February 17, 2018

R.I.P AKWILINA, ETI MKOA WA DAR ES SALAAM UNA BARABARA ZA HEWANI ZA KUPITA DALADALA!!


 MIAKA mitano iliyopita nilipata kuandika kuwa, ‘utamaduni wa wananchi kupigwa risasi, kushambuliwa kwa riasi za moto, kushuhudia wapendwa wao wakifariki dunia mbele ya macho yao, kuna matokeo hasi yenye athari kubwa nchi yetu. 
 
Nilisema wananchi wanazoeshwa kupigwa risasi za moto. Wanazoeshwa kuuana. Watatamani kuuana. Watatamani kujiua. Wanazoeshwa kuchukia kwa vitendo vinavyoumiza mioyo yao.  

Mwishowe nilisema kuwa wananchi hawa wanapotenda jinai wakitumia mapanga, marungu au visu, jawabu ni kwamba wanatumia vitu hivyo kwasababu ‘hawana bastola wala bunduki’. 
Nilisema hali hii inachochea ghadhabu inayoota mizizi na kuumba tabia za chini kwa chini kiasi kwamba madhara yake hayawezi kuonekana haraka, lakini yatakuwa makubwa sana. 

Nimepokea taarifa za kufariki dunia mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji

katika shahada ya Manunuzi na Ugavi, Aqulina Akwiline (AKWILINA), mwenyeji wa wilaya ya Rombo, Kilimanjaro. Binti huyo anatajwa kuwa alikuwa anatumia usafiri wa daladala za kutoka Makumbusho kwenda Mabibo. Tumeambiwa risasi zilipigwa hewani. Kwahiyo mkoa wa Dar es salaam una barabara za hewani zinazotumiwa na Daladala?
SWALI; Hivi kama risasi zilipigwa hewani ina maana daladala hiyo ilitumia ‘Flyover’ ipi kutoka Gerezani (Kariakoo) kwenda Makumbusho via Mabibo? Aibu ilioje!
Pumzika kwa amani mrembo Akwilina.

--MARKUS MPANGALA©Andunje wa Fikra

No comments:

Post a Comment

Maoni yako