May 31, 2013

WABUNGE WETU HAWAFAHAMU MASLAHI YA TAIFA?


NA MARKUS MPANGALA
TUMESHUHUDIA bunge letu likigeuzwa sehemu ya kufanya mizaha isiyokwisha, kana kwamba wanehshimiwa wamekwenda pale kupiga ulabu na kadhalika. Staha ya kibunge inaelekea kutokeweka sababu hata kauli ya Mheshimiwa Ezekiel Wenje dhidi ya chama chenye mifumo na kuunga mkono Uliberali, ikidhaniwa alikilenga chama cha CUF haikuwa na staha.
Tunapojadili masuala ya taifa tunalazimika kuweka kando mzaha wowote ambao unasababisha tuonekana tuna wazimu fulani. Sote tunaunga mkono mabadiliko katika nchi yetu. 
Ukumbi wa Bunge letu

 Sote tunamhimiza Rais Kikwete afanye juhudi kutekeleza ahadi zake ikiwemo kununua Meli katika Ziwa Nyasa ambayo ni muhimu kumkumbusha. Sote tunafahamu kuwa ili tuweze kuyafikia maendeleo lazima tuchukue hatua za msingi. 

Kama Mbunge anayo hoja ya msingi kuhusiana na chama fulani na inalenga kuwakumbusha wabunge na viongozi wa chama husika kwamba mwenendo wao haupaswi kuigwa sababu unahatarisha ama unasababisha hatari katika taifa. 

Lakini kama Mbunge anakuja na maelezo kuwa chama fulani kinafadhiliwa na chama fulani cha nje na ambacho kinaunga mkono ushoga au usagaji, sidhani kama linaleta mantiki kwa wananchi. 

Mbunge anapotamka maneno kama hayo kisha Bunge zima linaahirishwa hakika huku ni kuchezea akili za watanzania. Bunge linatumia gharama kubwa. 

Tanesco inamwaga umeme bungeni. Kuna wataalamu wanalipwa posho. Wabunge wanalipwa posho. Mafundi mitambo wnaalipwa posho. Watumishi na wasaidizi mbalimbali wamepiga kambi yao Bungeni katika kuhakikisha gurudumu la maendeleo ya taifa hili yanakwenda sawa. 

Lakini hakuna kinachotia kinyaa kama ile Bunge linaahirishwa kwa sababu za kitoto kabisa mbunge kuleta utoto. Hatukati kwuapa changamoto washindani wako lakini jambo kubwa zaidi katika Bunge ni majadiliano yenye kufuata taratibu husika. 

Kama mbunge anaona hatendewi haki taratibu zipo na tunazieleza hizo kwa wananchi ili wajue kinachoendelea katika bunge letu sio vinginevyo. 

Haiwezekani pesa za watanzania zikatumia kuwafanya wabunge waketi na kuzungumzia mizaha kwamba mfadhili wa chama fulani anahusudu mashoga ama la. 

Jambo hili linaleta fadhaa kubwa miongoni mwetu kwani halina maslahi yoyote kwa wananchi. Tatizo kubwa la wanasiasa wanatuchukulia sisi wananchi kama watoto tusiweza kufanya tafakuri jadidi. 

Kila siku bunge letu linakuja na taswira kanganyishi. Tunakubaliana kwamba yapo malumbano ya hoja na yenye kulinda maslahi ya nchi.
Lakini kama lililotokea siku chache zilizopita hadi Bunge kuahirishwa na mheshimiwa Naibu Spika, Job Ndugai, hakika linakasirisha. 

Inaelekea siku hizi ili uwe mwanasiasa makini na hodari lazima uwe na hasira, kejeli, na ubabe fulani kama akina Mohamed Ali ulingoni.
Bahati mbaya, badala ha kujijengea ubabe wa kifikra na hoja tumejigeuza kuwa wababe wa maneno ambayo yanalipiwa posho na hayana msaada wowote kwa taifa hili. 

Tumeruhusu bunge letu liwe na maneno yanayolipiwa posho wakati hayana msaada wowote kwa wananchi wanaopata shida huko mitaani.
Tumeruhusu kukanganyana ndani ya Bunge kwa sababu ya kulinda na kujigamba wka vyama vyetu kisha tunasahau hivyo vyama pasipo kura za wananchi tusingelifika hapo.
Wananchi wanakaa na kuangalia Bunge kwa kiwango cha juu sana. Wanasikia maneno yanayotolewa na waheshimiwa Wabunge.Mjadala unapokuwa na mantiki huku wabunge wakijadili masuala nyeti ya taifa bila shaka wananchi watawaunga mkono zaidi na kuonyesha mapenzi yao kwa wawakilishi. 

Wananchi watafurahia na kuamini kuwa posho wanazolipwa wbaunge na watendaji mbalimbali walioko bunge zinafanya kazi ipasavyo.Lakini tukiendelea kuruhusu uchafuzi huu ufanyike ndani ya bunge huku kura zetu ndio zimewapa mamlaka ya kutoa maneno yasiyo na staha mbele ya wageni pamwe na weenyeji hakuna shaka ni aina fulani ya ukosefu wa heshima kwa wananchi. 

Bunge ni sehemu ya kuisaidia serikali na kuikumbusha namna ya kuendenda mambo ya msingi. Tumekuwa tukilalamika wkamba serikali inafanya uzembe kwenye suala la sheria za gesi na mafuta, lakini badala ya kuikumbusha na kuchambua mambo nyeti tumebaki kuelezeana habari za mashoga na wasagaji ama vyama vya kiliberali vinavyosaidiwa na waungaji ama wanaohimiza ndoa za jinsi moja. 

Fedha za taifa zinateketezwa na bunge linaahirishwa. Posho inaingia mfukoni mwa mbunge wakati hana lolote la maana alilosema. Ni uchovu wa kufikiri kudhani kukishambulia chama fulani na kuchungulia udhaifu wao ni moja ya demokrasia nzuri kuliko, lakini ikigeuzwa kwako inakuwa nongwa. 

Lazima tukatae siasa za namna hii. Lazima tukemee matumizi mabovu ya fedha zetu kwenye Bunge ambapo mbunge analipwa posho lakini anazungumza mambo yasiyoleta changamoto. Bunge sio kijiwe cha kahawa ama kaya moja inayopiga soga baada ya kushiba. Ni uzandiki kuvumilia shughuli za Bunge zinaahirishwa kwa sababu za kipuuzi. Ni ukosefu wa adabu kwa Wabunge kudhani wnaanchi tumekuwa watu tusielewa kinachoendelea.  

No comments:

Post a Comment

Maoni yako