September 18, 2017

HIMID MAO; NINJA ALIYEKABIDHIWA USINGA BADALA YA JAMBIA

NA HONORIUS MPANGALA

KATIKA makuzi ya kila mtoto katika familia,kitu cha kwanza ambacho mtoto ataiga ni yale matendo ya mama au baba. Wako watoto ambao wanajifunza hata kwa kificho kuvuta sigara kama mzazi wake anavuta na anamwona avutapo. Huku kunaitwa kujifunza kwa kuona katika makuzi ya mtoto baada ya kuzaliwa kama inavyoelezwa na wanasaikolojia wa masuala ya elimu ya awali kama muitaliano Maria Montessori.

Himid licha ya kuwa ninja kama aitwavyo lakini akiwa ninja nje ya filamu. Yeye ni kijana wa kizazi cha soka kakua na kujifunza kwa kuona kama ilivyo nyanja za ujifunzaji wa watoto akamwona baba Mao mkami akipendelea mpira nyakati zote. Mazingira hayo mtoto hakwepi kuiga anachofanya mzazi. Katika soka lake Himid amekuwa kiraka kwa kutumika katika nafasi nyingi uwanjani. Hii ni aina ya watu wanaopenda kujifunza Mara kwa Mara na kujaribu Mara kwa Mara.
  
Mwandishi wa makala haya akiwa na nahodha wa Azam FC, Himid Mao katika viwanja vya Jakaya Kikwete, Jijini Dar es salaam.
 Awali nilimwona akiwa kama kiungo mkabaji katika timu za vijana. Lakini akaja kucheza nafasi zote za beki hasa kulia na kushoto pamoja na kiungo mchezeshaji na kiungo wa pembeni pia. Akiwa kama kijana aliyepita katika njia stahiki ya vituo vya kulelea watoto yaani Academy. Huko ndiko unakopata mafunzo mengi yanayohusu soka ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Mchezaji utawezaje kuishi katika jamii inayokuzunguka.


Licha ya kuwa na jina la utani la kibedui huyu bwana ni kama kiongozi aliyeandaliwa tangu angali chini ya miaka 17. Hivyo hata Uninja wake humfanya apunguze makeke akiwa kama kiongozi awapo uwanjani. Himid kapita katika ngazi tofauti za uongozi kwa wachezaji wenzake. Mwaka 2008 alikuwa nahodha wa Serengeti Boys timu ya taifa ya chini ya miaka kumi na saba. 

Mwaka 2009 akawa nahodha wa Ngorongoro Heroes timu ya taifa chini ya miaka ishirini licha ya kuzidiwa umri na baadhi ya wenzake lakini alipewa unahodha. Haikuishia hapo katika msimu wa ligi kuu 2011/12 Azam fc wakaamua kumpa unahodha msaidizi nafasi aliyoitumikia chini ya Ibrahim Shikanda na John Raphael Bocco. 

Katika msimu wa 2017/18 Himidi anakuwa Nahodha mkuu wa Azam akipokea majukumu toka kwa swahiba wake aliyetimukia Klabu ya Simba. Katika timu ya taifa Kocha Salumu Mayanga aliona Mchezaji huyo awe msaidizi wa Mbwana Ally Samatta. 

Himid ni kiongozi aliyepita katika ngazi zote za kiuongozi. Wakati wakiwa Ngorongoro, Mbwana alikuwa chini ya Himid na sasa Himid yuko chini ya Mbwana. Unaweza kusema kuimba kupokezana lakini katika soka hakuna jambo geni katika masuala ya utawala na uongozi. Kuna wakati ambapo namwona kabisa Ninja akitamani kuonyesha uhalisia wa jina hilo ila 'usinga' unamfanya awe mpole zaidi. 

Katika kumbukumbu zangu hakuna kazi chafu ambazo nazikumbuka kama zile Tanzania dhidi ya Malawi nyumbani na ugenini.Katika dimba la Chichiri pale Malawi mwaka 2015 pamoja na Tanzania dhidi Algeria nyumbani na ugenini mechi zote hizo akiwa na Mwenzake Mudathir Yahya. 

Miongoni mwa muunganiko ambao kila mwanafamilia ya soka akikumbuka kiungo cha Himid na Mudathir anatikisa kichwa kwani kilitoweka kama kiungo cha Frank Domayo na Sureboy Salum Aboubakari. Mbuyu Twite anamkumbuka kwa mengi kila walipokutana eneo la kati ilikuwa Mzee mzima lazima apate huruma wa mwamuzi. Anacheza soka lote liwe la shoka au la kiungwana 'aste aste au nainai'.

Makuzi ya kiuongozi yanamfanya Ninja awe na maneno mazuri na yenye staha kama anahojiwa na waandishi kuzungumzia mchezo aliocheza. Ni manahodha wachache sana wanaoweza kuongea mbele ya kamera.Kwa bahati Ninja ameishi na kuona kupitia wengi kama ilivyo Nahodha wa zamani wa Tanzania na wa sasa wa Yanga Nadir Haroub Ally 'Cannavaro' wanautulivu mkubwa mbele ya kamera.
Kikosi cha Azam FC 2017-2018
Wakati haya ya kiuongozi yakimwondoa kwenye uhalisia wa jina la Ninja yako ambayo yatabaki kufanya jina liwe lake hasa akiwa uwanjani. Baada ya Bocco kupishana na 'Standing ovation' pale chamazi lakini naiona kesho ya Himid itakayopambwa na mabango ya kumwagia sifa kemkem. Kesho ya kila mmoja huandaliwa leo japo maandiko yanasema "iache kesho itajihangaikia yenyewe".

Yako mengi ambayo Himid anayahitaji akiwa Azam,moja na kuu ni kunyanyua kwapa kama ilivyofanyika kwa mtangulizi wake Bocco. Baada ya mchezo dhidi ya Simba nilimwambia kuna kitu nakiona rohoni mwako.Ilikuwa morali inayoonyeshwa na Azam inaanzia kwake kama kiongozi. Nasubiri siku kuona kwapa akizinyanyua na ule wimbo mtamu ambao wachezaji wa Azam hupenda kuimba niusikie, “popote tunakanyanga”. Tusubiri kuiona Azam ya Ninja anayecheza soka akiwa na usinga badala ya filamu na akawa na jambia.

+255628994409

No comments:

Post a Comment

Maoni yako