May 12, 2013

KAMARA KUSUPA: MWAFRIKA ALIKUWA WA KWANZA KUWASILI MAREKANI KABLA YA CHRISTOPHER COLUMBUS

Na Markus Mpangala, Dar es Salaam
HIVI karibuni nilipata fursa ya kumhoji mwandishi wa kitabu cha ‘Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake: Mradi mgumu kuliko yote,’ Mwinjilisti Kamara Kusupa.
Haya ndiyo mazungumzo yetu ambayo bila shaka yatawanufaisha Watanzania kufahamu nini maana na asili ya Afrika kwa ujumla wake na maisha halisi ya bara letu.
SWALI: Niliwahi kusoma vitabu vyako viwili, “Maisha yangu Gerezani”, baadaye kile cha “Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka”. Kuna tofauti gani kati ya vitabu hivyo na hiki cha sasa?
KUSUPA: Tofauti ipo, sababu kile cha kwanza niliongelea maisha ya gerezani na namna vijana wanyonge wanavyoteseka. Wengine wanakosa utetezi na wengine hawana msaada wa kisheria na wapo wanaogandamizwa.
Nikiwa na Mzee Kusupa
Halafu kuna wale wanaosota miaka mingi bila kesi zao kutatuliwa. Kitabu changu cha pili kimeongelea suala la nchi yetu ya Tanzania, kwamba tunataka iweje na iongozwe vipi katika kutafuta katiba mpya. Naizungumzia Tanzania ya wakoloni, baada ya ukoloni, kipindi cha Nyerere na baada ya Nyerere. Halafu nimeongelea hili suala la vyama vingi vya siasa. Lakini kitabu hiki kipya namtazama Mwafrika na matatizo yake yanayomsonga kila kukicha bila ufumbuzi huku akiwa tegemezi. Mwafrika ambaye hajachukua nafasi kuyachukua mazuri ya mababu wa asili yake.
SWALI: Lakini maandiko ya namna hii yako mengi hapa nchini na kote Afrika kwa ujumla kuhusiana na Mwafrika. Wapo Watanzania ambao wameandika vitabu kuelezea matatizo ya Afrika, mfano Dk. Malima Bundara aliandika, “Waafrika ndivyo Tulivyo”. Je, wewe unazungumzia nini kwenye hiki kitabu kipya?
KUSUPA: Nakiri yapo maandiko mengi kuhusiana na Waafrika. Yapo maandishi kama ya akina Cheikh Anta Diop (Senegal), Dk. Elly Kamugisha (Tanzania), Franz Fanon (Algeria), Julius Nyerere, Leopold Senghor (Senegal), Ali Mazrui, Marcus Garvey, Nelson Mandela na wengineo.
Lakini jambo kubwa lililokuwa likijadiliwa ni nani hasa huyu Mwafrika. Lakini wakasahau kuwa Mwafrika huyu ana asili zake, hizo ndizo ninazoongelea kwenye kitabu hicho kipya.
SWALI: Unakubaliana na mahitimisho mengi ya wasomi wa Afrika kuhusu Mwafrika ni nani na anaweza kurudi kwenye asili yake kwa njia gani?
KUSUPA: Wengi wanakubaliana kwamba Mwafrika ni mtu mweusi, hivyo kuwatenga Waarabu, Wahindi, Wazungu na Waberiberi ambao kimsingi nao wamejikuta wakiwa wamezaliwa katika bara ya Afrika hivyo hawawezi kutengwa.
Kwa mfano; msomi Dk. Harrith Ghassany alipata kuandika nini asili ya Afrika. Kwa utafiti wake akaelezea kuwa asili ya Afrika ni kutoka kule Tunisia.
Dk. Harrith alisema hayo kwenye kitabu chake cha “Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni: Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia.” Yote haya yanatuletea swali la msingi Mwafrika huyu ni nani?
Hata hivyo dunia imebadilika na kila kona inatusaidia kujua nini hasa kinachopaswa kusemwa kwa dhati na moyo safi kwa nyakati za sasa na baadaye. Kuna Wazungu wamezaliwa Afrika Kusini, Tanzania na wengine nchi nyingine za Afrika.
Je, hawa watakwenda wapi ikiwa hawajui asili zao au mahali walikoanzia zaidi ya kujikuta wakiwa katika nchi wanazoishi. Ni kama ambavyo Waafrika walioko Ulaya, Amerika na Asia wanavyojiuliza ni namna gani wataweza kurudi Afrika ambako hawajui waanzie wapi.
Ni vigumu leo kumwelezea Jesse Jackson, Mohamed Ali warudi Afrika kutoka Marekani. Ni vigumu vile vile kumweleza Lennox Lewis wa Uingereza arudi barani Afrika.
Ni vigumu kumwambia Danny Jordan wa Afrika Kusini kwamba uchotara wake sio kitu arudi kwenye asili ya makaburu Uholanzi na kwingineko. Au ni vigumu kumwambia Hellen Zille, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance (D.A) pale Afrika Kusini na gavana wa jimbo la Cape Town, kwamba arudi kwa wazungu wenzake.
