NIKIWA njiani kurejea Dar es
salaam, mdogo wangu Honorius Mpangala alinitumia ujumbe mfupi katika simu
yangu, “Aisee tupo Tingitingi, lakini nimeng’atwa na manyigu. Vifaa tulibeba
kama kawaida,”.
Nikashangaa. Sikufikiria kama
eneo lile laweza kuwa na manyigu au hatari zozote za wanyama wakali. Leo pichani
anasema, “Nikiwa najikagua mkono na miguu baada ya kung'atwa na manyigu saba. Ilikuwa
tarehe 25/12 saa saba mchana pori moja kando ya ziwa Nyasa.Pori lenye msitu
unaogota katika maji ukiwa na mawe makubwa huko ndo maskani ya wanyama kama
ngedere, nyoka, nungunungu, mijusi wa rangi rangi,ndege kama kanga pori na Kwale.
Baada ya shambulizi nilijiziba uso na kuacha sehemu ya miguu kuwa wazi lakini
ajabu niling'atwa hadi kwenye makalio,”.
Ninalifahamu pori hilo lilipo
kandokando ya Mlima Chipyaghela, upande wa magharibi wa kijiji cha Lundu.
Zamani tuliwinda ndezi na sungura pamoja na kutega mitego kunasa ndege. Tulipita
wakati tukienda kuoposha samaki na kugundua ujenzi wa ukuta wa mawe na eneo la
wazi kama pango.
KWANINI TINGITINGI?
Honorius na Kizito wanalichunguza
eneo la Tingitingi ambalo lilikuwa makazi ya askari wenyeji (Wampoto) waliokuwa
wakipigana vita dhidi ya wageni (Wangoni). Kuna mawe makubwa yamejengwa kufuata
mstari. Ni muundo wa ujenzi wa mapango ambayo yalitumika kujificha na makazi
yao dhidi ya adui.
Ukisoma kitabu cha “Pugu hadi
Peramiho 1888-1988” cha Shirika la Wabenediktine wa Peramiho wanaeleza kuwa “Wangoni
walipenda sana vita,” walikuwa na tabia ya kusafiri hadi baadhi ya vijiji vya
jirani na kulianzisha vita dhidi ya wenyeji.
Sasa eneo la TINGI TINGI lipo
kwenye forodha ya kijiji cha Lundu wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma. Bado hatujajua
kwanini liliitwa Tingi tingi. Haifahamiki kama limewahi kuandikwa au
kutembelewa na wataalamu wowote wa masuala ya kihistoria vyuoni hapa nchini au
nje. Lakini Honorius na Kizito Mpangala wanalichunguza eneo hilo kwa kina na
kujua nini zaidi ya ujenzi wa mawe wenye mpangilio wa makazi ya watu. Utafiti wa
kujitolea.
Bila shaka! Naamini watakamilisha
suala hilo. Nina imani wadogo zangu bado mnayo kiu ya kufanikisha angalau kujua
tu kulikuwa na nini au mna nini mle ndani ya eneo la wazi licha ya changamoto
ya wanyama wakali na manyigu. Tingitingi na baadhi ya maeneo(ambayo
hayachunguzwa wala kugunduliwa) ni sehemu inayoweza kuwavutia watalii pia.
Msirudi nyuma. Songeni mbele. Mkimaliza
mtaandika mengi.
Karibuni Lundu, Karibuni Nyasa.
NB: Wenye taarifa zaidi za eneo
la Tingitingi tunawakaribisha.
Markus Mpangala
Disemba 28/2017
Dar es salaam (Dasalamu kwa
sauti ya kingoni)
No comments:
Post a Comment
Maoni yako