September 25, 2012

Tunaomba kambi ya JWTZ, Katiba itamke mipakaWakazi wa Wilaya mpya ya Nyasa wameiomba serikali kuanzisha kambi za Jeshi la Wananchi nchini katika makao makuu ya wilaya hiyo, Mbamba Bay ili kukabiliana na hali mbaya inayoweza kujitokeza hapo baadaye.

Wakizungumza katika kongamano la Usalama wa raia, wakazi wa Wilaya ya Nyasa, wameiomba serikali kuangalia uwezekano huo ili  kuimarisha ulinzi wa mji wa Mbamba Bay ambao ni lango kuu la kuingilia kwa upande wa Tanzania kutokea kusini.

Wamesema kuwa ingawa serikali imepiga hatua katika mazungumzo yake na serikali ya Malawi, bado wakazi wa wilaya hiyo mpya wanaishi kwa hofu na wasiwasi mkubwa.

“Sisi wakazi wa mpakani hasa hapa Nyasa tunaishi kwa wasiwasi, tunaomba Jeshi la Ulinzi lije kuweka kambi maalumu hapa, tunafahamu wapo polisi, lakini wenyewe hawatoshi kwani tunahitaji ulinzi zaidi,” alisema mkazi mmoja wa Mbamba Bay

Kaika hatua nyingine, baadhi ya wakazi wa wilaya Nyasa wamebainisha maoni yao kuwa ni vema Katiba Mpya itakayopatikana hapo baadaye baada ya kuidhinishwa na Bunge la Katiba, itamke waziwazi mipoaka ya nchi yetu.

Wakazi hao wanasema kuwa pamoja na uhuru walionao kuingia nchi za Msumbiji au  Malawi bado kunahitajika uwazi zaidi na Katiba ya nchi yetu inalazimika kutaja mipaka ya nchi yetu ili kulinda mipaka na kuwa mwongozo wake.

Wamesema Katiba inatakiwa kuchukua nyaraka zote za mipaka na kubainisha mipakaya ndani ya nchi, na nje ambako tunapakana na nchi mbalimbali.

Wakitolea mifano Namanga, Sirari, Kasumulu, Tunduma, Mbamba Bay na mingine mkoani Kagera. Aidha, walisema kuwa ni lazima Katiba itamke kuwepo kwa Vituo vya kudumu vya Polisi katika vijiji vyote katika jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NB: maoni ya wakazi wa vijiji vya Tingi, Kingirikiti, Chiwanda, Kilosa, Mtipwili, Peramiho, na Mbamba Bay

No comments:

Post a Comment

Maoni yako