
Mtu mwingine akiwa na hiyo shilingi elfu kumi mfukoni haoni kama ana fedha, isipokuwa anaweza hata kukueleza kuwa “sina fedha kabisa”. Kwa mwingine milioni moja sio fedha wakati kwa mwingine milioni moja ni utajiri!
Kinachofanya mtu mmoja aone kuwa elfu kumi ni fedha na mwingine aone kama si fedha inatokana na mtazamo wanaokuwa nao watu hawa katika fedha. Mtazamo huu hauanzi pale mtu anapoishika hiyo elfu kumi, isipokuwa ni kuwa mtazamo wao ulishajengeka mapema kabla hata ya kushika hiyo fedha.
Baada ya kusema hayo sasa nigeukie upande mwingine kulijibu swali la msomaji Yule, “Je, nawezaje kuzalisha fedha?”. Kwa wale wenye kumbukumbu bila shaka wangali wanaikumbuka makala niliyopata kuiandika wiki chache zilizopita iliyokuwa na kichwa, “Tumeamua kuichuuza thamani ya fedha yetu”.
Katika makala hiyo nilieleza kwa kina dhana na maana ya fedha, lakini pia nilisema fedha sio mafanikio zikisimama peke yake; isipokuwa fedha ni matokeo ya mtu kufanikiwa. Fedha inatakiwa kumjia mtu baada ya kuzalisha thamani fulani katika uchumi. Hapa tunaangalia maeneo kadhaa zinakopatikana fedha.
Kunapotokea mdororo wa uchumi, mara nyingi mitaani huwa tunasema fedha zimepotea,!  fedha hazionekani,! Kitu cha kujiuliza ni “Je, fedha zinapopotea ama kutoonekana zinakuwa zimepotelea wapi?” Ukweli ni kuwa fedha zote zilizopo duniani zinazunguka miongoni mwa watu. Idadi ya fedha huwa haipungui, ila kinachopungua ama kuongezeka ni thamani ya fedha.
Ukiwa na fedha leo na kesho ukawa huna basi ujue fedha zipo kwa watu. Kwa maana hii ukitaka kupata fedha ni lazima uzitafute kutoka kwa watu.  Fedha zinapatikana kutoka kwa watu. Je, unazipataje fedha kutoka kwa watu?
Watu katika maisha ya kila siku wanakabiliwa na changamoto na matatizo mbalimbali. Unapochukua wasaa wa kutatua changamoto na matatizo yao ni lazima utapokea ujira wa utatuzi wako. Hii ina maana kuwa wakati wote ikiwa unahitaji fedha ni lazima uwe ni mtu unaetazama matatizo na changamoto kama fursa za kukusaidia kupata fedha.

Tunaposikia kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira; kuna makundi mawili ya watu yanayolitazama hili kwa mitazamo tofauti. Mosi wapo wale wanaosimama upande wa kulalamika na wakitazamia kuhurumiwa. Ni vema wasomaji mkafahamu siri hii: kihisia, fedha ni kama ina masikio, haitaki malalamiko haitaki manung’uniko!
Ukizoea kulalamika na kunung’unika ovyo unaifukuza fedha! Lakini ukichunguza upande wa hawa walalamishi na wanung’unikaji sana; utagundua kuwa wengi wao huamini kuwa kushindwa kwao ikiwemo kiuchumi(kifedha) ni matokeo ya uzembe ama kutokuwajibika kwa wengine.
Kundi la pili ni wale wanaofikiri namna ya kuikabili na kuitatua changamoto hii. Ndani ya kundi hili la pili ndimo wanakopatikana wale wanaoamua kujiajiri lakini ninaowakusudia zaidi hapa ni wale wanaowasaidia wengine kujiajiri. Hawa ni kundi la watu wanaoamua kufanikiwa katikati ya matatizo na changamoto.
Ndio maana ukichunguza kwa umakini utabaini kuwa, watu wanaofanikiwa katika jamii zetu katika maeneo mbalimbali (ikiwemo kifedha) huwa wako “bize” na mambo yao, hawana muda wa kulalamika wala kunung’unika ovyo. Wanaofanikiwa mara zote huwa hawawanyooshei vidole watu wengine kutokana na kushindwa kwao. Wanaofanikiwa huamini kuwa wanawajibika kwa sehemu kubwa katika mafanikio yao.
Kwa kuwasaidia wengine kuweza kujiajiri kundi hili hufanikiwa kujipatia fedha. Unapotatua changamoto ama tatizo lolote kiubunifu ni lazima unufaike. Tunatakiwa tufahamu kuwa matajiri wote duniani wameupata utajiri wao kwa kutatua changamoto na matatizo waliyoyabaini miongoni mwa watu. Fedha zinapatikana kwenye matatizo na changamoto
Tunapoangalia kuwa fedha zinapatikana kwa kutatua changamoto na matatizo tunajiuliza, Je, unawezaje kutatua hayo matatizo na changamoto? Jibu lipo hivi: Ili kutatua tatizo ama changamoto ni lazima ubuni bidhaa na huduma zinazojibu matatizo na changamoto hizo. Watu walipoonekana wanatembea peku na kuhatarisha afya zako, alitokea mtu akabuni viatu.
Mpaka leo tunawalipa wanaotengeneza viatu. Baada ya kuona watu wanahitaji kusafiri kwa haraka na kwa ufanisi, walitokea waliogundua ndege na hadi leo tunawalipa watu mbalimbali wanaofanikisha usafiri huo kila tunapotaka kusafiri. Kila bidhaa unayonunua ama huduma unayolipia unatakiwa kutambua kuwa ni matokeo ya ubunifu wa wajasiriamali uliochagizwa na changamoto na matatizo waliyaona miongoni mwa watu.
Wapo wajasiriamali mbalimbali ambao wamechangamkia fursa zilizotokana na ukosefu wa ajira na sasa wameanzisha makampuni yanayotoa huduma za kiushauri na kimafunzo kuwawezesha watu kujiajiri. Hivyo tunaona kuwa eneo jingine ambako fedha zinakaa ni katika bidhaa na huduma
Njia rahisi ya kubuni  bidhaa na huduma zitakazowavutia wengine kukuletea fedha ni kutumia karama na vipaji vyako. Kama wewe ni mwimbaji, ukiimba nyimbo nzuri moja kwa moja utauza nakala na utatumbuiza katika matamasha. Kama wewe ni daktari mwenye uwezo na kipaji kikubwa cha kutibu kwa ustadi, ni lazima watu watakuja kupata huduma na kukuletea fedha. Ndani ya karama na vipaji ndiko zinakopatikana fedha.
Kitu ambacho tunatakiwa kuepukana nacho ni mawazo ya kupata fedha za mkato-mkato. Shida ya fedha za mkato-mkato kama ufisadi, wizi, utapeli, udokozi na uhujumu; sio ile hatari ya kukamatwa na kufungwa jela; isipokuwa zipo hatari kubwa zaidi ya hapo ambazo ndizo ambazo mimi daima huzitambulisha.
Ukifanya ufisadi kazini na ukajipatia fedha kasha ukajenga majumba na kuanzisha miradi lukuki, hata usipokamatwa usidhani upo salama! Kuna kitu kinaitwa hukumu ya moyoni “Spiritual Condemnation” ambacho kinaweza kukutesa sana. “Spiritual Condemnation” ni hatia anayokuwa nayo mtu kwa ndani kutokana na njia alizotumia kupata fedha zake.
Hili la madhara ya kutafuta  fedha na mafanikio kwa njia zisizohalali linahitaji makala ya peke yake. Hata hivyo kitu cha kufahamu na kuamini ni kuwa inawezekana kupata fedha na utajiri kwa njia halali; huna sababu kupita njia za mikato zitakazokutesa unapofanikiwa.  Nihitimishe kwa kusema kuwa inawezekana na tena ni rahisi kuzaisha fedha ikiwa tutajizoesha kuyafuatilia na kuzingatia maeneo niliyoyataja ambako fedha zinapatikana!
Ni haki ya kila mtanzania kuwa na fedha za kutosha

No comments:

Post a Comment

Maoni yako