January 06, 2018

JIMBO LA NYASA: KWANINI WANANCHI WAISHI BILA HUDUMA ZA POLISI?

NA MARKUS MPANGALA, August 24, 2017 
JESHI la Polisi limepata Kiongozi mpya, Kamanda Simon Sirro. Kiubindamu Kamanda Sirro si mtu mpya kwakuwa anafahamika tangu makuzi yake. Kiuongozi Sirro anafahamika tangu akiwa askari wa cheo cha chini, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo na baadaye Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam.
Nikiwa nazungumza na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa.

Hii ni sehemu ndogo tu kumhusu Sirro ndani ya Jeshi la Polisi. Kwa maana hiyo kiongozi huyo mpya aliyechukua nafasi ya Ernest Jumbe Mangu anao wajibu wa kuendeleza na kuleta ufanisi wa utendaji wa Jeshi la polisi nchini.
Pamoja na hayo ninalo jambo linaloniogopesha mno kwenye jamii zetu. Nimechunguza kwa muda mrefu na baadaye kuchora picha ya miaka ijayo, kwamba ni kwa namna gani tutaendelea kuishi katika jamii ambayo haina vituo vya Polisi?

Ni kwa vipi wananchi wawe mbali na walinda usalama na mali zao? Ni kwanini wananchi washindwe kupata huduma za Jeshi la polisi nchini kwenye baadhi ya maeneo? Chukulia mfano maeneo yaliyoko mipakani, lakini hayana vituo vya jeshi la Polisi. 

Takwimu za Jeshi la Polisi zilizoko kwenye tovuti yao (www.policeforce.go.tz) zinaonyesha kuwa matukio ya uhalifu na ajali zilizoripotiwa kati ya Januari hadi Desemba 2015 ni 1,909,685.

 
Msemaji wa Jeshi la Polisi bwana Barnabas Mwakalukwa na Markus Mpangala
Aidha, takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la matukio ya uhalifu na ajali ni nyingi kuliko ripoti ya mwaka 2014. Mwaka 2014 matukio ya uhalifu na ajali yaliyoripotiwa ni 1,654,247. Ndiyo kusema ongezeko hilo ni matukio 255,438 sawa na asilimia 15.4. Idadi ya matukio ya uhalifu pekee yaliyoripoitiwa mwaka 2015 ni 519,203. Hata hivyo imeonyesha kupungua kwa uhalifu kwa sababu mwaka 2014 kulikuwa na matukio 528,575. Ikiwa na maana ni pungufu ya 9,372  sawa na asilimia 1.8.

Ripoti ya Jeshi la polisi ya mwaka 2015 imeonyesha aina tofauti za matukio ya uvunjaji wa sheria; uhalifu, ujambazi, uporaji,udhalilishaji, unyang’anyi na kadhalika. Kila mkoa unazo taarifa zake. Nafasi hii haitoshi kutaja mikoa yote na matukio yake ya uhalifu au uvunjaji wa sheria.

Hoja yangu ya leo ni namna ambavyo matukio kama hayo yanapotokea maeneo ambayo hakuna vituo vya polisi. Kwamba wananchi watalindwaje katikati ya wimbi la uhalifu? Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa Wilaya ya Nyasa inao wakazi 146,160. Chukulia mfano, katika wilaya ya Nyasa yenye na vijiji vyake,miji, vitongoji na kadhalika, nini kitatokea iwapo matukio ya uhalifu yatatamalaki huku vituo vya polisi havipo?
Kwa mfano, kutoka mji wa Lituhi hadi Lundu katikati hakuna kituo cha polisi. Kutoka kijiji cha Lundu hadi mji mdogo wa Liuli hakuna kituo cha polisi. Hiyo ina maana Tarafa ya Ruhuhu inacho kituo kimoja cha Polisi cha Lituhi. Ni kituo kidogo ambacho hakiwezi kutoa huduma katika tarafa nzima kwenye vijiji vyake.

