January 15, 2013

MRADI WA MAJI KIJIJI CHA NG'OMBO WAKAMILIKA

Na Mwandishi  wetu, Ng'ombo
Wakazi zaidi ya 2450 wa kijiji cha Ng’ombo katika Kata ya Chiwanda wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wameondokana na adha iliyokuwa ikiwakabili ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji kijijini hapo,

Akizungumza na Lundunyasa Network, Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo Amos Mtweve alisema mradi huo ambao umejengwa kwa ufadhili wa UNDP kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira umegharimu jumla ya shilingi 298,346,700 na kwamba kuna vituo 23 ambavyo wakazi wa kijiji hicho watakuwa wakivitumia kupata maji.
Mhandisi Mtweve alisema kuwa kabla ya kujengwa kwa mradi huo wananchi walikuwa wakilazimika kutumia maji ya ziwa Nyasa kwa ajili ya kunywa, kupikia, na kuoga hali ambayo ilikuwa ikihatarisha usalama wa afya zao.
Alisema pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza wakati wote wa ujenzi wa mradi huo ikiwemo baadhi ya wananchi kutojitokeza kuchangia nguvu zao kama uchimbaji wa mtaro kwa ajili ya kulaza mabomba lakini bado mradi umekamilika kwa kwango kilichotakiwa.
“kukamilika kwa mradi huu kimsingi ni sifa kubwa kwetu kwani itawapa matumaini wafadhili wetu kufadhili miradi mingine hasa ikizingatiwa kuwa UNDP wamefadhili miradi michache ya maji hapa nchini ikiwemo huu wa kwetu,” alisema Mhandisi Amos Mtweve.

1 comment:

  1. TUTAFANYAJE SASA KATIKA NCHI HII YA MATESO NA UONEVU KWA WAPIGA KURA WAKE MASIKINI. INAUMA SANA TENA SANA!!!!!!!!. TUSHUKURU KWA YOTE HATA HUO MRADI.JAPO SITAJUTIA KAMWE KUZALIWA NYASA!

    ReplyDelete

Maoni yako