Na John Chitanya, Nyasa
Mei 4, 2012 yalifanyika maandamano
makubwa sana katika wilaya mpya ya Nyasa iliyogawanywa kutoka wilaya ya Mbinga.
Nyasa ni wilaya ni kiserikali, lakini katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi
inafahamika kama jimbo la Mbinga Magharibi. Maandamano yaliyofanyika yalilenga kuishinikiza
serikali kumruhusu Mganga wa Kienyeji apewe kibali cha kufanya kazi yake ya kuwaumbua wachawi wilayani
hapa.
Maandamano yale yalionyesha na
televisheni ya TBC1 wakazi wa mji
wa Kilosa nje kidogo ya mji mdogo wa Mbamba Bay, kwa hakika ilikuwa fedheha
kubwa kwa wananchi wa ukanda wa ziwa Nyasa na maeneo mengine yanayounda wilaya
hiyo kwa upande wa mashariki ambayo yanakaliwa na jamii ya Wamatengo.
Kwa mtazamo wangu kama kuumbuana na
kushika uchawi wameshikana sana, sasa tunataka maendeleo sio kuimba
nyimbo za wachawi kuwanyima maendeleo baadhi ya watu.
Watu wengi wanaamini kuwa kuna kasoro
pale inapotokea jambo fulani likawa baya, basi linazungumzwa kuwa linatokana na
kurogwa na wachawi.
Mganga wa kienyeji |
Niliwahi kushuhudia tukio moja kwa moja
ya familia iliyokuwa ikiendesha kikao cha kifamilia, kwamba binti mmoja wa
shule ya msingi alishindwa kusoma na kuandika hivyo walipanga kwenda kwa Mganga
wa Kienyeji ‘kumfungua” kwa madai alifungwa na watu wabaya(wachawi) asiweze
kujua kusoma na kuandika.
Hakika suala hilo lilileta mtafaruku kwa
wale waliofanikiwa kwenda shule, wakadai kuwa hilo ni suala la mwanafunzi
mwenyewe wala halina uhusiano na kufungwa kwa misingi ya uchawi. Lakini ilishikiliwa uchawi ndio umemfunga
binti yule. Hadi naandika makala hii juhudi za kumfikisha mwanafunzi yule kwa
Mganga wa kienyeji zilikuwa zimesimishwa ila sina shaka zitaendelea kwani nia
yao ipo na wanaonekana kuamiani sana uchawi umetumika kwa binti yule.
Matukio ya uchawi yamekuwa yakitangazwa
sana hata wakati uchaguzi unapofanyika, kwani wagombea mbalimbali wanadaiwa
kuwategemea waganga wa kienyeji, wapiga ramli na kuamua hatima ya harakati zao. Kwenye michezo ya mpira wa miguu na
mingine suala la uchawi limekuwa likichukua nafasi kubwa bila kutegemea sayansi
ya kuleta mafanikio.
Hatua za vigogo kuhangaika na kuwategemea
waganga wa kienyeji inaleta ujumbe kuwa jamii yetu inakabiliwa sana na janga la
uchawi na kutoamini nguvu zilizomo kwenye akili na miili yetu.
Leo hii ni vigumu kufanya jambo la
maajabu kwa kutohusisha uchawi. Hapa ndipo mimi siku zote huamini mapinduzi ya
maendeleo ya wilaya ya Nyasa na yale yenye kasumba za kutegemea wachawi
yanapaswa kuanzia katika fikra zetu. Tuna mambo mengi ya kuyafanyia maandamano
katika nchi hii, mfano umeme, bandari, barabara isiyoisha na mengine mengi,
lakini wananchi wameshikilia na kuamini kuwa uchawi umesababisha wawe na maisha
duni.
Hata hivyo tukio la mji wa Kilosa,
waliohamasishwa mapema mwezi Mei, ili Mganga wa kienyeji kutoka Tanga
walikamatwa na mamlaka zinazohusika. Mganga huyo alihamasisha vijana wa Mbamba
Bay wafanye fujo kushinikiza apewe kibali ili atoe uchawi kwenye nyumba za watu,
basi wale vijana wakavunja ofisi za serikali na kuchoma moto, huku wakalazimisha kila familia kuchangia shilingi
5000.