SWALI: Unadhani hilo linatokana na uhusiano wa Waafrika na wageni, ndio kiini cha Mwafrika kurudi kwenye asili yake?
KUSUPA: Kwanza niseme hii ni moja ya mabadiliko makubwa ya mipaka ya nchi ambayo imeshindwa kuzuia uhusiano wa wanadamu kutoka nchi moja hadi nyingine au kutoka jamii ya nchi moja kwenda jamii ya nchi nyingine.
Leo Mwafrika anaweza kuzaa na Mchina au Mkorea hivyo ni vigumu mtoto atakayezaliwa kutotambuliwa kuwa Mwafrika, na kuangalia asili. Lakini wapo watu wanaojaribu kujiuliza ni namna gani wanaweza kuwakumbusha Waafrika wenzeo kuwa Mwafrika alikuwa na asili yake.
Hata kwenye dini, Waafrika wanazo. Ukisema Waafrika hawana dini nitakuambia soma maandiko ya Mchungaji Blacid Temple kwenye kitabu chake cha “Bantu Philosophy”, kwa hiyo ushahidi wa asili zetu upo kidini, kisiasa na kiuchumi.
Propaganda iliyohubiriwa kwa nguvu na pia kufundishwa na elimu ya kikoloni ni kwamba Mwafrika ameanza kuwa na dini baada ya ujio wa Waarabu na Wazungu barani Afrika.
Baada ya kazi ni gumzo
Kwa mfano; katika Afrika ya Mashariki, Uislamu uliingizwa katika karne ya nane na wafanyabiashara kutoka Ghuba ya Uajemi (leo tunaita Iran), hao wafanyabiashara wa kiajemi ndio walioitia jina la Dar es Salaam mji maarufu wa Tanzania lenye maana ya mbingu ya amani.
SWALI: Je, ni kweli kwamba kabla ya ujio wa wafanyabiashara wa kiajemi, Waafrika wa eneo hili hawakuwa wakimwabudu Mungu?
JIBU: Narudi kama nilivyoeleza mwanzoni, Waafrika walimjua Mungu wa kweli, walimwabudu na kuishi kulingana na miongozo yake. Ushahidi wa kuonyesha Mwafrika aliabudu Mungu kabla ya ujio wa Uislamu na Ukristo ni uwepo wa majina yanayoendana na masuala ya kiroho na ibada.
Lakini tunapokuja kwenye eneo linalohusu mambo ya kiroho, maneno kama ibada, Nnungu, Mungu, Mulungu, Ngai, Nkoyi, Kyala, Malaika na Banzelu neno kutoka lugha ya Kilingala lenye maana ya viumbe weupe wanaong’ara  ni udhihirisho wa kwamba Mwafrika  alimjua Mungu na alikuwa na mawasiliano naye.
Katika somo hili tunajadili kwa ufupi juu ya Uislamu, Ukristo, Ubuntu na dini ya asili iitwayo Alabba ndani ya kitabu nimeeleza sana hili.
SWALI: Mwafrika haonekani kutajwa kwamba mmoja wa watu waliowahi kuishi au kufika Marekani kabla ya ukoloni. Labda tuseme Latini Amerika yote kusini na kaskazini. Lakini tunashuhudia Waafrika wengi wakiwa huko na baadhi ya mila na desturi zao zinalingana na Waafrika wa bara la Afrika. Kwa nini?
KUSUPA: Kwanza niseme wanaoeneza kuwa Mwafrika hakuishi Marekani kabla ya biashara ya utumwa hawako sahihi, au kule Latini Amerika. Kuna sababu nyingi, lakini kubwa ilianzia kwa Columbus.
Mwafrika alikuwa wa kwanza kuwasili Marekani kabla ya Christopher Columbus, hata ukisoma maandiko yenye ushahidi yaliandikwa na Profesa Ivan Sertima kwenye kitabu chake "THEY CAME BEFORE COLUMBUS". Hizo  'voyage' mbalimbali za Christopher Columbus zimejaa mengi ya kushangaza na kwa nini yanachukuliwa kuwa kama yalivyo au ukweli wenyewe? Waafrika wanayo mengi hayakuandikwa vizuri.
SWALI: Kwa hiyo una maana kwamba ndani ya Kumrudisha Mwafrika kwenye Asili yake: Mradi mgumu kuliko yote umeelezea nyongeza yake na hali halisi ya Mwafrika na asili zake, ukizingatia dhana ya uhai pia?
KUSUPA: Kwanza tunaangalia sisi Waafrika ni nani na asili yetu ikoje, hicho ndio kiini. Dhana ya uhai inakuwa kubwa na inachukua mkondo mkubwa pia, hivyo basi kitabu cha KUMRUDISHA MWAFRIKA KWENYE ASILI YAKE; MRADI MGUMU KULIKO YOTE nimeleta baadhi ya majibu ya maswali ambayo kila mara watu wanajiuliza.
Nimeelezea kuanzia kwenye dini, siasa, utamaduni, na mengine mengi kuhusu Afrika, nimeelezea mengi kwamba kuna makosa kadhaa yanafanyika ni vigumu kuizungumzia Afrika kama wanazuoni Ali Mazrui wanaoitazama Afrika kichotara.
SWALI: Unazungumzia Afrika ya kichotara, una maana gani hasa?
