October 22, 2017

PHILIP EMEAGWALI: MWANASAYANSI YA KOMPYUTA ALIYEIPA KASI ZAIDI INTANETI TUNAYOTUMIA SASA.

NA KIZITO MPANGALA

SOTE tunafurahia kutumia mtanadao wa kimataifa “international network” ambapo kwa utaalamu zaidi wa lugha maneno hayo mawili yamefupishwa kwa kuchukua herufi tano za mwanzo za neno INTERnet na haerufi mbili za mwanzo za neno NETwork na kupata neno INTERNET yaani mtandao wa kimataifa, na katika Kiswahili tumetoho na kpata neno INTANETI.

Mtandao huo unatusaidia kwa kiasi kikubwa sana katika shughuli mbalimbali. Wapo waliotumia muda na maarifa yao kwa ajili ya manufaa ya ulimwengu wote. Mtandao huo ulipoanzishwa haukuwa na nguvu kubwa ya “kukata mitaa” ya dunuia yote hii, lakini leo mtandao huu una pilikapilika nyingi na sehemu nyingi duniani na una matumizi makubwa. Ada yako ya kutumia intaneti ni bando tu!


Leo tunaye Mnigeria Philip Emeagwali ambaye amechangia mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nguvu na kasi ya intaneti. Kumbuka kwamba yeye si mvumbuzi wa intaneti lakini kwa kifaa alichokibuni kimesaidia kuboresha na kuipa nguvu na kasi zaidi intaneti tunayofurahia sasa hivi ambapo tunaweza kuwasiliana. Hata hapa usomapo, intaneti imesaidia sana kupata maandiko haya!

Philip Emeagwali alizaliwa mwaka 1954 katika mji wa Akure nchini Nigeria katika jamii ya kabila la Igbo. Mwaka 1967 aliacha shule kutokana na vita vya Biafra  na alishiriki vita hivyo kama mpiganaji (askari) kwa lazima alipokuwa na umri wa miaka 14. Vita vilipomalizika alihitimu masomo ya sekondari kwa kufundishwa nyumbani na baba yake. Shule nyingi zilifungwa. Baba yake huyo alikosa fedha za kumlipia ada hivyo akaingia vitani Biafra. Wakati alipokuwa akifundishwa nyumbani na baba yake, alifundishishwa hisabati na kupewa maswali 100 kila siku na aliambiwa awe anayafanya kwa muda wa saa moja tu awe amemaliza! Hakika aliweza jambo hilo!

Katika zoezi hilo maana yake ni kwamba alikuwa anafanya kila swali kwa wastani wa sekunde 36 tu!

Philip anatushirikisha kumbukumbu ya maisha ya familia yake baada ya mapigano ya vita vya Biafra, ansema “tulikuwa tukiishi kama watumwa. Chakula tulikuwa mara moja tu kwa siku na wakati mwingine siku ilipita bila kupata chakula. Nilijitahidi kuwa na fikra ya kufanikiwa kimaisha ndio maana nilijijengea bidii” 


Alikuwa akiishi kwenye nyumba ambayo ni banda tu lililozungushiwa mabaki ya roketi zilizolipuliwa vitani Biafra. Alikuwa akijisomea kuanzia saa 6 mchana hadi usiku saa 4. Ndipo alipofaulu mtihani wa kujinga na chuo kikuu cha Oregon nchini Uingereza kwa udhamini. Alidhaminiwa kutokana na nia yake thabiti ya kupenda kujisomea vitabu na kujifunza zaidi.

Alijiunga na chuo kikuu cha Oregon nchini Uinngreza ambako alitunukiwa shahada ya kwanza ya Hisabati. Baada ya kumaliza masomo na kutunukiwa shahada ya kwanza ya hisabati nchini Uingereza, alienda jijini Washington DC nchini Marekani na baadae alitunukiwa shahada ya uzamili katika chuo kikuu cha George Washington katika uhandisi wa ubaharia na mazingira (Ocean & Marine Engineering and Ecology) na baadae alitunukiwa shahada ya pili tena ya uzamili katika chuo kikuu cha Maryland katika Hisabati Tumizi (Applied Mathematics). Aliajiriwa na mamlaka ya ardhi mjini Wyoming kama mhandisi.
Emeagwali alitunukiwa shahada ya uzamivu katika chuo kikuu cha Michigan nchini Marekani katika masomo ya Sayansi ya kompyuta. Baadae chuo hicho kilificha taarifa zake kutokana na rangi yake nyeusi, maana yake ni kwamba lilikuwa ni jambo la kibaguzi. Alifungua kesi mahakamani kuhusiana na hujuma hiyo ya kufichwa taafifa zake kwamba isijulikane kama alisoma hapo lakini kesi yake ilifutiliwa mbali kwa vigezo vileveile vya kibaguzi. Hakukata tamaa, alijiamini ya kwamba amesoma Michigan.

