January 08, 2013

WATANZANIIA TUNAWEZAJE KUISHI KWA GHARAMA KUBWA KILA MWEZI?


Na Yasinta Ngonyani, Sweden
Fikiri, matumizi nyumbani:- chakula, umeme, gesi, maji, soda au juisi za wageni. Ada za watoto zinazolingana na za vyuo vikuu. Na hapa nazungumzia ada za shule za binafsi sio zile za serikali  kwani tunajua unafuu wake. Matumizi mengine matibabu hospitalini, pesa ya walinzi kwa kila mwezi, sherehe za kuaga na kukaribisha mwaka mpya.
Zaka ya Kanisani na Misikitini, kupanda Mbegu/ Sadaka, Shukurani ya neno, ahadi na makusanyo, shukrani ya chakula cha Bwana kanisani, marekebisho ya Kitasa cha mlango kabla mwenye nyumba hajashtuka, gharama za marejesho ya mkopo wa Saccos kazini.
Tozo za Flying (wazoa takataka wa mikokoteni ambao huzitupa hapo hapo), Madalali wa nyumba, viwanja, pango la nyumba, fremu ya biashara na ofisi.
Mitandao ya simu (airtime vouchers), mafuta ya gari, walindaji na waoshaji magari. Daima kauli zao “oyaah sista/blaza, mdogo wako nipo apaaa.”
Tozo za kuegesha magari, makato ya mikopo, tozo za internet cafe ili uweze ku-surf. Rambirambi ya mfiwa mtaani kwetu, harusi ya ndugu yako wa ukoo na zawadi.
Bado sijamaliza kutaja, kuna Sendoff ya mtoto wa mdogo wake rafiki yako na zawadi, kumuaga mfanyakazi mwenzetu na zawadi, michango ya komunio ya 1 & 2 na kipaimara.
Michango ya birthday party na zawadi; Ndugu wa kule kijijini, mshahara wa hausigeli na hausiboi; matumizi ya Bodaboda, teksi na bajaji. Duka la dawa kwa mchaga, tuisheni ya mtoto, kuchangia wahanga wa mabomu na mafuriko. Mengine ni kwenda kumuona mtoto aliyezaliwa, kununua CD/DVD ya uzinduzi wa Kwaya yetu.
Chakula cha mbwa, mchango wa ujenzi wa kupanua Kanisa, kuchangia Uinjilisti Masasi, outing ya kitimoto, ujenzi wa Nyumba Mabwepande, Kuendeleza shamba Mkuranga (linalotaka kutaifishwa kwa kutoendelezwa). Na matumizi mengine kwa wale wenzetu wanaokwenda umbali wa Viti Virefu, moja moto, moja baridi. Maji ya Trafiki, Chai ya Nesi na Daktari, Kahawa ya Hakimu, Karani na PP.
Matumizi ya Vishoka waunganisha maji na umeme; Kidogo dogo cha mjumbe na mtendaji wa mtaa, makaribisho ya get together na dinner kwa rafiki wa kikazi ambaye hamjuani ila kweye simu tu.
Mchango wa matibabu ya mtoto nyumba ndogo kule Ngusero, mchango kidogo kwa rafiki aliyevamiwa na vibaka na kuumizwa vibaya. Gharama za malipo ya Mkulima Bar Moshi, manunuzi ya maji ya Kilimanjaro uwanjani Sheikh Amri Abeid, Ukiangalia mechi ya Yanga na JKT Oljoro, malipo kwa ajili ya Uji wa Shangazi, baada ya kazi Njiro jioni ya Alhamisi. Vipi manunuzi ya kandambili kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Hivi hali inakuwaje?
Mia mbili ya watoto wa mtaani au ombaomba, kitu kidogo cha wale wanaolazimisha kuosha kioo cha gari kwenye foleni barabarani. Umeme uliopanda bei, gesi iliyopanda bei, maji yaliyoadimika, bado contingency maana huu usafiri unaotembelea ball joint, bush, feni belt havijafa, hapo bado hujafanya service. Bado msosi wa mchana kazini hasa kama maofisi yetu akina Mama Ntilie na vyakula vyao vinapokaribiana bei za restaurants, bado mchango wa kitchen party na sare, kuna hii baby shower.
Na hapo bado hujatoa watoto outing jumapili, Upo wapi uwezekano wa kununua laptop mpya ambayo ni muhimu katika mfumo wa maisha ya kisasa. Desktop nyingine kwa ajili ya watoto nyumbani, rim mpya za gari ambazo zimeingia kwaajili ya ku-modernize gari lako kuu kuu. Vipi kuhusu gharama za kujipendekeza kwa kimwana wa kazini kwako ambaye amekubali kwenda nawe out leo.
Gharama za matibabu katika hospitali binafsi kwa kuwa madaktari wa serikali wapo katika mgomo. Dogo naye “Bro ninunulie basi japo kasimu ka promosheni, ile yangu imedondoka chooni” Mara “Bro/Sister Next week on Saturday shuleni tuna-visit snake Park na sina shilingi 3000 za mahudhurio”.
Mke naye nyumbani anaongeza yake, “Daddy leo Mwakasege yupo relini, vipi tutapitia? Hapo unatakiwa kujua kichwani mwako kuwa gharama ya taxi baada ya semina.
Vipi tozo za Toyo kwa kuwa nimeachwa na gari la ofisi (Staff Bus). Mwingine kama kawaida anakusubiri uwajibike kwa gharama zako hana muda wa kudhani unahitaji msaada. Mama yangu!
Ukigeuka huku na huko unajikuta nafuu yenyewe ni pale mwajiri anapokuongezea mshahara kwa 7% tu wakati inflation ni juu ya 19%. Ukifikiri kwa makini, unajiuliza Watanzania wanaishi vipi kwa mtindo huu?
Ndipo unapoimba "Mwokozi nitoe roho niepuke, hili balaaa." Napenda msomaji utafakari mwenendo wako wa matumizi kulingana na hali hali ya uchumi wan chi na jamii yetu.
Kama ukiyumba kwenye suala la kuweka akiba, basi maisha yako yatakuwa yanakabiliwa na ukosefu wa msingi wa muongozo au utakuwa unatumia gharama kubwa kwa mambo yasiyoweza kusaidia familia yako.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako