January 08, 2013

RAIS FRANCOIS BOZIZE ALIKUWA AKISUBIRI VITA ATIMIZE MAJUKUMU?


Na. Markus Mpangala, Lundu
Moja ya mambo yanayonikinaisha ni suala la mgogoro wa nchi ya Afrika ya Kati.
Serikali ya Bangui inaonekana lilala usingizi wa pono kiasi ambacho sasa baada ya mapigano ya muda mrefu na waasi wameamua kuitisha majadiliano huku serikali ya rais Bozize ‘ikiwatongoza’ waasi hao kwa mambo ambayo yaliapaswa kuwa kwenye ilani ya uchaguzi. 
Serikali ya mjini Bangui chini ya rais Francois Bozize inasema kuwa, kwa sasa imejipanga kwa dhati kutimiza majukumu yake kwa wananchi.
Serikali hiyo inasema katika majadiliano yake na waasi wan chi hiyo yatakayofanyika nchini Gabon, imekusudia kuwasilisha mipango thabiti ya maendeleo ya kiuchumi, mapenndekezo imara ya mabadiliko ya ndani ya jeshi la nchi hiyo na kadhalika.
Ikumbukwe Rais Bozize hivi karibuni alimtumua madarakani waziri wa ulinzi ambaye ni mtoto wake. Kwa upande wa waasi wan chi hiyo wanasema kuwa wanataka rais Bozize aondoke madarakani ili kurejesha amani ya nchi hiyo. Mazungumzo baina ya serikali na waasi yanafanyika baada ya miaka takribani miaka 12 ya kukosekana kwa amani, huku utawala wa Bangui ukiendelea kulemaa na kushindwa kutimiza makubaliano ya awali ya mwaka 2001.
Katika mazungumzo ya sasa, Jumuiya ya Nchi za Afrika ya Kati(CEEAC) imeratibu majadiliano baina ya Rais Bozize na waasi hao yatakayofanyika mjini Libraville nchini Gabon yakiwa na lengo la kumaliza mapigano ya pande hizo mbili.
Moja ya masharti yaliyowasilishwa na waasi ni kwamba lazima rais Bozize aondoke madarakani kwasababu ameshindwa kupata ufumbuzi na kutimiza makubaliano yaliyowahi kufikiwa huko nyuma.
Aidha, mwaka 2007 kulifanyika mazungumzo ya kusaka amani lakini hakukuwa na mwendelezo wowote uliofanyika chini ya rais Bozize. Ni jambo la aibu sana leo hii, Rais Bozize kuamua kuwasilisha mezani ajenda za kupata ufumbuzi ili kumaliza machafuko nchini mwake. Leo hii Rais Bozize anawasilisha mipango ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Afrika ya Kati, huku akihimiza mabaidliko ya kijeshi ndani ya jeshi la nchi hiyo.
Kimsingi Rais Bozize anaonekana kukosa dira ya kuongoza taifa hilo lililopo katikati ya bara la afrika. Sababu mapigano yake dhidi ya waasi yanafahamika kwa kipindi cha miaka kumi sasa, na ajenda zinazoelezwa na waasi ni hali mbaya ya wananchi, kukosekana wka matumaini ya kiuchumi na kadhalika. Lakini kwa upande wa Rais Bozize haonekani kuona kwamba yeye anaweza kuwa kikwazo cha kufikiwa makubaliano hayo.
Waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Kama ambavyo waasi wamesema, wanataka kuona Rais Bozize akiondoka madarakani ili kupata ufumbuzi, vivyo hivyo wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanavyopendekeza.
Hata hivyo kwa mtindo wa kutaka kukwepa majukumu, ni dhahiri rais Bozize anaweza kuwatupia lawama wasaidizi wake ili kuonekana hana hatia. Ni sababu hii ndio maana alimfukuza kazi mwanaye ambaye alikuwa waziri wa ulinzi na usalama wan chi hiyo.
Kumfukuza kazi waziri huyo hakukuweza kuwashawishi waasi wa nchi hiyo ili waone rais huyo anakusudia kuleta mabadiliko, bali waasi wanaona ni njia ya kujisafisha kwa sasa kutokana na kuachia machafuko kufikia kipindi kibaya sana.
Jambo jingine ni mabadiliko ya taratibu za uchaguzi wan chi hiyo. Ikumbukwe, waasi hawalalamikii taratibu za uchaguzi uliomuingiza madarakani rais Bozize bali wanalalamikia hali mbaya inayotokana na utawala wake. Kwa maana hiyo kutaka kufanya mabadiliko katika taratibu za uchaguzi anakusudia kuwaleta waasi hao katika ulingo wa siasa badala ya kuangalia njia za kukomesha mapigano ambayo yamesababisha watu kadhaa kufariki dunia na wengine kukosa makazi.
 Katika hali kama hiyo kwa vyovyote uchumi wa nchi lazima uzoroteshwe, kwani watu badala ya kutumia nguvu zao katika uzalishaji hivyo hutumia nguvu hizo matika kuyakimbia makazi yao au kuelekea uhamishoni. Sio kitu rais ambacho rais Bozize anaweza kuishawishi Afrika, lakini jambo la msingi ni kukubali kuwajibishwa kulingana na hali halisi inayoendelea nchini humo.
Wananchi wanapolalamikia hali mbaya ya kiuchumi huku rais wao akitumia muda mwingi na nguvu za kutosha kutaka kuwashawishi waasi waache mapigano, ni wazi ameshindwa kubaini kwua hata yeye ni sehemu ya tatizo la machafuko hayo.
Endapo yeye asingekuliwa sehemu ya tatizo basi tusingeona leo kuna machafuko yanaendelea nchini humo na tungeona serikali ya Bangui ikisifika kwa wananchi wake kutokana na juhudi za kuboresha na kuimarisha uchumi wake. Nadhani ni wakati wa Rais Francois Bozize kung’atuka madarakani, hivyo ikibidi kuitisha uchaguzi mkuu ambayo utashirikisha vyama vyote vya siasa na wananchi wa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako