February 04, 2013

WADAU WA HANDENI KUKUTANA IJUMAA LEADERS CLUB


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKAZI wa Dar es Salaam wenye asili ya wilayani Handeni, mkoani Tanga, pamoja na maswahiba zao, wamepanga kukutana Ijumaa ya Februari 8, katika Viwanja vya Leaders Club, kuanzia saa 10 za jioni ili kutafuta namna ya kusaidia watu wasiojiweza wilayani humo.
Kikao hicho ni cha kwanza kufanywa na watu wa asili ya Handeni, katika jiji hili ambalo wananchi wengine kutoka mikoa na wilaya mbalimbali wamekuwa wakikutana na kujadili hali ya maisha inayowakabili.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mmoja wa wajumbe wanaoandaa kikao hicho, kilichopewa jina la ‘Handeni Kwetu’, Kambi Mbwana, alisema kwamba kukutana kwa wadau hao ni sehemu maalum ya kutafuta namna pia ya kusaidiana na viongozi wao kwa ajili ya maendeleo yao.
Alisema kwamba Wilaya ya Handeni imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya kila aina, ikiwamo njaa na shida ya maji, hivyo kwa wananchi hao kukutana pamoja, wanaweza kupata ufumbuzi katika baadhi ya mambo.
“Wakati Handeni ikiendelea kutajwa kama wilaya zisizokuwa na maendeleo kwa miaka 51 ya Uhuru, sisi tunakutana na kutoa kauli moja yenye tija kwa watu wote.
“Bila kuangalia nafasi zetu, vipato vyetu au heshima katika jamii, naamini moyo tu wa kukaa na kuzungumza au kuimba wimbo mmoja wa maendeleo, naamini mambo yatakuwa mazuri, hasa pale kitakapofanyika kilichojadiliwa na wote,” alisema.
Handeni, inayoongozwa na Muhingo Rweyemamu kama Mkuu wa Wilaya na Mbunge wake Abdallah Kigoda, imetajwa kukumbwa na baa la njaa na kulazimika baadhi ya wakazi wake kulalia mboga mboga pamoja na shida ya maji, jambo linalohitaji kujitolea kwa kila mmoja kwa nafasi yake.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako