January 04, 2018

SALAMU KUTOKA MBAMBA BAY, ZIWA NYASA

Honorius Mpangala
..Niko Mbamba Bay katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa hususani Idara ya Elimu. Kuna changamoto ambayo wanaipata wakazi wa Wilaya ya Nyasa, nawashangaa sana wale wanaosema kuna usawa wa utoaji wa huduma kati ya Mikoa na Wilaya. Hii keki haigawiwi sawa.

Miundombinu ya Barabara mibovu, eneo la mlima wa Malongo, Kata ya Kihagara ni korofi na sumbufu miaka nenda rudi. Ukifika baadhi ya maeneo ya kijiji cha Chinula ukorofi wa mlima Malongo nao uko vilevile. Mvua ikinyesha tu ni shida hata pikipiki kupandisha mlima haiwezekani. Utelezi uko eneo kubwa sana la Mlima Malongo na kijiji cha Chinula.

Mawasiliano ya simu katika ukanda huu licha ya simu yangu ya Philips analogia kuweza kutumika maeneo hata yale ambayo ni tata lakini huku kwetu nasalimu amri kwani yako maeneo watu hata karatasi la Vocha lilivyo hawalijui. Yako maeneo hata maana ya vocha hatujui. Tunahitaji sana kuwa na mawasiliano stahiki lakini tunaona wanasiasa mnazidi kuwadanganya wananchi.

Kesho Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakuwepo Mbamba Bay, sasa kwa mikwara ya wanasiasa na watu wao wa idara tofauti naona wako bize sana na shughuli zao. Hata barabara kwa kutoka Ndengele hadi Mbamba Bay inarekebishwa, huu ndo ujinga wa wale ambao tunawapa dhamana huwa wanafanya jambo wanapoona kuna ugeni wa kitaifa, ndipo hutumia nguvu zao zote na kuhaha huko na huko.

Nisiwalaumu sana hawa kwani hata Dar es salaam watu walideki barabara wakati wa ziara ya Rais wa Marekani, Barrack Obama alipokuja Tanzania. Kuna aliyewaroga wapiga kura kwani wanaamini maendeleo ni kupitia boksi la kupigia kura.

Honorius Mpangala
4/1/018
Mbamba Bay

No comments:

Post a Comment

Maoni yako