Mamlaka zinazohusika zilifanikiwa kuzima
jaribio hilo, na kuwakamata baadhi ya vijana waliohusika. Baadhi ya vijana yao
ni mabinti watatu waliokamatwa kwa kosa la kuandamana bila kibali na kufanya
vurugu, walishikiliwa mjini Kilosa, Mbamba Bay. Tukio hilo linaturejesha kwenye mjadala
hivi masuala ya uchawi yanachukuliwaje kama turufu ya kufanya uhalifu au
uvunjifu wa amani? Uchawi umekuwa ukizungumziwa sana katika jamii zetu.
Wafanyabiashara wanategemea uchawi, watu
wa kawaida wanategemea uchawi, ina maana hata masuala yenye kuhitaji utaalamu
yamepewa dhana ya uchawi. Jamii yetu imeshikilia dhana ya uchawi kama nyenzo ya
kupata mafanikio. Wengi hushikilia sana kupiga ramli,
wamekuwa wakishindwa kujielemisha na kupata ufumbuzi wa matatizo ya familia na
jamii huku wakiamini matukio hayo yanatokana na uchawi.
Idadi ya wapiga ramli nayo inaongezeka
kila kukicha. Ulimwengu unatuacha nyuma, na kila mwenye mafanikio maishani
anaweza kutazamwa kwa namna mbili; mosi aliiba mahli na pili amefanya uchawi. Hakuna watu wanaoamini kuwa juhudi hizo
zimefanywa na mhusika. Kuna masimulizi mengi sana kwa wana jamii ya wilaya ya
Nyasa kuhusiana na uchawi. Magari yakipinduka husemwa uchawi, hakuna anayesema
kuwa barabara ni mbovu, wote husikilia uchawi.
Kuna mambo mengi yanatisha na bila juhudi
za serikali kusambaza elimu kila jambo lingeonekana kwua uchawi. Na serikali
yetu haiamini uchawi hivyo ni kosa la mtu kufanya fujo kama vijana wale kwa
kisingizio cha uchawi. Sio hapa tu, hata Afrika Kusini,
aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Pits Mosimame aliwahi kukaririwa
na vyombo vya habari akijibu swali kwanini Bafana Bafana haijashinda mechi
nyingi tangu achukue madaraka.
Naye alijibu kwa urahisi kuwa shirikisho la soka la Afrika Kusini
halijamlipa Sangoma (mganga wa kienyeji) tangu michuano ya kombe la dunia. Hali
hiyo inaonyesha namna gani jamii imetawaliwa na uchawi. Kila kitu tunachofanya kinaonekana
kimetokana na uchawi. Wachawi wamekuwa vikwazo kwenye mafanikio ya jamii yetu.
Dhana hii ya uchawi itaendelea
kutuangamiza ikiwa juhudi za makusudi hazitachukuliwa. Kwa mtazamo wangu, naona
uchawi ni sumu kali sana, lakini kama uchawi wa kisayansi basi nitasema kila
nchi inao uchawi.
Nasema kila nchi inao uchawi kwa maana ya
kisayansi kutokana na mila na desturi za nchi hiyo. Ujerumani walileta utabiri
wa Pweza Paul, akatabiri ushindi kwa wahispania. Nao ni uchawi kama wapiga ramli za kisayansi sio
mazingaombwe. Zipo nchi zinatumia uchawi wa kisayansi kwa njia ya maneno
hususani katika dini, “kuapishwa”
au “kusimikwa”, kinachotendeka ni uchawi, ni mila na desturi za nchi husika na
tamaduni zao. Mikoa ya kanda ya ziwa inakabiliwa na dhana hii ya uchawi
imesababisha hofu kwa ndugu zetu albino, na wazee wenye macho mekundu. Wazee
hao huuawa kwa kisingizio eti wachawi. Nionavyo uchawi uliosababisha watu wa mji
wa Kilosa waandamane mapema mwezi Mei mwaka huu ni sumu kali sana, na kawaida
sumu haiwezi kutibu ugonjwa mwingine, kwani huua.
John Chitanya ni mwandishi na mwalimu wa Miracle Center, mjini Songea. Niandikie: 0718 005557
No comments:
Post a Comment
Maoni yako