February 04, 2013

CHOMBEZO: WEKA MALENGO MAISHANI

Markus Mpangala

Ni mwenyezi Mungu anayetuweka hai kwenye hii dunia huku wenyewe tukichukua jukumu la kujilinda dhidi ya hatari zozote. Leo ninapenda kukuelezea jambo lililonishangaza zaidi ingawaje nilikwisha simuliwa nyakati fulani na baadhi ya wanazuoni, na lenye elimu muwali. Jambo hili ndilo linalenga kukuuliza maswali haya; wewe ni mfanyakazi kwenye ofisi fulani, hivi unafanya kazi ili iweje? Labda wewe huna kazi, unaishi ili iweje? Kwanini huna kazi au shughuli yoyote? Lau umri wako mdogo au hujapata kazi, unadhani kuna umuhimu wa kazi? Na kwanini unaona kuna umuhimu wa kuishi kama ulivyo? Wengine ni wafanyabiashara na mengineyo; hivi katika maisha yako una malengo gani? Yaani unaamka mapema, unakwenda kazini aidha kwa usafiri wako au wa jamii (Daladala).
Unakwenda ofisini kufanya nini? Lengo lako hasa ni nini kadiri mshale wa saa unavyokwenda hapa duniani? Unaishi ili kufanya nini? Kwanini unadhani una haki ya kuishi na si yule au mimi? Lengo lako la kuishi liko wapi? Sababu yako ya kufanya kazi iko wapi? Ndiyo, unapenda cheo, halafu iweje? Ukishakupata cheo hicho unalengo gani na maisha yako?
Unadhani cheo chako kitaisaidia nini ofisi yako? Kwanini wewe unapenda sana kupendelewa? Unapotaka kupendelewa je, wewe umewafanyia upendeleo wenzako? Unadhani ukipendelewa wewe ni muhimu kuliko yule na mimi? Lengo lako la kupendelewa ni nini? Unapenda kupewa kuliko wewe kutoa? Lengo lako ni nini hasa?

Jiulize sana msomaji ili tuende sambamba nikupe jambo hili. Tueleweshane hapa kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuweka malengo katika maisha yetu haya. Kama wewe huna ndoto basi hutafanikiwa. Kama wewe huna maono maishani, basi una kazi kubwa kujitambua. Una kazi kubwa ya kutambua uendako. Ni lazima uanze kufikiri sasa, maana mtu mwerevu huzifikiria hatua zake. Basi tusiende mbali msomaji mpenzi, nakupenda sana, tambua hilo.
Shaban akitimiza majukumu yenye malengo ofisini kwake
Sikiliza sasa, Aprili 19 mwaka huu nilinunua kitabu cha “Barrack Obama: Yes, We Can”, kimeandikwa na Lila Luce. Mambo yaliyomo kitabuni ndiyo yananifanya nitafakari nawe leo kupitia safu hii. Rudi juu anza kusoma upya halafu uelewe zaidi. Kwenye kitabu hiki kuna mambo ambayo sikujua kuhusu Rais huyu wa Marekani. Inachekesha na kuelimisha, lakini ukweli maisha aliyopitia Barrack Hussein Obama (jina lake la utani Barry O’Bomber) kuna mengi ya kujifunza.
Ukisema mitishamba, Obama amenyweshwa sana kule Kogelo, Kenya. Ukisema Daladala, basi Obama amepanda sana pale Kenya (huita Matatu). Obama alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya (teja) enzi za ujana wake, tafakari hilo.

Obama ana kauli mbiu ya “Mabadiliko”. Mabadiliko ni dhana ambayo ilitokana na aliyoona na kuishi maishani mfano Kogelo na Indonesia. Tusione Obama anaongoza Marekani, alilumbana na mkewe (Michelle Obama) kwa wazo la Urais. Michelle akamwita msaliti, hamwelewi anafikiria nini juu ya familia, alimwambia; “mume wangu nitawezaje kulea mabinti hawa wawili (Natasha na Malia) peke yangu?

Lakini Obama alimjibu mkewe, “tafadhali hii ni mara yangu ya mwisho, kabla ya kuishi kwa utulivu mke wangu, niruhusu.” Msomaji unapaswa kutambua kuwa wakati anagombea kuwa Useneta alitofautiana na mkewe, lakini aliruhusiwa kwa ahadi hatawania kiti kingine.
Obama anakufunza mengi; alifundishwa imani ya Ukristu na akawa mkristu, akajifunza Uislamu alipokuwa Indonesia, kwahiyo dini zote kazipitia kabla ya kufunga pingu za maisha kwa Mchungaji Jeremiah Wright. Alifundishwa mila na desturia za Wamasai. Alishatumia Vibatari kule Kogelo, Kenya. Alitembea kwa miguu vijijini, hakika ni mengi mno. Hata hivyo kauli aliyomwambia mkewe wakati anaomba amruhusu kuwani Urais ndiyo inatuleta hapa leo msomaji.

Awali alisema, ‘Nimeona nafasi ya kushinda’. Hii ilitokana na malengo yake aliyoweka ili kutimiza ndoto zake. Akamjibu mkewe, ‘hii ni nafasi ya mwisho mke wangu. Nahitaji kuyafanyia kazi mawazo yangu kabla sijatulia na kuishi kwa amani kwenye familia yetu.”  
Hii inakuonyesha ndoto zake maishani. Inakuonyesha malengo yake maishani. Inakupa mwanga wa kutengeneza sura mpya na kuacha ya kale. Inakupa matumaini mapya ambayo lazima utayatendee kazi.
Rafiki yangu Shaban a.k.a Don King, akiwa ofisini kwake
Lazima uwe na malengo maishani msomaji. Ujue dhumuni lako maishani. Tambua hakuna aliyeandikiwa kufanikiwa au kupewa uhalali wa kukusanya mafanikio yote. Hayupo binadamu aliyeshushiwa mafanikio kutoka mbinguni bila kuweka mkazo kwenye malengo yake. Anza kutimiza ndoto zako kwa kuweka malengo yafanyayo kazi. Amini juhudi zako na mawazo yako ni muhimu mno kwa jamii. 
Jamii inahitaji mawazo yako ambayo unatakiwa kuyatendea kazi. Fanya kazi kwa bidii ukiwa unajua dhumuni lako ni lipi. Tumia kipato chako kwa uangalifu maana huwezi kujenga nyumba ukiwa mwingi wa starehe. Wapo wajinga wachache hawaweki akiba na kila kukicha wanalalamika maisha magumu. Ndugu yangu kama huna malengo maishani ni bure. Utaishi kulingana na mazoea tu yaliyomo.
Unakwenda kazini, mwisho wa mwezi ukifika mshahara wote unalipa madeni. Halafu eti unataka kulingana na tajiri wa Mexico Carlos Slim au Tokyo Sakswalle wa Afrika Kusini. Mafanikio hutengenezwa, katu mafanikio hayakutengezi wewe. Ukitaka kufanikiwa lazima ujue njia zake halali na kubuni mpya ambazo zitakupa sura mpya ya maisha yako. Ndoto zako zitakupa msukumo wa kufanikiwa.
Anza sasa kupanga vipaumbele. Pima kipato chako kama kinakuruhusu kufanya yanayokuzidi. Mawazo yako mazuri yakuongoze ili ufanikiwe. Tumia 80% kufuatilia fursa zilizopo na mpya.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako