January 23, 2013

SAKATA LA GESI LIMEZUA JIPYA MKOANI MTWARA-Mgodi Unaotembea


Kambi Mbwana

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

HALI ya mkoani Mtwara ni dhahiri inatishia amani, hivyo kuna kila sababu ya serikali na wadau wote kukaa na kuliangalia suala hilo kwa marefu. Nikiwa kama Mtanzania, nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mno sakata hilo la gesi inayopingwa na wadau kuletwa jijini Dar es Salaam, badala yake wanataka ibaki mkoani Mtwara, ingawa wenye akili ndogo wanapinga au kutukashifu kadri ya uwezo wao, wakijidanganya kuwa sipaswi kufuatilia mambo ya Mtwara na Lindi.
Huu ni udhaifu na hauwezi kuchekewa, maana ni dhahiri Mtwara, Lindi ni sehemu ya Tanzania kama ilivyokuwa Tanga, Arusha, Kilimanjaro na kwingineko. Wananchi hao waliojikusanya kwa ajili ya kupigania sakata hilo, wamefikia kubadilisha kabisa hisia zao, bila woga wowote katika kulizungumzia suala la gesi.
Kama nilivyowahi kuhoji hapo nyuma, kuwa tatizo ni gesi, choyo, siasa au ubaguzi? Makala haya yalitoka katika blog hii ya Handeni Kwetu na kupokea maoni mbalimbali. Na haya ndio maoni ya Watanzania hao wanaoishi mkoani Lindi na Mtwara. Mwanzo wa ugaidi Tanzania ni mwisho wa amani. Kusini hawaogopi jeshi. Kauli ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ipo kwenye mioyo yao. Leo nasema, ila wana Mtwara watasema kwa sauti zao, maana vitisho kwao ni kama kuitukana maiti.
Chochote kitatokea iwe ni vita vyovyote vile 2015 hatutaki uchaguzi na hatutaki pia tuletewe kiongozi na ole wenu, +255712897794
Maandamano Mtwara
Kaka nimefurahishwa na makala yako isemayo Tatizo ni ni gesi, siasa, choyo au ubaguzi? Inaonekana na wewe pia umeandika makala hii kwa lengo lako binafsi. Umeshindwa kutoa uhalisia wa jambo lenyewe, badala yake umeandika kwa lengo la kutaka kumfurahisha ama kuwafurahisha watu fulani. Rudi nyuma angalia wanachofanyiwa wakulima wa korosho wa Mtwara je ni sahihi? Lile zao halisaidii kuinua pato la Taifa? Angalia hali ya maisha ya wakazi wa Mtwara. Nadhani umekurupuka na si mawazo yako kuna mkono wa mtu nyuma yako.
Nenda kazunguuke na kufanya utafiti wa kina utapata majibu sahihi kwa wenyeji. +255657614354.
 Tatizo la mikoa ya Kusini sio gesi bali ni kusahauliwa kwa miaka 51 ya Uhuru. Korosho, reli, Bandari, miundo mbinu, tatizo la elimu na kuwa waanga wa ukombozi wa nchi zilizopo kusini mwa Afrika.
Wanasiasa kujiingiza katika hoja si ajabu kwasababu duniani kote wanasiasa ndio huibua matatizo ya wananchi , maana wasomi wetu wengi hawana meno ya na ndio wanaopitisha  mikataba mibovu .
Sio choyo, lakini tunafikia wakati tunajuta kwa nini sisi Mtwara Lindi tumekuwa sehemu ya Tanzania. Tuna rasilimali tosha za kuweza kuitwa, kama vile Bandari, Bahari, Ardhi yenye rutuba, watu, mito, madini, korosho, ufuta, mhogo na nyinginezo. Kusini tuna haki ya kumdai mume wetu Tanzania haki zetu za msingi, maana tumevumilia mno hadi kilio cha kwi kwi. Ni mimi mwanaharakati,  Amoni, wa Kata Msangamkuu, Mtwara Vijijini. +255652221100.