Kwa elimu yake ya mazingira (Ecology) alifanya uchunguzi wa kina jinsi nyuki wanavyotengeneza asali kwa haraka na kwa ufanisi. Baada ya kumalisha uchunguzi wake huo kwa siku nyingi alichapisha matokeo yake ambayo aliyaongezea nguvu kwa elimu ya sayansi ya kompyuta. Lengo lake lilikuwa ni kuunda kompyuta yenye kasi zaidi. Alifanikisha jambo hilo ambapo alitumia vifaa vidogo vidogo 65,000 vya kielektroniki kuunda kompyuta hiyo ambayo ndiyo yenye uweza wa kasi kubwa duniani na ndiyo inayofanikisha intaneti iwe ya kasi zaidi. Kompyuta hii (Supercomputer) yeye ndiye mbunifu wa kwanza. Ina uwezo wa kukokotoa toni bilioni 3.1 kwa sekunde moja.

Ni ngumu kueleza ni wanasayansi wangapi na wanahisabti wangapi walichangia kupatikana kwa intaneti. Hakika walikuwa wengi. Lakini nguvu ya kasi ya intaneti imeletwa na kuasisiwa na mwanasayansi huyu Philip Emeagwali. Philip ndiye aliyebuni kanuni (formula) inayoruhusu kompyuta nyingi kufanya kazi kwa wakati mmoja zinapotumia intaneti.

Alifanikisha pia kuunganisha kompyuta 8 kubwa na kupata kile tunachoita KOMPYUTA MAHSUSI (SUPER COMPUTER). Hii alifanikisha katika maabara ya sayansi ya kompyuta jijini Los Alamos ambapo wanasayansi waliomtangulia walikata yamaa kutokana na ukweli kwamba kompyuta walizokuwa wakitumia hazikuwa na kasi sana kwa kuwa walitaka kuunda kompyuta itakayoweza kulisisimua bomu la nyuklia lilipuke haraka endapo mitambo itasetiwa mbali na bomu lilipo. Philip alifanikisha jambo hilo kwa kuunda “SUPER COMPUTER” ambayo iliongeza kasi ya nguvu ya utendaji wa intaneti na hivyo leo hii zipo kompyuta za aina hiyo nyingi na ambazo zina uwezo wa kusisimua mabomu yalipuke. Uvumbuzi huu ulimfanya apate tuzo ya nishani ya taasisi ya elimu ya elektroniki ya Gordon Bell mwaka 1989.

Anakili kwamba familia yake ilikuwa masikini wa kutupwa duniani kati ya familia masikini zilizokuwepo duniani. Philip ndiye mwanzilishi na mboreshaji wa sekta ya mafuta nchini Marekani, ushauri wake wa kitaalamu kwa sayansi ya kompyuta ulifanyiwa majaribio na kuona ya kwamba unafaa na mpaka sasa ndio unatumika na unaiingizia serikali ya Marekani mabilioni ya dola.

Milinganyo amabayo aliiasisi kutokana na kipawa chake cha hisabati na ambayo inatumika katika mashine za kuchimba mafuta inapofanyiwa kazi huweza kukupa mwelekeo wa kiasi cha mafuta unachoweza kuchimba na kama unaweza kuongeza uzalishaji au kama uzalishaji unaweza kupungua basi milinganyo hii inakupatia majibu. Ni wakati wa wanafunzi wetu vyuoni kudadisi mambo na si kusoma tu kwa lengo la kushinda GPA ya juu! Tunao wanafunzi wengi wenye uwezo huu lakini mazingira yanawafunika au wanajifunika vichwa!

Philip anasifika sana kwa kuwa gwiji wa hisabati na mwenye bidii ya kujifunza bila kukata tamaa. Mara nyingi yeye hakupenda kuitwa gwiji kwani alidai gwiji ni baba yake aliyeuhamishia ugwiji kwake yeye. Philip anasema “wakati fulani silipendi jina hilo, yaani sipendi kuitwa gwiji kwa sababu watu wengi hudhani ugwiji upo kwenye hisbati tu, si kweli. Sidhani kama kila mmoja kati yetu anayo nguvu ya kujipa ugwiji yeye mweyewe, mimi sikuzaliwa nikiwa gwiji na sikufahamu kama itakuwa hivyo. Ugwiji ulipandwa na baba yangu ndani yangu, hivyo, baba yangu ndiye gwiji” aslisema akiwa katika mkutanao wa wazazi nchini Nigeria mwaka 1999.

Philip anaongeza na kusema “watu huniita mimi gwiji wa hisabati, lakini mimi nawaambia kuwa yeyote anaweza kuwa gwiji kama akikokotoa maswali 100 kwa muda wa saa moja”. Philip aliwasisitiza wazazi katika mkutano huo kuwa mtoto akipewa kazi kutoka shuleni akaifanya nyumbani waichukulie kwa uzito kwa kuwa kazi za nyumbani (home work) zina umuhimu kwa mwanafunzi yeyote duniani.

Wazazi na welezi, fuateni mfano huu wa Philip. Leo inaweza kuonekana ajabu sana mtu kujisomea nyumbani na kuweza kimasomo, unaweza kukumbana na falsafa za kwamba umefoji vyeti lakini hakika jambo hili la kujielimisha nyumbani linawezekana. Mnapaswa kuwaamini watoto wenu katika kujifunza. Igeni mfano wa baba yake Philip alipoamua kumfundisha Philip nyumbani na kuweza kusonga mbele. Hamishia kipawa kwa mtoto wako ili asonge nacho mbele.

Philip kwa sasa ana uraia wa Marekani na ana taasisi yake inayoshughulikia masuala ya mawasilianao. Mpaka sasa ametunukiwa tunzo zaidi ya 80.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako