September 20, 2017

UCHAMBUZI WA KITABU CHA CARLO ANCELOTTI

KITABU: CARLO ANCELOTTI; QUIET LEADERSHIP;WINNING HEARTS,MINDS AND MATCHES.
WAANDISHI: CHRIS BRADY& MIKE FORDE
MCHAMBUZI: MARKUS MPANGALA

HAIBA ya kiongozi wa taasisi yoyote hubeba maana kubwa sana kwa watu anaowatawala. Haiba hiyo huweza kuleta matujndo bora au mabaya. Lakini jambo muhimu ni namna haiba ya kiiongozi yeyote inapotumika kuhamasisha,

kuunganisha na kuleta mafanikio makubwa katika taasisi yake.
Kitabu chetu cha leo ni “Carlo Ancelotti: Quiet Leadership: Winning Hearts, Minds and Matches” kilichoandikwa kwa lugha ya kiingereza na waandishi Chris Brady na Mike Forde.
Kitabu hicho kina jumla ya kurasa 336 na kuzinduliwa Mei 26 mwaka huu, kimechapishwa na kampuni ya Penguin Books Ltd na kupewa nambari ISBN-13: 978-0241258781.

Taasisi nyingi zina aina tofauti za uongozi. Kiongozi anapokuwa madarakani anakuwa na staili yake. Wapo wanaofurahishwa na wengine hukejeli au kumponda kwa madai hawezi kufanikiwa. Kwahiyo kila kiongozi anayo staili yake ya kuongoza Taasisi fulani au nchi.


Jambo la pili ni namna kiongozi anavyotumia nafasi yake kujenga uhususiano bora kati ya watawala, yeye na watawaliwa (watumishi). Namna ambavyo kiongozi unatumia nafasi yako kuhamasisha na kuwapa moyo watu ambao wana uwezo wa kufanya mambo makubwa, lakini wanakosa vitu vidogo vidogo tu; ikiwemo moyo wa kupambana.

Aidha, tatizo lao wanakosa mtu wa kuwahamasisha na kufungua vifua vyao viongee nini kinachowasumbua, na kutiwa moyo ili wazidi kusonga mbele. Napenda ujifunze kitu hapa leo.
Ancelotti anasimulia makuzi yake ya kimasikini nchini Italia. Anasimulia namna alivyocheza soka na baadaye kugeukia uongozi kupitia nafasi ya ukocha. Katika kitabu hiki anasimulia namna uongozi wa soka unavyoweza kuleta changamoto kwa taasisi mbalimbali pamoja na vyuo vya elimu.

Ancelotti anasema, “nilichagua kuongoza kwa njia za ukimya (Quiet Way) nilipokuwa meneja wa klabu za AC Milan, Real Madrid, Chelsea na PSG, ambapo sasa nipo Bayern Munich. Katika mfumo wa uongozi wengi wanadhani mbinu za uongozi zinazotumia ni dhaifu. Lakini mimi sifikiri kwamba njia niliyochagua ilikuwa dhaifu,”

“Kwanini uongozi wangu nasema ni ukimya? Unaweza kuongoza Taasisi yenye watumishi wenye hulka tofauti. watumishi wenye ubinafsi, chuki na wivu dhidi yaw engine, pia wana makuzi tofauti. inahitajika mtindo wa kipekee kuongoza na kubeba imani ya mafanikio. Ni namna gani unawatuliza watumishi wako katika mazingira magumu na pale wanapokosa utulivu,”

Carlo anakigawa kitabu hiki katika sura mbalimbali, zikiwemo “The Leadership Arc” (mbinu za kuongoza), na “The Product” (matunda ya uongozi). Mtu yeyote anayeingia kwenye menejimenti analazimika kusoma kitabu hiki na kujifunza mbinu za utawala.

“Unapokuwa kiongozi ni lazima uwe na mbinu za kuongoza, hiyo ndiyo ‘The Leadership Arc’. Na unatakiwa kuhakikisha kuwa unao watumishi wenye uwezo, nidhamu, na malengo yenye kuleta matunda mazuri kwa taasisi au shirika, hiyo ndiyo ‘The Product’.

“Utamaduni” (Culture), taasisi yoyote lazima iwe na utamaduni wake unaoeleweka kwa hadhira au wateja. Ni lazima utamaduni wa eneo husika ujenge mshikamano, kuunga mkono mipango ya watawala, na kuwapa wachezaji mahitaji husika na wakati sahihi, pamoja na kuhakikisha wanaweza kutengeneza urithi wa uongozi kwa vijana ili wawe na mwelekeo,” anasema Ancelotti katika utangulizi wa kitabu hiki.

“Katika mchezo wa soka kuna wachezaji ambao wameweka madaraja yanayotambulika. Wapo wanajiona wao ni daraja la Rivaldo (kwa kuwataja daraja la kwanza la wachezaji wa Kibrazil), na wengine hujiweka daraja la tatu kwa ubora. Wanaamini daraja la Rivaldo ni aina ya wachezaji ambao hawakai benchi (kuwa wachezaji wa akiba).

Kiongozi unatakiwa kufutilia mbali dhana hizo ili kuleta usawa na mshikamano.Carlo anatusimulia visa mbalimbali kupitia vitabu hiki, kuanzia uongozi wa mabilionea kama Roman Abramovich, Adiariano Gilliani, Florentino Perez na wengineo.

Moja ya kisa cha kusisimua ninachopenda kukishirikisha msomaji ni kile kinahcomhusu mshambuliaji mpya wa klabu ya Manchester United, Zlatan Ibrahimovich.

“Siku moja kabla ya mechi kubwa, mshambuliaji wa PSG (kabla hajahama) Zlatan Ibrahimovich aliuliza; ‘Carlo unamuamini Mungu?, Ancelotti alijibu ndiyo ana imani na Mungu. “Safi sana, sababu unatakiwa kuniamini mimi pia,” Baada ya mechi PSG ilishinda pambano lao.

Tujifunze; maisha yetu yanakuwa bora kuanzia mioyoni mwetu. Tunashindwa kwakuwa tunaiskiliza mno kando. Tujifunze kushinda mengi hata kama kuna wenye uwezo wa kutushinda. Mapambano ni kupambana, siyo kuketi chini na kulia.

©Nishani Media
Julai 13, 2017
Dar es salaam

No comments:

Post a Comment

Maoni yako