Ninaomba uelewe lengo la wananchi wa Mtwara na Lindi sio kwamba hawataki gesi isitumiwe na wengine hapana, wao wanataka kiwanda kitengenezwe Mtwara. Kule itoke gesi safi, maana wanakataa mambo yasijekuwa kama ya madini ya Geita ambayo mwekezaji anachimba anaenda kuhakiki Mwanza na kulipa kodi ya uwongo na kuiibia nchi na kuwa masikini, huku wakifaidi watu kutoka nje.
Nimesoma makala yako, inayosema tatizo ni gesi, siasa, choyo au ubaguzi? Mimi nimeisoma na kwa utafiti wangu, nimegundua kwamba wewe ni CCM na ndio maana ukaona eti ni siasa. Hapana, ni kwasababu vyama vya upinzani vinapenda maendeleo ya Watanzania.
Mbona hawakuhamisha miwa kutoka Kagera na kuileta Dar es Salaam ili itengenezwe hapa? Pili, hebu fikiria gharama za kuweka bomba ni kiasi gani? Tatu, kumbuka msongamano mkubwa wa watu, ina maana wakiongeza viwanda wanazidisha msongamano. Nne, kwanini wasiwaachie watu wa Mtwara na Lindi na wao wapate ajira? Tano, kila kilichokuwapo Dar es Salaam, Mtwara kipo kama vile Bandari na mengineyo. +255713221244.
Ingawa hujaonyesha wazi ujumbe unaopeleka kwa wana Mtwara, lakini ninachofahamu, Taifa halina rasilimali. Mikoa, wilaya, vijiji, ndivyo vyenye rasilimali, kama vile mbuga za wanyama, madini, mazao na mengineyo ambayo mapato yake hukusanywa na kuwa pato la Taifa. Gesi ni kama rasilimali nyingine tu. Ikiwa Mtwara, Lindi, Kigoma, Mbeya au popote nchini, tueleze ni vipi italinyima Taifa letu pato? Au italigawa vipi Taifa? +255717757797.
Hongera bwana Kambi Mbwana kwa makala yako. Endelea kuwapa elimu Watanzania wenzetu wasioelewa. Naitwa Moi, +255757295249.
Unajua sisi tunaotoka Mtwara tunafananishwa na nyani katika Taifa hili. Hatuna thamani mbele ya makabila mengine toka Uhuru. Barabara haijaisha, mazao yetu hayana usimamizi na hatuna huduma za jamii zilizo bora. Tukipata wakarimu, sio bora pamoja na watumishi wote. Sisi ni jamii ya mwisho katika Taifa hili, hujiulizi gesi na mafuta aliyotupatia Mwenyezimungu ingekuwa sehemu nyingine ingehamishwa? Kwakuwa sisi nyani, hatuna thamani, gesi itaondoka na mafuta pia yataondoka, maana hawa hawatatuthamini milele. +255712848839.
Asante kwa makala yako, lakini usiwe mwandishi mwoga anayeogopa watawala walioshindwa kuwaondolea wananchi umasikini na kuligawa Taifa, kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. Jitahidi kuwa mkweli ili upate mafanikio maishani mwako. +255755045295. Kijana mbona unakuwa kama popo asiyejulikana kama ni mnyama au ndege. Ya Handeni Kwenu yamekushinda sasa umehamia kwenye gesi.
Nasikitika ujumbe huu uliotumwa kwa namba +255757602075. nimeufipisha kwa sababu za kimaadili, maana ulijaa matusi na kashfa kutoka kwa mtumaji, ambaye pia hakujitambulisha jina lake. Kaka nimesoma makala zako nyingi, nimegundua wewe ni kada wa CCM na usiyejua nini wanachokitaka Watanzania.  Hata hujui huko vijijini watu wanaishi vipi. Unaogopa ya Daudi Mwangosi na Amina Chifupa na huo sio uzalendo, hivyo hupaswi kuwa mwandishi.
