VITUO viwili vinavyotoa huduma
za Tiba mbadala katika Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma vimefungiwa kutoa
huduma hizo baada ya kubainika zinaendesha huduma kinyume cha sheria za Tiba
asili na Tiba mbadala zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto. Vituo hivyo ni Ndulu Herbal Clinic kilichopo Mahenge
na Bethlehemu Samaritan Clinic kilichopo Mfaranyaki mjini Songea.
Vituo hivyo vimebainika
kuendeshwa kinyume cha sheria baada ya kufanyika ziara ya kushitukiza
iliyofanywa na timu ya watalaam wa Afya ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma Dk.Gosbert Mutahyabarwa kwa kushirikiana na timu ya watalaam toka
Manispaa ya Songea ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Mameritha
Basike.
Baada ya ukaguzi wa kina toka
katika timu mbili za wataalam wa Afya ngazi ya Mkoa wa Ruvuma na wa Manispaa ya
Songea umebaini vituo vya Ndulu Herbal Clinic kilichopo Mahenge na Bethlehemu
Samaritan Clinic kilichopo Mfaranyaki Songea vinapima wagonjwa kwa kutumia
kipimo cha Qantum Resonance Magnetic Analzer ambacho kimepigwa marufuku na
serikali.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
amesema vituo vyote vya tiba asilia viliandikiwa barua kutoka Manispaa ya
Songea kuacha kutumia kipimo hicho ambacho kinawarubuni wananchi kuwa wanaumwa
magonjwa mengi hivyo kulipa gharama kubwa kwa ajili ya matibabu ambazo ni kati
ya shilingi 150,000 hadi 300,000.
Hata hivyo vituo tiba vya asili
vimekaidi na kuendelea kutumia kipimo hicho kupima wagonjwa ambapo utafiti
uliofanywa na madaktari ulibaini kipimo hicho kinatoa vipimo vya uongo na
hakina viwango vya ubora.
Licha ya kutumia kipimo ambacho
kimepigwa marufuku,mapungufu mengine ambayo yamebainika katika operesheni hiyo
ni vituo hivyo kutumia watalaam ambao hawana sifa za kuwa madaktari na wahudumu
wa afya ambapo kituo cha Betherehemu Samaritan Clinic hakijasajiriwa.
Kutokana na mapungufu hayo
vituo hivyo vimefungwa kuanzia leo Novemba 10,2017 na mashine walizokuwa
wanazitumia zimechukuliwa na Idara ya Afya Manispaa ya Songea.
Hata hivyo vituo hivyo vinaweza
kufunguliwa iwapo vitafanyia marekebisho maagizo ya serikali kupitia Wizara ya
Afya kwa kuzingatia sheria,kanuni na miongozo ili vituo hivyo vitoe huduma
rafiki na salama kwa watumiaji.
Dk.Mutahyabarwa amesisitiza
kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo ziara za kushitukiza zitafanyika katika mkoa
mzima wa Ruvuma ili kulinda maisha ya wananchi kutokana na matumizi yasiokuwa
salama katika tiba asili na tiba mbadala.
©Songea Municipal.
No comments:
Post a Comment
Maoni yako