December 21, 2012

WAZIRI MKUU AAHIDI KUCHANGIA SH. 25M/- ZA JENERETA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameahidi kuchangia gharama za ununuzi wa jenereta kwa ajili ya kata ya Majimoto wilayani Mlele mkoani Katavi ili waweze kuwa na umeme wa uhakika.
Alitoa ahadi hiyo jana mchana (Jumatano, Desemba 19, 2012) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Majimoto kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya saba ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
“Kuna wafanyabiashara wa hapa Majimoto ambao walikuja kuniona na wakasema wako tayari kuchangia ununuzi wa jenereta lenye uwezo wa kutoa kilovoti 60 za umeme kwa nyumba kama 300. Wao watoe milioni 25 wakiwa tayari na mimi nitatoa milioni 25... jaribuni mkae na kupanga namna ya kuchangia gharama.”
“Baada ya muda fulani mtakuta mmemaliza kuchangia, tuwarudishie wafanyabiashara hela yao ili hilo jenereta liwe la kijiji. Mkilipata, nitawasiliana na TANESCO ili watupatie nguzo za umeme,” alisema.
Akijibu hoja kuhusu viwanja, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi alisema upimaji wa viwanja ulifanyika miaka miwili iliyopita na vikapatikana viwanja 270 lakini hadi sasa havijagawiwa kwa wananchi. Aliwataka viongozi wa kata na wilaya wasimamie zoezi hilo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya juu ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara kando ya barabara kuu. ” Ninawasihi sana mheshimu sheria za barabara... msijenge nyumba zenu ndani ya hifadhi ya barabara.
Kesho (Ijumaa, Desemba 21, 2012) Waziri Mkuu atakwenda kata ya Usevya ambako atazindua mradi wa umemejua (solar power) kwenye sekondari ya kata ya Usevya na kuhutubia wananchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 20, 2012.

1 comment:

  1. I am sure this post has touched all the internet people, its really really pleasant paragraph on building up new
    web site.
    Also visit my web-site :: reduce acne

    ReplyDelete

Maoni yako