Wazee wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, wameunga mkono hoja ya serikali kwamba, mpaka wa Tanganyika na Malawi, upo katikati ya ziwa hilo, wakisema ndivyo walivyoelezwa na wazee wao walipokuwa vijana.
Walisema hayo mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipokutana nao ili kupata ushahidi kuhusu mpaka halali wa nchi hizo.
Waziri Membe akiongea na wazee wa Kyela katika ziara yake ya kuzungumza na wazee kuhusu mipaka ya Ziwa Nyasa. Picha: Subi Sabato/Wavuti
Mzee Edwin Kasirati (75) alisema alizaliwa na kulikuta ziwa hilo na wakati wakiwa vijana walielezwa na wazee wao kuwa mpaka wa Tanganyika na Malawi ni mto Songwe, ambao unaingia ndani ya Ziwa Nyasa.
Alisema mwaka 1961 Wamalawi wenyewe walikiri kwamba, mpaka ni katikati ya ziwa na mto Songwe.
Mzee Michael Mwang’onda (70) alisema tangu wakiwa wadogo walikuwa wakielezwa na wazee wao kwamba, mpaka wa Tanzania (wakati huo Tanganyika) ni huo huo uliopo katikati ya ziwa kama ilivyo na wameendelea kuulinda hadi sasa.
Alisema wanavyoelewa ni kwamba, Tanzania ndiyo inayomiliki eneo kubwa la ziwa hilo linalofikia theluthi mbili ya ziwa lote na Malawi wanalo eneo dogo ikilinganishwa hata na Msumbiji.
Mwang’onda alisema kama ni kulalamika, basi wangelalamika wananchi wa Msumbiji, ambao ndio wanafuatia kwa kumiliki eneo kubwa la ziwa na wala siyo Malawi.
wazee wa Kyela wakimsikiliza waziri Membe
Alisema hivi karibuni ziwa hilo limepanuka na kumega eneo lao, akidai kuwa hata makaburi ya mababu zao hivi sasa yamefunikwa na maji umbali wa zaidi ya kilometa mbili ndani ya ziwa Nyasa, hivyo haiwezekani ziwa lote ni mali ya Malawi.
Katika safari yake ya kukusanya ushahidi, tayari Waziri Membe amekwishapita katika mikoa ya ya Ruvuma, hususan wilayani Mbinga na Mbeya katika wilaya ya Kyela, ambako alikutana na wazee mbalimbali na kuzungumza nao.
Awali, akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mbeya, Waziri Membe alisema serikali haitarudi nyuma kushugulikia mgogoro wa mpaka baina yake na Malawi ndani ya ziwa hilo na kwamba, inataka kufikia mwaka 2015 suala hilo liwe limepata ufumbuzi.
Alisema licha ya Serikali ya Malawi kusuasua kuhudhuria vikao vya kuzungumzia mgogoro huo, Serikali ya Tanzania haitalifumbia macho suala hilo kabla ya kulipeleka katika Mahakama ya Kimataifa (ICJ).
wavuvi wakivua samaki katika ziwa Nyasa
Akiwa wilayani Kyela, Waziri Membe alizungumza na wananchi wa Kata ya Katumba Songwe na Matema akiwataka waendelee kuishi kwa amani na utulivu na asitokee mtu kwenda kuwatisha na kuwadanganya kwamba kuna hatari yotote katika mpaka huo.
Alisema serikali inalitambua tatizo hilo na inalifuatilia kwa makini ili kulipatia ufumbuzi na ndio sababu hivi sasa yeye anakwenda kwa wananchi na kuzungumza na wazee kwa nia ya kupata ushahidi utakapelekea kupata suluhu.
Alisema hata Rais Kikwete alitoa kauli ya kuwaahidi Watanzania kwamba, kabla ya kumaliza uongozi wake anahitaji suala hilo liwe limepata ufumbuzi ili wananchi wa eneo hilo waendelee kuishi bila wasiwasi, kwa amani na utulivu.
Aliwahakikishia wananchi hao kuwa hata kama suala hilo litapelekwa ICJ, lazima Serikali ya Tanzania itashinda kutokana na ushahidi unaotolewa na wazee katika maeneo mbalimbali anakopita. CHANZO: SOMA ZAIDI, HABARI ZINGINE SOMA HAPA KUHUSU NYASA NA WAZEE WA KYELA
CHANZO: HABARI NA EMMANUEL LENGWA
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
Maoni yako