May 14, 2013

TUMEAMUA KUJIRIDHISHA NA FEDHA ZA “UWONGO”!


 Na: Albert Sanga, Iringa.

Nianze kwa kuwasalimu wasomaji wa safu hii ya Anga za Uchumi na Biashara, ambayo haikuwa hewani kwa takribani wiki saba. Sababu kubwa iliyonifanya nikatoweka safuni ni msiba niliokuwa nao baada ya kufiwa na binti yangu wa kwanza na wa pekee, Faith, aliyekuwa na umri wa takribani mwaka mmoja.
Katika juhudi na mahangaiko ya kuokoa uhai wake, binti yetu alifariki katika hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi wilayani Kilosa. Msiba huu uliniachia uchungu na majonzi makubwa mno kiasi ambacho akili, moyo na morali vilitoweka kabisa na isingekuwa rahisi kumudu tafakari pana zinazoijaza safu hii.
Nimekuwa na uzoefu (kiasi Fulani) wa kumudu majanga, mitikisiko na mikasa ya kibiashara; lakini lilipokuja suala la kupoteza mtu muhimu kama mwanangu, hakika nilijikuta ni mgeni kabisa wa kuhimili mtikisiko wa msiba huu.
Matakwa yetu na maombi yetu yalikuwa ni kupona kwa binti yetu, lakini Mungu aliamua kuutwaa uhai wake. Tunamshukuru na kumtukuza Mungu kwa yote tuliyopitia nasi tunajua Mungu anabaki kuwa Mungu hata kama hakujibu tulivyotaka.
Kipekee kabisa ninatumia fursa hii kuwashukuru makumi ya wasomaji wa safu hii kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao, baada ya kuona sionekani walinitafuta na kutaka kujua kulikoni? Mbarikiwe sana mliotutumia rambi rambi za fedha na salamu za faraja.
Ijapokuwa sikuaga wakati napotea safauni lakini sisiti kupiga mbiu inayoashiria kuwa nimerejea. Yapo mambo mengi ambayo tutaendelea kushirikishana yahusianayo na ustawi wetu kiuchumi, kiujasiriamali na kibiashara. Kwa kuwa leo ndio kwanza ninarejea, nitachambua kiunaga ubaga namna utamaduni wa watu kupenda fedha kuliko thamani ya walivyonavyo; jinsi unavyourubuni uchumi wetu.
Ni vema tukajikumbusha historia ya namna fedha zilivyoanza kutumika katika maisha ya wanadamu. Hapo zamani kulikuwa kukifanyika biashara ya ubadilishanaji wa vitu kwa vitu (barter trade). Ilikuwa kwamba mtu awapo na ng’ombe basi atabadilishana na mwenye chumvi, vivyo hivyo kwa mwenye mahindi anaweza kubadilishana na mwenye nguo.
Kadiri mfumo huu ulivyoendelea ikaonekana suala la kubeba vitu na kuzunguka navyo ili kutafuta wa kubadilishana nae ni usumbufu na lina ugumu mkubwa wa kuoanisha hayo mahitaji. Wakati mwingine mwenye ng’ombe anapohitaji chumvi halafu mwenye chumvi akawa hayupo tayari kupokea ng’ombe; basi hakuna biashara itakayofanyika na hivyo mwenye ng’ombe anakwama kupata chumvi.
Katikati ya mfumo huu kukaja kuibuka matumizi ya vito vya thamani (mfano dhahabu, pembe za thamani, chuma na madini mengine); kama viambata vya kubadilishia bidhaa (media for exchange). Hapa ilikuwa kwamba, mkulima anapovuna mahindi yake, pengine gunia kumi,  anayachukua mahindi hayo  na kuyapeleka kwa hao wanaotengeneza vito vya thamani, kasha anapewa idadi ya vito vya thamani vinavyolingana na thamani ya mahindi yake. Huu ndio ulikuwa mwanzo wa hiki tunachokiita fedha.
Hata hivyo baada ya muda kupita ikaonekana kuna upungufu katika uthamanishaji wa vito vya thamani na bidhaa wanazozalisha watu. Ndipo kukatokea watu ambao walikuwa kama wahakiki wa thamani ya vitu, mali ama bidhaa alizonazo mtu.
Hapa ilikuwa hivi; mkulima anapolima na kupata mahindi yake, pengine tuseme gunia kumi, alikuwa anayapeleka mahindi hayo eneo maalumu ambapo wanamtunzia. Wale wenye ile stoo (eneo alipotunzia), walikuwa wanaandika karatasi (kibali) linaloonesha kuwa mkulima A anamiliki magunia kumi ya mahindi yaliyopo stoo B.
Kwa hiyo mkulima alikuwa hana tena sababu ya kutembea na magunia ya mahindi kumtafuta mwenye chumvi; badala yake alitembea na lile karatasi kiasi kwamba anapofika kwa mwenye chumvi anampa lile karatasi na kupewa chumvi.
Yule aliyempa mkulima chumvi ataenda kule kwenye stoo (iliyotunza mahindi) na kuchukua mahindi yanayolingana na thamani ya chumvi aliyompa mkulima; kasha lile karatasi analiacha pale stoo. Hizi stoo zilikuwa ndio chimbuko la benki tunazoziona hadi sasa nay ale makaratasi yaliyokuwa yanaandikwa na wenye stoo ndio chimbuko la hizi noti tulizonazo hadi leo.