Aidha, katika wilaya nzima ya Nyasa kuna vituo vitatu vya Polisi; Lituhi, Liuli na Mbamba Bay. Hii ina maana Lituhi iliyopo kwenye tarafa ya Ruhuhu inahudumia wananchi wa vijiji vya Lituhi,Njomole, Ndumbi, Liweta,Mbaha, Lundu,Kihanga, Ngumbo,Mbuli, Mkili, Nindai na Liwundi.

Ndiyo kusema katika tarafa nzima ya Ruhuhu kuna kituo kimoja cha Polisi. Vilevile katika tarafa ya Ruhekei kuna vituo vichache, kwa maana ya Liuli na Mbamba Bay pekee. Swali langu la msingi ni namna gani Jeshi la Polisi linaweza kuhudumia wakazi wa maeneo hayo? Ni kwa vipi wananchi wetu wataweza kupata huduma za ulinzi na usalama wakati wote au nyakati za matatizo?

Ninazungumza hayo kwakuwa mimi ni mwenyeji wa wilaya husika. Kwa mfano, unapofika njia panda kati ya wilaya za Songea, Mbinga na Nyasa katika kijiji cha Kitai ina maana ndipo unaachana na huduma za Jeshi la Polisi kwa ukaribu. Ukifika kijiji cha Amanimakoro kuna wawekezaji wa makaa ya Mawe kutoka TanCoal. Swali letu linarudi, ni kwa vipi katika maeneo hayo tunaweka ulinzi na usalama wa mali za wawekezaji na raia?

Mfano mwingine ni katika kijiji cha Ndumbi, kuna gati la bandari limejengwa hapo ambalo litatumiwa na Meli za Mzigo na abiria za Mv. Ruvuma na Mv. Njombe ambazo zimezidunduliwa hivi karibuni na waziri mkuu. Ni nani anahusika kulinda vifusi vya Makaa ya Mawe au usalama wa raia na mali zao? Namna gani tunaweza kuwahudumia wananchi wetu kwa ufasaha kabla ya kusubiri matukio ya uhalifu au vitendo vya uvunjaji wa sheria au matukio ya uhalifu?

Ninasema hayo kwasababu wakazi wa mwambao wa ziwa nyasa wanapakana na nchi ya Malawi kwa upande wa magharibi, na upande wa kusini wanapakana na Msumbiji. Ni kwa namna gani tunawapa huduma ya ulinzi wa usalama na mali zao? Ni lini tutatambua kuwa maeneo ya pembezoni yanahitaji kuwa na vituo vya Polisi kama sehemu muhimu ya kuimarisha ulinzi na usalama?

Jambo zuri ni kwamba jeshi la Polisi linaendesha mpango wa Polisi Jamii. Binafsi sijawahi kuona wala kusikia kuwa mpango huo unaihusisha wilaya ya Nyasa au jamii hiyo licha ya kutambua kuwa ni suala linalotakiwa kufanyika jamii nzima.

Tunaweza kusema matukio ya uhalifu na uvunjaji wa sheria hayafanyiki maeneo ya pembezoni au vijijini. Ni kweli, lakini itafaa nini kusubiri matukio ya uhalifu yajitokeze ndipo tuanza mikakati ya kukabiliana nayo? Kwa maoni yangu ni kwamba, nchi yetu italindwa kwa mikono, akili na nguvu zetu wenyewe. Ni muhimu maeneo kama hayo kuwekwa vituo vya polisi kama sehemu ya kwanza ya kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na rasilimali zetu kabla ya kuwatazama maadui wa nchi yetu. Hatujachelewa. Tuanze sasa kwa kujiuliza hivi jamii iliyopo mbali au isiyo na vituo vya Polisi inaishi namna gani?

MAKALA HAYA YALICHAPISHWA KATIKA SAFU YA “MAWAZONI” YA GAZETI LA RAI, TOLEO LA August 24, 2017. ISOME HAPA;

No comments:

Post a Comment

Maoni yako