UPANDE wa kushoto katika picha hii tazama jinsi mchanga ulivyojipanga. Haya ni matokeo
ya vipindi mbalimbali katika Jiografia ya ziwa Nyasa. Kipo kipindi ambacho
kikitokea mchanga huwa unasombwa na mawimbi na kupelekwa majini, hivyo unaweza
kuingia majini na kutembea meta 50 na zaidi halafu kina si kirefu kwa sababu
mchanga mwingi unakuwa umesambaa ndani ya maji. Kama unavyoona pichani, sehemu
kubwa ya mchanga inemegwa.
Na
kuna mchanga wenye rangi nyeusi inaying'ara nyakati za jua, pichani unaona
sehemu fulani ya mchanga ni mweusi, ni mchanga unaovutia kwa macho.
Kipindi
kingine ni kile kinachotokea halafu mchanga unarudishwa nchi kavu na
kutengeneza kitu kama tuta fulani wakati huo ndani ya maji ukiingia unaweza
kutembea meta 10 tu maji yakafikia shingoni, maana yake ni kwamba kina
kinaongezeka kutokana na mchanga kurudi nchi kavu. Haya yote hayafanyiki kwa mikono ya Wanyasa wenyewe bali ni mambo ya asili ya dunia hii. Ndivyo Jiografia hiyo ilivyo. Ni JIOGRAFIA YA KIUMBO yaani 'PHYSICAL GEOGRAPHY' (kwa Kimombo). Vipindi vilivyopo ni MBELU, LULENGA, na MUHWELA.
MBELU:
Ni kipindi cha mawimbi makali sana. Katika ziwa Nyasa kipindi hiki si rafiki sana kuogelea kwa sababu huenda ndani ya dakika chache tu unaweza kuuyumbisha ubongo ikiwa wimbi litakubamiza. Ni mambo ya asili tu. Ni Jiografia ya Kiumbo. Meli zetu hupata taabu sana katika kipindi hiki, hapo ujuzi wa nahodha unahitajika sana, na inashauriwa usimsemeshe nahodha akiwa anaendesha meli katika kipindi hiki. Wala hutakiwi kuvua samaki kwa usalama wako!
LULENGA:
Nj kipindi kinachoendana na MUHWELA kitabia, hivyo nibazungumzia tu Lulenga. Hiki ni kipindi ambacho mawimbi huwa si makali sana na ni ya wastani lakini kunakuwa na mkondo mkubwa sana kadiri unavyoenda mbali zaidi. Kipindi hiki ndicho kinachokwangua mchanga na kuuingiza ndani ya maji na hivyo kufanya kina kupungua kwa muda. Pichani unaona jinsi mchanga ulivyokwanguliwa.
Katika kipindi hiki meli hukumbwa na taabu ya aina yake. Kwa kuwa mawimbi hubadili mwelekeo, yaana badala ya kufika moja kwa moja mbela, yenyewe katika kipindi hiki huwa na mwelekeo wa pembeni. Ukisimama na kulitazama ziwa basi mawimbi huelekea kushoto au kulia kwa mkondo mkubwa hasa kilindini.
Basi ikiwa meli inahitaji kwenda upande wa kulia na mawimbi yakiwa yanakwenda kushoto basi napo usimsemeshe nahodha akiwa anaendesha meli kwa sababu atahitaji umakini, itabidi "afe kidogo" ndipo afanikishe zoezi hilo. "Kufa kidogo" ni fasihi tu, maana yake ni kwamba atatakiwa akielekeze chombo upande ambao mawimbi yanaelekea huku akitafuta mbinu kuushinda mkondo ule ba hatimaye aelekee upande aliokusudia. Jambl hili hutokea na nahodha hufanikisha misheni hiyo.
Kuyajua haya, usione aibu kutaka kujifunza jambo hata kama ni dogo. Katika shughuli za uvuvi inashauriwa usivae shati yenye vishikizo kwa kuwa nyavu inapokuwa kwenye maji huwa na nguvu sana na mara nyingi huelemewa na mchapuko (siyo MCHEPUKO) wa graviti yaani "gravitational acceleration", basi huelekea chini, hivyo ikiwa itakamata kwenye kishikizo basi uwe mwepesi kuiondoa vinginevyo itakuvuta kwenda chini. Haya yote na mengineyo ni Nyasa!
© Kizito Mpangala
No comments:
Post a Comment
Maoni yako