July 16, 2013

MAREKANI INAVYOINUFAISHA TANZANIA KUPITIA AGOA


Na, Albert Sanga, Iringa.
Rais wa Marekani Barack Obama alipofanya ziara ya kiserikali nchini kuna mengi tumesikia. Ujio wa Obama umekuwa na shamrashamra nyingi sit u Dar es Salaam bali macho na masikio ya watanzania wote yameelekezwa katika safari hii. Ni ziara ambayo pamoja na mambo mengine mengi pia imekusudia kuimarisha uhusiano mwema baina ya Tanzania na Maekani.

Kwa miongo mingi huko nyuma, Marekani imekuwa na historia ya kuzisaidia na kushirikiana na nchi mbalimbali za Kiafrika. Maeneo ambayo Marekani imeng’aa kuisaidia Afrika ni katika mapambano dhidi magonjwa ya malaria na Ukimwi. Pia Marekani imekuwa mstari wa mbele katika kuzisaidia nchi za Afrika kibajeti, kiulinzi, haki za binadamu na utawala bora. Eneo jingine muhimu ambalo Marekani imeelekeza macho yake Afrika ni katika ushirikiano wa kibiashara. Ni Katika ushirikiano huu wa kibiashara ndipo ambapo Marekani iliamua kuanzisha mpango na sheria maalumu iitwayo Africa Growth Opportunities Act (AGOA). 

Kupitia mpango na sheria hii, Marekani imekusudia kuimarisha ushirikiano wa kibiashara wenye usawa baina ya Africa na wao. Kabla ya AGOA ilionekana kuwa nchi nyingi za Afrika hazikuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye kukidhi vigezo vya kiviwango vilivyoko katika masoko ya Marekani. Mojawapo ya zana muhimu sana kupambana na umasikini ni biashara. Afrika inahitaji sana kuongeza uwezo wake wa kusafirisha bidhaa inazozizalisha kwenda nje ili iweze kugharimia maendeleo yake. Mbali na changamoto za ruzuku katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, fursa ya Afrika kusafirisha bidhaa zake katika nchi zilizoendelea ni finyu mno. 

Ukomo wa ujazo (quotas) unazuia kiwango cha bidhaa zinazoweza kuingia katika soko Fulani; na wakati huo huo ushuru unaotozwa kwa bidhaa hizo unazifanya bidhaa hizo kuwa gharama na zinashindwa kushindana katika masoko hayo ya kimataifa. Wakati mwingine viwango vya ushuru vinakuwa vikubwa mno kiasi kwamba Afrika inakwama kuendelea kuzalisha bidhaa hizo kwa kokosa masoko na ushindani.

AGOA ni njia mojawapo ambayo Marekani imeamua kuitumia ili kufungua masoko yake kwa Afrika. AGOA ilianzishwa mwaka 2000 kama sheria ya kibiashara inayokusudia kuongeza na kuhamasisha biashara baina ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Marekani. Katika sheria hii Marekani inaruhusu bidhaa kutoka katika nchi hizi kuingia nchini humo pasipo kulipiwa kodi. Tangu kuanza kwa mpango huu wa AGOA nchi nyingi zimeendelea kunufaika mno kibiashara.

Zaidi ya bidhaa 6,000 zimeorodheshwa kunufaika na mpango huu wa AGOA. Kimsingi ili nchi ipate fursa ya kuingizwa katika mpango wa AGOA inatakiwa iwe imetimiza masharti kadhaa ikiwemo kuboresha utawala wa sheria, haki za binadamu na kuheshimu haki na viwango vya wafanyakazi. Tanzania imekuwa ni moja ya nchi takribani 40 zilizokidhi vigezo, hivyo na hadi sasa imo ndani ya AGOA.

Baadhi ya bidhaa zilizomo kwenye orodha ya mpango wa AGOA ni pamoja na madini, mafuta, bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, bidhaa zilizoongezwa thamani ikiwemo nguo, viatu, vinywaji, Hii ina maana wakulima wa maua, wafugaji wa nyuki, ng’ombe na bidhaa zingine wote kwa pamoja wananafsi ya kunufaika na AGOA.

Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha bidhaa zinazoingia Marekani kutoka katika nchi za AGOA kimekuwa kikiongezeka kila mwaka tangu kuanzishwa kwa AGOA.  Inatajwa kuwa kiwango hicho kimekuwa kikiongezeka kwa wastani wa asilimia 30. Vile vile biashara baina ya pande hizi mbili imeongezeka mara tatu zaidi ya ilivyokuwa awali kabla ya kuanzishwa kwa sheria hii ya AGOA. Wajasiriamali wa Tanzania hatujachangamkia vya kutosha fursa AGOA kwa sababu taarifa zinaonesha kuwa nchi zinazooongoza kuitumia fursa ya AGOA ni zile za Magharibi mwa Afrika. Katika jumla ya thamani ya bidhaa zilizopelekwa Marekani za takribani dola bilioni 100, mafuta yanaonekana kuongoza. Ingawa nchi zinazozalisha bidhaa za kilimo, nguo na mashine za kimakenika zimenufaika pia.

Ingawa, AGOA ilipangwa kukoma mwaka 2008, lakini Marekani iliamua kupitisha marekebisho ya sheria ya AGOA na kurefusha mpango wa AGOA hadi mwaka 2015. Katika mpango na marekebisho haya inaruhusu nchi masikini kutumia malighafi za bei nafuu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya kutengeneza nguo na kuzipeleka Marekani.

