March 21, 2010

DIWANI YA FADHILI MTANGA a.k.a FADHILI MSHAIRI

Wasiwasi na Neno zuri.


Humkosesha mtu raha, wasiwasi unakera,

Huleta nyingi karaha, hata kw'ongeza hasira,

Huwezi fanya madaha, wafungwa nayo nira,

Wasiwasi.



Wasiwasi ni utumwa, wa kuusumbua moyo,

Huleta kama kuumwa, yale yakusumbuayo,

Moyo wahisi kuchomwa, kwa yale yautesayo,

Wasiwasi.



Wasiwasi unaghasi, unakosesha amani,

Kutengwa unakuhisi, kama mwokozi humwoni,

Huharibu mitikasi, na kukurudisha chini,

Wasiwasi.



Neno zuri ndiyo dawa, wasiwasi huondoa,

Furaha moyoni huwa, hofu yako kuitoa,

Faraja wewe kupewa, na raha isiyo poa,

Neno zuri.



Ni hedaya neno zuri, muhimu kwayo dunia,

Upatapo ni fahari, moyo wako hutulia,

Haliyo iwapo shwari, mamboyo wajifanyia,

Neno zuri.



Neno zuri ni muhimu, kila mtu ahitaji,

Kulipata kuna hamu, neno zuri hufariji,

Neno zuri kweli tamu, hulifaidi mlaji,

Neno zuri.

8 comments:

  1. Kaka,
    Moyo wangu mwingi wa shukrani,
    Kuniweka hapa kwako barazani,
    Hakika kabisa umenithamini,
    Mungu akujaalie nyingi ihsani,
    Daima akulinde na walo nuksani,
    Uwe na mafanikio nayo amani,
    Siku zako zote hapa duniani,
    Ukiondoka akupe hifadhi peponi,
    Hakika nasema tena shukrani.

    ReplyDelete
    Replies
    1. shairi kama uzuri wako nalipenda kulisoma so halipatikan cku izi

      Delete
  2. shairi limetulia kwa kweli watu wana vipaji hapa diniani.

    ReplyDelete
  3. God bless your way,
    The word you say,
    Poem is beautiful way,
    That make people live in the dream way,
    The poem end as I say,
    God bless your way.

    ReplyDelete
  4. God bless your way,
    The word you say,
    Poem is beautiful way,
    That make people live in the dream way,
    The poem end as I say,
    God bless your way.

    ReplyDelete
  5. kaka Fadhy tambua blogu yako imejaa utajiri kama ya mtakatifu Kitururu,
    yaani sijui niseme neno gani, ila nakwambia nakuthamini sana, blogu yako ni mgodi wa elimu kaka

    kesi yangu na wewe ni kuandika kitabu kuhusu mashairi yako, ngoaja nikamtonye dada Weshi Lema pale E&D limited akuchungulie kazi zako.

    FITA upooooooooo, how is UDOM kaka?

    piga kitabu kaka, uskonde

    ReplyDelete
  6. naogopa kupata kigugumizi endapo nami nitajaribu kuweka 'mistari'.

    ReplyDelete
  7. kaka Markus nakushukuru sana kwa ushauri wako. Toka ile siku umeniambia baada ya kuandika shairi la vijinopembe, nimekuwa nikiufanyia kazi ushauri wako. Nilikuwa nje ya Dar na sasa nimerudi. Nimeanza kuyapitia mashairi yangu yanayofiki 135 ili kuchagua walau nusu yake kama kitabu cha kwanza.
    Ninathamini sana mchango wako wa mawazo. Ninalifanyia kazi na nitawasiliana nawe hatua ninayopiga.
    Kaka Fita naye nasikia amekuwa mchapaji wa vitabu.
    Kaka John hata wewe waweza kuwa mshairi mzuri kabisa kabisa.
    Da Yasinta pamoja sana sana.
    Ahsante tena na tena kaka Markus.

    ReplyDelete

Maoni yako