Hii ina maana mfumo wa mabenki na fedha ulitokea ili kuwe na haki, usawa na ukweli. Mkulima mwenye magunia kumi ya mahindi ni lazima apewe karatasi (fedha) inayoonesha kweli anamiliki hayo magunia kumi na si vinginevyo. Kama huyu mkulima akipewa karatasi inayoonesha anamiliki magunia kumi ya mahindi wakati hajapeleka chochote kule stoo ingekuwa ni kumrubuni, kumdhulumu na kumlaghai Yule mwenye chumvi.
Hii ni kwa sababu mwenye chumvi atakapoletewa lile karatasi na mkulima (aliyedanganya) ataitoa chumvi yake; lakini atakapoenda kule stoo ataambiwa hapa hakuna magunia ya hayo mahindi yanayoonekana kwenye karatasi uliyotuletea!
Baadae sana jukumu hili la kuandika (kuchapisha) haya makaratasi (fedha) yanayoonesha fulani kazalisha nini kilichopo wapi, likachukuliwa na mamlaka za kiserikali zilizokuwa zinasimamia jamii mbalimbali. Hivyo ikawa mkulima akizalisha mahindi yake anapewa karatasi lake (fedha), vivyo hivyo kwa mfugaji anapofuga na kuongeza mifugo na mjenzi anapojenga jengo. Kila mtu katika jamii alikuwa anashika fedha inayoonesha thamani halisi ya kile alichozalisha katika uchumi.
Kwa jinsi hii, tunaona kuwa, fedha katika uhalisia wake ni matokeo ya uzalishaji anaoufanya mtu katika uchumi.  Fedha sio mafanikio, isipokuwa ni utambulisho wa mafanikio. Utajiri wa mkulima hauwi katika yale makaratasi aliyoyashika (fedha) isipokuwa utajiri wake unakuwa kwenye yale magunia aliyoyazalisha. Thamani ya mwalimu haitakiwi kupimwa kwa kiwango anacholipwa isipokuwa kwa maarifa aliyoyazalisha kwa wale anaowafundisha.
Lakini katika jamii na nchi yetu sasa, watu wamekuwa wanathamini fedha kuliko uzalishaji. Watu wanapenda kupata fedha hewa! Ndio maana wanataka kuonekana ni matajiri wakati hakuna lolote walilozalisha katika mfumo wetu wa uchumi. Tunapokuwa na jamii inayothamini fedha kuliko uzalishaji; maana yake ni kuwa tuna jamii inayopenda kurubuni, inayopenda mikato-mikato, uwongo-uwongo na unyonyaji kwa wengine.
Kwa mizania ya uchumi ni kuwa moja ya sababu za mfumuko wa bei ni uwepo wa ujazo mkubwa wa fedha katika uchumi usiolingana na uzalishaji (uzalishaji mdogo). Kinachotokea ni kuwa fedha zinakuwa nyingi na bidhaa ni chache.
Wale walioshika fedha wanaanza kugombania zile bidhaa chache zilizopo; kinachotokea? Watu wanapandishiana “dau”, mwenye nguvu ananunua na mnyonge anabaki kulalamika. Matokeo? Ndio tunasikia vitu vinapanda bei kwa kasi kubwa.
Unapoona madalalai wamejaa mtaani, ambapo kila unachotaka kununua wapo katikati, ujue kuna ulaghai unafanyika kiuchumi. Ikiwa ninataka kununua nyumba na mwenye nyumba anaeuza namfahamu, dalali wa nini hapo katikati? Kwa kuwa tumeshauzoea mfumo wa udalali, ninaenunua nyumba ya milioni 25 ninalazimika kulipa milioni 30 ili dalali apewe milioni 5 yake.
Kiuchumi ni kwamba tunakuwa tumempa dalali milioni 5 za uwongo kwa sababu hakuna uzalishaji wowote alioufanya; ingawa “kijamii” tutamuona anamiliki utajiri wa milioni tano! Dalali anapoichukua ile milioni 5 na kwenda kwa mkulima kununua mahindi, unakuwa ni ulaghai kiuchumi.
Ni ulaghai kwa sababu hela ile (milioni 5) imechapishwa wakati hakuna uzalishaji katika uchumi. Kesho na keshokutwa mkulima anapotaka kuitumia ile milioni 5 kununua pembejeo anajikuta haitoshi tena (imeshuka ama kupoteza thamani) kwa sababu ni ya uwongo!
Sina ugomvi na madalali na wala siwachukii; isipokuwa tunatakiwa tuwatumie madalali pale tu panapokuwa na ulazima na ikiwa kweli uwepo wao unazalisha thamani “halisi” ya gharama wanazotaka. Madalali ni mfano mmoja tu lakini ulaghai wa kupata fedha pasipo uzalishaji upo katika mazoea mengi mno.
Kahaba anapodai malipo ya elfu 50, ni nani anaekuwa amethibitisha kiuchumi ya kuwa huduma yake ina thamani hiyo? Mfanyakazi wa serikali anapotaka asilimia kumi (10%) ili kutoa tenda kwa upendeleo, ni uzalishaji gani ameufanya kiuchumi? Mfanyakazi anapolilia mshahara mkubwa pasipo kuongeza tija kiuzalishaji, anatutakia nini kiuchumi kama sio balaa?
Uchumi wetu hauwezi kusonga mbele kwa kiwango kizuri ikiwa tunaendekeza kupata fedha na utajiri usiolingana na uzalishaji tunaoufanya katika uchumi. Hakuna fahari ya mtu kujiridhisha na utajiri ama mafanikio ya fedha yaliyopatikana kiujanja-ujanja, kimteremko-teremko na kiusanii-sanii.
 stepwiseexpert@gmail.com

1 comment:

Maoni yako