Kila mwaka huwa kunaitishwa jukwaa la AGOA ambapo huwaleta pamoja viongozi wa kiserikali na sekta binafsi kutoka Afrika na Marekani. Jukwaa hili hufanyika jijini Wshngton kila mwaka na pia jukwaa hili hitishwa katika moja wapo wa nchi zilizokidhi vigezo kuwemo katika AGOA. Hadi sasa majukwaa ya AGOA yamefanyika mara nne jijini Washington, na mara moja moja katika nchi za Senegal, Ghana, Kenya na Zambia.

Kimsingi mpango wa AGOA umelenga kuwanufaisha wajasiriamali ambao ndio wanaotakiwa kuchangamkia fursa ya kuzalisha bidhaa na kuzisafirisha Marekani ambako licha ya kusamehewa ushuru lakini pia kuna masoko ya uhakika. Ni katika njia hii ndipo ambapo nchi yetu inaongeza thamani yake kwa kupata fedha nyingi za kigeni na kukuza uchumi. 

Wajasiriamali na makampuni yote yanayotaka kusafirisha bidhaa zake kupitia mpango wa AGOA, ni sharti wafikie vigezo kadhaa vya biashara za kimataifa ikiwemo kuwa na maelezo sawia na ya kina kuhusu asili (zinakotoka), ya bidhaa zenyewe.

Msafirishaji husika (kampuni, mjasiriamali) anatakiwa kujisajiri katika wizara husika katika nchi anakotoka. Kwa hapa msafirishaji atatakiwa kujisajiri katika wizara ya viwanda na biashara. Vile vile kunakuwa na hatua kadhaa za kufuata ili kupatiwa vibali vya kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi.

Vitengo katika serikali na ndani ya wizara zinazohusika na ufanikishaji wa mpango wa AGOA, kwa pamoja wanahitaji taarifa za wajasiriamali na haya makampuni kwa ajili ya takwimu, kudhibiti ubora na viwango vya bidhaa zinazopelekwa huko nje pale inapohitajika.

Nimebainisha hapo juu ya kwamba wajasiriamali na makampuni yana fursa za kusajiliwa na kunufaika na AGOA, hata hivyo pia niseme kuwa anayesajiliwa anaweza kuwa mzalishaji, mtengenezaji ama msambazaji wa bidhaa zilizopo kwenye orodha ya AGOA.  

Kwa upande wa Tanzania yeyote anayetaka kusajiliwa kwa ajili ya AGOA anashauriwa kuwa amejiunga ama kusajiliwa na mpango wa EPZ (Export Proccessing Zone). EPZ ni maeneo maalumu ya kiuchumi na kiuzalishaji yenye lengo la kuwasaidia wazalishaji kuongeza ubora wa bidhaa zao na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa katika maeneo hayo zinakadhi vigezo vyote vya kimataifa.

Vigezo rahisi vinahitajika katika kwa msafirishaji kujiunga na AGOA ikiwemo jina la biashara, majina ya wakurugenzi, orodha ya bidhaa zinazokusudiwa kusafirishwa kwenda nje, orodha ya malighafi zinazotumika na rejea zake za ushuru, ufafanuzi kuhusu bidhaa, mchanganuo gharama. Sio lazima mzalishaji, msambazaji ama mtengenezaji kuhangaika na kila kitu, isipokuwa inawezekana kuwatumia mawakala wa usafirishaji na uingizaji.

Serikali kupitia vyombo vyake vinavyohusika na biashara ikiwemo TRA vinatoa usaidizi na maelekezo ya kutosha sana kuwawezesha wajasiriamali wanaochangamkia AGOA. Katika vitengo hivi mjasiriamali anaechangamkia fursa ya AGOA atapewa nyaraka zote zinazohitajika ambazo zitamsaidia kupokelewa kwa bidhaa zake huko Marekani. 

Serikali kupitia vyombo vyake vya kibiashara vitakagua na kujiridhisha katika maeneo yafutayo kabla ya kutoa nyaraka na ruhusa. Watakagua maghala ya kuhifadhia, watasaidia kuidhinisha malighafi za bidhaa husika, watapitia takwimu za usafirishaji kwa mujibu wa taratibu za AGOA, watakabidhi vyeti na nyaraka kwa mjasiriamali.

Wajasiriamali wa Tanzania tunatakiwa tujiamini kwa kuchangamkia fursa za kimataifa ikiwemo AGOA. Hakuna sababu ya kujiweka kando na kudhani kuwa AGOA ni ya watu Fulani Fulani ama kudhani ni kwa ajili ya makampuni makubwa. Kila mjasiriamali ana haki ya kunufaika na AGOA mradi tu akidhi vigezo vilivyoainishwa. 

Tujenge mazoea ya kutembelea vitengo mbalimbali serikalini ikiwemo wizara ya viwanda na biashara ili kujifunza na kupewa maelekezo ya namna ya kunufaika na mpango wa AGOA. Mbali na kutembelea wizarani vile vile wajasiriamali wanaweza kutembelea kituo cha uwekezaji (TIC) pamoja na chemba ya TCCIA.

0719 127 901, stepwiseexpert@gmail.com

No comments:

Post a Comment

Maoni yako