KUSUPA: Hakuna wakati wowote katika historia ya dunia na maisha ya mwanadamu kiujumla, ambapo Afrika imeacha kuhusiana na watu kutoka nje ya bara hili, hivyo nazungumzia Afrika na Wageni kutoka Ulaya, Amerika na Asia. Tangu awali na baada ya Kristo watu kutoka nje wamekuwa wakiingia Afrika kwa sababu moja au nyingine.
Katika mada hii ya Afrika na wageni, tunazungumzia wageni wa aina tatu kutoka nje ya bara la Afrika. Tunajadili juu ya Afrika na wafanyabiashara kutoka mabara mengine ya Asia, Ulaya na Arabuni, Afrika na waeneza dini kutoka nchi za ulaya magharibi na Afrika na Wazungu wa  magharibi waliojifanya wavumbuzi yaani wale wachoraji wa  ramani za kuonyesha mito mikubwa, milima mirefu na maziwa.
Tunajadili juu ya Afrika na tamaduni za kigeni, Afrika na dini za kigeni na mwisho tunajadili juu ya Afrika na tawala za kigeni ikiwa ni pamoja na mifumo inayoendelea kutumika hadi sasa kuongoza maisha ya Waafrika.
Kila jamii imekuwa kwenye asili yake na inakuwa vigumu kurudi kwenye asili yake. Tujiulize je, dini za Waafrika ni zipi? Mfumo wa utawala wa Waafrika ni upi?
Msingi wao na dhana ya uhai vikoje? Uhusiano wao na jamii za nje ukoje? Je, Mwafrika ataepuka dhahama ya mabadiliko ya kijamii duniani? Je, Mwafrika ataweza kurudi katika asili yake?
Nadhani ni moja ya mambo ya kusisimua na hakika yatakuwa na hamasa kwa wasomi mbalimbali na wananchi wengine. Kikubwa tuseme kama kweli tutaweza kurudi kwenye asili yetu au ni mradi mgumu?
SWALI: Katika kitabu chako umegusia suala la muungano wa bara Afrika?
KUSUPA: Hilo nimezungumzia kwa kina. Nimeanza toka kwenye utumwa, ukafuatia ukoloni na baadaye utawala wa chama kimoja au udikteta wa chama kimoja.
Hatimaye Afrika imeletewa utandawazi unaoyafanya mataifa yenye nguvu yawe dikteta wa kudumu wa kuzilazimisha nchi za Afrika kujiendesha sawa na watakavyo wao.
Afrika iligawanywa vipande vipande na kuitwa majina mapya na wakoloni, lakini pia wakoloni hao wakati wanachora na kuweka mipaka yao ya kufikirika, ndipo waafrika tulipogawanywa na kutenganishwa na kupewa utambulisho mpya wa kuitwa Watanganyika, Wakenya, Waganda, Wakongo, Wanyarwanda, Warundi, Warhodesia, Wamozambiki, Wanigeria, Wakameruni, Waghana, Wasenegali, Wamali, Waliberia, Wasealeoni, Wanamibia, Waangola, Wasudan, Wasomalia, Waethiopia n.k.
Wakati wakoloni wanaigawa Afrika na kuweka mipaka yao mipya tofauti na ile mipaka ya asili iliyokuwa inatambuliwa na wenyeji, pia waafrika walitenganishwa na kuumbiwa hisia mpya. Mpaka wa kutenganisha nchi na nchi nyingine uliweza kupita katikati ya eneo moja na kuwafanya watu wa kabila moja au ukoo mmoja kuwa na uraia wa nchi mbili tofauti. Hivyo Afrika lazima iungane.
SWALI: Nashukuru kwa kushirikiana katika fursa hii. Naamini Watanzania watanufaika kutoka katika maandiko yako mazuri ya kitabu chako.
KUSUPA: Karibu wakati mwingine, ninyi vijana mnatakiwa kujua zoezi jipya la Afrika kuwa na mipaka mipya lilimpa Mwafrika hisia mpya na utambulisho mpya. Nitafanya mhadhara UDOM kuelezea hilo Mungu atujalie. Kwa hiyo lazima tujirudishe kwenye asili zetu.
Baruapepe; mwanazuoni27@gmail.com

1 comment:

  1. Anonymous24 May, 2013

    I drop a leave a response when I especially enjoy a post on a website or if I have something to add
    to the conversation. It's triggered by the passion displayed in the article I read. And after this article "KAMARA KUSUPA: MWAFRIKA ALIKUWA WA KWANZA KUWASILI MAREKANI KABLA YA CHRISTOPHER COLUMBUS". I was excited enough to write a thought ;) I do have some questions for you if you do not mind. Could it be just me or does it look as if like a few of the responses look as if they are coming from brain dead people? :-P And, if you are posting on additional places, I would like to keep up with anything new you have to post. Would you make a list all of your social sites like your twitter feed, Facebook page or linkedin profile?

    Here is my blog :: magazine blackjack trade stimulator

    ReplyDelete

Maoni yako