Hivi unajua CCM wanaiendashaje nchi hii? Umeshahoji wananchi wangapi kuhusu maisha yao badala yake unamfuata Nape Nnauye, unataka CCM ndio waiongoze nchi milele na milele kwakuwa wewe si mzalendo. Ujumbe huu ulitoka kwa namba +255652273836. Nashukuru brother kwa kuweza kupata fursa ya kuweza kusoma makala yako.
Ni kweli hoja zako ulizozisema zinaweza kushabihiana na ukweli,  ila kutokana na vile hali ilivyo naweza (kudetermine ya words) nazo yanatokana na siasa pia. Hebu nambie kaka angu, umaskini uliopo katika mikoa ya kusini, moja kwa moja tumekuwa maskini na hii ilikua nafasi pekee ya kuweza kupata ahueni.
Hebu jamani isifike wakati tukawa tunaangalia swala hili kijuu juu, hali ni mbya kusini hatuna pa kushikia, serikali ilibidi iangalie gesi hii pia katika kutafuta namna ya kuikomboa miji hii ya kusini.
Ni wazi kuwa serikali imekua ikifurahia tu kupata neema hiyo kuendesha mambo yao na si kusaidia kuondosha umaskini.
Nyinyi waandishi tunawategemea kutoa hoja za kusaidia kuondokana na majanga ya kimaskini. Ujumbe huu ulitumwa kwa njia ya barua pepe kutoka kwa Raya Juma, Nashkuru Haya ni baadhi ya maoni yaliyoingia mara baada ya kuandika makala ile, huku watu wakiingia moia kwa moja katika hoja yangu ya siasa, ubaguzi na choyo nilizokemea. Kwanini nasema siasa? Ukiangalia hapo, wapo waliotuma ujumbe huo wakiwa na chukia serikali ya CCM. Hata hivyo, kuyaanika maoni yao si kuwaletea matatizo, bali kusoma mawazo ya watu wa Mtwara.
Wao ndio wahusika. Ndio wenye kupigania suala la gesi, hivyo inaweza kuwa njia muafaka ya kuepusha shari inayozidi kujengeka mioyoni mwa Watanzania, hususan wale wanaoishi mkoani Lindi na Mtwara. Watu wamekuwa na mawazo tofauti juu ya sakata hilo. Wapo wale wanaofikia kutamani Mtwara iwe na utawala wake, jambo ambalo hakika si la kuchekea.
Rasilimali za Tanzania zinaanza kutugawa kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, ndio maana nikaamua kuyaanika mawazo ya ndugu zetu hao. Kwa kumalizia tu, sakata la gesi linaweza kujadiliwa upya kwa kuwashirikisha wadau na wananchi wa Mtwara, hasa kwa kupewa mikakati ya namna ya serikali kuwapelekea maendeleo maana ni wajibu wao.
Masuala ya chokochoko ya gesi yasiachwe tu kwa wanasiasa ambao wamekuwa wabunifu kuingia kwenye hoja zinazoshirikisha watu kwa ajili ya kujijenga kisiasa, jambo ambalo si zuri.
Na sisi tunaofikia kujadili suala la gesi, wakiwamo wana harakati, wasitumie maneno makali, maana siku zote jazba inaondosha maana husika. Maoni mengi ya Watanzania nimeshindwa kuyaandika kwa kwasababu hayajatolewa kiungwana, huku niliyoaandika nikiyafanyia marekebisho mengi mno.
Katika hili, serikali kwa kupitia Waziri wake wa Nishati na Madini, Professa Sospeter Muhongo, anapaswa kukaa na kulijadili jambo hili kwa mapana yake.

kambimbwana@yahoo.com
www.handenikwetu.blogspot.com
+255712053949
+255753806087

No comments:

Post a Comment

Maoni yako