Na,
Albert Sanga, Iringa.
Nawasalimu wasomaji wote, pia ninawapongeza na
kuwashukuru wale wote ambao wamekuwa wakiwasiliana nami. Mbarikiwe. Itakumbukwa
kuwa huko nyuma nimepata kuandika makala iliyokuwa na kichwa, “Naiona Afrika
ikiinuka tena”.
Katika makala ile
nilieleza kwa sehemu namna Afrika
ilivyoanza kuzinduka na leo katika makala haya (na zitakazofuata kila
nitakapopata wasaa wa kuchambua uchumi wa Afrika) nitaeleza namna Afrika
ilivyoanza kutembea katika mstari wa mafanikio ya kiuchumi, kijeshi na kijamii
pasipo kuwategemea akina “bwana mkubwa” kutoka ng’ambo.
Nauona umuhimu wa
kuyachambua haya ili kwamba Waafrika wote tujitambue, kujikubali, na kisha
tujenge ari ya matumaini na fikra za ushindi sasa na kwa vizazi vijavyo.
Tumejikunyata vya kutosha, na sasa ni wakati wetu kutamba duniani!
Kwa miaka mingi sasa
kila neon Afrika linapotajwa huwa linaunganishwa na migogoro ya kivita, mabaa
ya njaa na magonjwa, umbumbumbu na ulafi wa watawala, umasikini na ufukara
uliopindukia, mikosi, laana, kuonewa pamoja na harufu ya jehanamu.
Waafrika wengi
tulijiona katika picha hiyo (nab ado wengi wanajiona hivyo), lakini vile vile
dunia imekuwa ikiiona Afrika kwa jinsi hiyo hiyo. Mengi yameandikwa sana kuhusu
Afrika, mengi yamesemwa, mikakati mingi kutoka nje ya Afrika imekuwa ikifanyika
(kwa madai) ya kuliokoa bara hili ambalo wakati fulani wazungu waliliita kuwa
ni bara la giza.
Wanazuoni mahiri kutoka
duniani waliibuka na nadharia na falsafa kedekede zinazoonesha kuwa Afrika
imefika katika hali mbaya kwa ajili ya ukoloni. Namkumbuka Walter Roodney namna
alivyoandika kitabu kiitwacho, “How Europe underdeveloped Afrika” ambapo katika
kitabu hicho ameeleza namna Ulaya ilivyocheza karata zake kuimaliza Afrika.
Wengine wakaja na mwanya wa kisayansi wakieleza
kibaiolojia.
Hawa wakadai kuwa Waafrika
wana genetiki zilizoumbwa kushindwa (unsuccessful genetic codes). Hawa
wanamaanisha kuwa umasikini na matatizo ya Waafrika ni matokeo ya kukosewa
kuumbwa! Yaani waafrika waliumbwa kushindwa (Programmed to fail). Haiishii
hapo; kwani wapo wachambuzi wa Biblia ambao husema kuwa Waafrika ni kizazi
kilicholaaniwa na Mungu ndio maana, kila kitu hakifanikiwi ndani ya Afrika.
Hizo ni sababu chache
kati ya nyingi zilizoelezwa na kuendelea kuaminika kwa miaka mingi. Kimsingi
kila nadharia, falsafa na sababu inayoelezwa kuhusu kukwama kwa Afrika
inaonekana kuwa na usadifu Fulani wenye mashiko; kiasi kwamba kila nadharia
imejipatia wafuasi wengi. Bahati mbaya ni kuwa nadharia na falsafa zote zinaua
uwezo wa Mwafrika kujikwamua na zinaendelea kuwafanya Waafrika waamini kuwa wao
sio sehemu ya wanadamu kamili katika hii dunia.
Hata hivo wale
tunaoifuatilia historia ya Afrika kwa macho ya uchanya, tunaona sababu za
Afrika kupita ilikopitia lakini pia tunaona Afrika inakoelekea. Ni kweli kuwa
Afrika imepita katika mkondo wa vita, umasikini, majanga, kutengwa, kuonewa na
kudharauliwa; lakini wasaa wa Afrika kujikwamua umewadia nao unaendelea
kutokea. Afrika inaumbika kwa upya!
Ninaposema Afrika
inaumbika upya, ni vema tujikumbushe historia ya nguvu za mataifa katika dunia.
Kimsingi mataifa tajiri na yenye nguvu yamekuwa yakipanda na kushuka huku
nafasi zao zikichukuliwa na mataifa yanayoibuka. Ukiyachunguza mataifa ambayo
huibuka na kuyapiku yale mataifa makubwa; mara zote huwa yametoka ama yamepitia
kwenye matatizo makubwa, ikiwemo umasikini mkubwa, vita ya wenyewe kwa wenyewe,
kuonewa na mengine niliyoyataja hapo juu.
Tunapoitazama China
tunaona kuwa kwa miaka zaidi ya 20 ilikuwa ikielea katika ujamaa ulioonekana
kama umepoteza mwelekeo lakini baada ya hapo imeibuka kwa kasi sana kiasi
kwamba sasa inaitishia nafasi ya Marekani kiuchumi na kijeshi.
Nchi ya India nayo kwa
miaka mingi ilihaha kwa umasikini mkubwa lakini ndani ya miaka 4 hadi 10 neema
ikaitembelea na sasa uchumi wake unastawi kwa kasi mno. Hata Brazil huko zamani
ilikuwa ikiogelea katika lindi la umasikini lakini kwa sasa ni moja ya nchi
zinazopanda kwa kasi katika ustawi wa viwanda duniani.
Zamani yale mataifa
saba tajiri (Marekani, Uingereza,
Ufaransa, Ujerumani, Italia, Canada na Japan) yalijiona kama miungu mtu
duniani, yakajiandikia haki ya kuitawala dunia katia kila jambo kuanzia uchumi,
nguvu za kijeshi na kijamii.
Siku zilivyokuwa
zinaenda yakabaini kuwa wanachoamini ni “kujilisha upepo” kwani kuna maaifa
ambayo yanapanda kiasi kwamba ustawi wa chumi zake ni mzuri kuliko wao
wanaojiita G-7. Hapana shaka kwamba nchi
hizi zilikuwa zikijionea haya kujiita tajiri wa matajiri ilihali kuna matajiri
wakubwa kupita wao
Baada ya mvutano na
mjadala mwingi; kwa shingo upande yakasalimu kujibadilisha jina kutoka G-7 hadi
G-8 ambapo walilazimika kuliongeza taifa la Urusi. Haikuishia hapo kwani
mataifa haya yakabaini kuwa matatizo ya kiuchumi ya dunia hayawezi kumalizwa na
wao pekee hivyo wakaona ni wasaa wa kutengeneza umoja utakaoyatabua mataifa
mengine ambayo yanazidi kuongezeka kila kona. Hii ikawa ndio sababu ya dunia
kupata kinachoitwa G-20.
Ukiacha ngazi ya uchumi
wa mataifa, tunaporudi katika chumi za mtu mmoja mmoja (micro economics)
tunaona pia mambo yakibadilika. Kwa miaka nenda rudi taifa la Marekani ndilo
limekuwa likitoa binadamu tajiri kuliko wote duniani. Lakini miaka ya karibuni
binadamu tajiri kuliko wote ametokea taifa la Mexico, taifa ambalo miaka kadhaa
nyuma lilikuwa kwenye orodha ya nchi za ulimwengu wa tatu
Nini maana ya mambo
haya? Ni hivi: mambo yanabadilika na yanabadilika kwa kasi sana. Taifa lenye
nguvu leo haimaanishi kuwa litakuwa na nguvu milele. Matajiri kwa sasa
wanapatikana kutoka nchi zote, za ulimwengu wa kwanza na za ulimwengu wa tatu.
Pia ukweli ni kuwa
mataifa mengi yanaanguka moja kwa moja na nafasi zao zinazidi kuchukuliwa na
yale mataifa ambayo yalidhaniwa kuwa ni madogo na manyonge kabisa. Mataifa
makubwa sasa yanatoa jasho!
Haya mabadiliko
yanayoipata dunia hayajaliacha nyuma bara la Afrika. Mwanga wa matumaini
unazidi kuonekana Afrika. Afrika imeanza kujitambua, imeanza kuamka, imeanza
kusimama na kimsingi itasimama moja kwa moja na kuitawala dunia, kiuchumi,
kijeshi na kijamii.
Hili jambo sio “habari
ya maono ya rohoni” isipokuwa ni mtiririko (trends) na mahesabu yajayo
(forecast) kutokana na yale yaliyotokea Afrika, yanayoendelea kutokea na Afrika
inavyojipachika (reposition) katika “mdundo wa mabadiliko”.
Kabla ya mwaka 1950
Karibu Afrika nzima ilikuwa ikitawaliwa na makoloni isipokuwa nchi chache tu.
Baada ya mwaka 1950 bara la Afrika lilipatwa na mfumuko wa ukombozi, ambapo
makumi ya nchi zilianza kujipatia uhuru wake miaka ya 60 hadi 80.
Ifahamike kuwa
kilichofanya nchi nyingi za Ulaya ziachie makoloni ni kuyumba kwa chumi zao
kiasi kwamba wakawa hawana tena jeuri ya kuendesa makoloni hasa baada ya vita
ya pili ya dunia. Mataifa haya ni kwamba yalilazimika kuyaachia makoloni kwa
shingo upande.
Msomaji napenda ushike
hapa: Afrika haikupata Uhuru kwa bahati mbaya ama kwa hiari ya walioitawala;
isipokuwa ilipata uhuru kwa sababu ya kuyumba kwa chumi za walioitawala”. Kisosholojia
na kiimani tunasema uhuru wa Afrika ulikuwa kama ujio wa nguvu za Mungu kwa
Afrika baada ya kutawaliwa kwa miongo mingi. (First God’s Visitation to Africa).
Bahati mbaya ninaweza
kusema kwamba Afrika iliuchezea ujio wa mara ya kwanza wa Mungu! Hii ni kwa
sababu baada ya nchi nyingi kujipatia Uhuru, wale viongozi wa kwanza na
wapigania uhuru wengi wao walijisahau. Badala ya kuwatumikia wananchi
wakajikuta wanalewa madaraka, wakawa walafi na mafisadi na idadi ya kutosha
wakageuka kuwa madikteta ghafla.
Huzuni ilitanda upya
Afrika pale ambapo, viongozi kutoka mataifa mengi yaliyopata uhuru; waliporudi
kuwapigia magoti wakoloni. Badala ya kubuni mikakati ya kujitegemea wakawa
kiguu na njia kwenda kuomba misaada kwa wale wale waliowatawala. Mataifa mengi
yakageuka kuwa tegemezi na mengi yao hadi leo hayana jeuri ya kujitegemea
asilimia mia moja kiuchumi, kijeshi na kijamii. Hata hivyo hali haijabaki vivyo
hivyo hadi sasa; kwani mambo yanabadilika mno Afrika.
Tuonane wiki ijayo
katika sehemu ya pili ya makala haya. Waafrika ni wakati wetu wa kung’aa
kiuchumi
0719
127 901, stepwiseexpert@gmail.com
No comments:
Post a Comment
Maoni yako