January 11, 2018

AFYA, IMANI NA HUDUMA LUNDU

Hapa ndipo tunapopata busara za kiroho tuwapo kijijini kwetu Lundu (Nyasa). Lilijengwa mwaka 1946. Awali wamisionari walifanya makao yao katika mlima Chipyaghela (haupo pichani).
Eneo walilofanya makao mlimani hapo lilikuwa linakumbwa na upepo mkali sana nyakati za kiangazi, ndipo mwaka 1929 wamisionari hao wakiongozwa na Padre Adrian (Mjerumani) waliiomba serikali ya kijiji cha Lundu kuwashawishi wazee Machwembele na Lipondelu ambao walikuwa ni wa ukoo wa akina Mpangala.
Ni ukoo ulioshika maeneo mengi yanayoizunguka misheni kijiji cha Lundu. Basi baada ya serikali kuwashawishi wazee Machwembele na Lipondelu, waliamua kuwapa wamisionari eneo la kujenga kanisa la kuanzia na nyumba ya kuishi mapadre.

Wamisionari hao hawakuishia hapo tu, mwaka 1931 waliomba kibali cha kupata maeneo mengi zaidi, ndipo walipopewa umiliki wa maeneo fulani ambapo waliweza kujenga kanisa kubwa zaidi unaloliona pichani, nyumba ya kuishi masista (watawa wa kike), mradi wa maji kwa ajili yao ambao ulikuja kusaidia watu walioishi maeneo ya jirani na misheni hiyo.
Mradi wa mashine ya kusaga nafaka mbalimbali na kadhalika. Walihifadhi mazingira kwa kupanda miti mingi aina ya misonobali, migwina, na aina fulani ya miti ambayo inaitwa "Eucariptus". Sifa ya miti hii ni mikubwa, inahitaji maji mengi, inastahimili ukame, ina majani membamba. Nitakufahamisha mengi zaidi siku chache zijazo.

AFYA NI MTAJI
Ukoloni haukutucharaza viboko tu, lakini pia ulituweka kivulini. Nyuma yangu ni Dispensari iliyoko kijiji cha Lundu (Nyasa). Ni ukombozi mkubwa kwa afya za wakaazi wa kijiji cha Lundu na vijiji vya jirani licha ya changamoto mbalimbali zilizopo. Hata huduma ya kupima VVU (HIV) kwa sasa inapatikana hapa bure. Afya ni mtaji.
 © Kizito Mpangala.
0692 555 874/ 0743 369 108


No comments:

Post a Comment

Maoni yako