April 12, 2013

C.C.CM ITUBU DHAMBI HII YA UDINI

Daniel Gingo


Nayaandika haya nikiwa katika ardhi ambayo usalama wa raia wake umejaa mashaka sana. Ni katika ardhi ambayo Dr. Ulimboka alitekwa na kuteswa vibaya, ni katika ardhi ambayo kabla hatujasahau ya Ulimboka Mwandishi wa Habari Daud Mwangosi alikufa kifo cha Kikatili kuwahi kukiona duniani, na wakati tunaendelea kuwa wenye mashaka juu ya jambo hilo Mhariri Absalomu Kibanda alitendwa aliyotendwa.

Na hawa ni wale ambao wanajulikana, hatujui wakina kajamba nani wangapi wametendwa yapi! Naandika nikiwa nayajua hayo!!

Ikitokea kuandika kwangu kukapelekea wahusika kunichukia na kuniondoa duniani, basi heri waniue lakini ukweli usimame, na kama nitatoweka ninyi mtakaobaki simameni na kweli hii!

Nakiandikia Chama Cha Mapinduzi nchini Tanzania, chini ya Mwenyekiti wake Jakaya Mrisho Kikwete, chini ya Katibu Mkuu Adullahman Kinana, Makamu Mwenyekiti Bara Philip Mangula, na Katibu Itikadi na Uenezi Nape Moses Nnauye. NARUDIA TENA, KAMA NITADHURIKA KWA KUUSEMA UKWELI HUU BASI MTAKAOBAKI SIMAMENI KA KWELI HII.

Wanafiki na Wazandiki watakataka kujipendekeza ili siku zao zisonge mbele watasema ninaichukia CCM, wataongeza na kusema ninachukia Rais Kikwete. Waache wafikiri hivi, lakini ukweli nitausema leo!

MIGOGORO YA KIDINI inayoendelea hapa nchini ni zao la mbegu ambayo CCM ilipanda katika uchaguzi mkuu uliopita. Kama kuna watu wanauana na kuchukiana sasa hivi kwa misingi ya kidini, CCM chini ya uongozi wake wote hauwezi kukwepa lawama hizi.

Walipokuwa wakitumia dini katika kutafutia kura walidhani ni jambo rahisi sana, walionywa lakini wao wakadhani wanaikomoa CHADEMA.

UDINI tunaoushuhudia sasa hivi hapa nchini CCM inahusika. Wana mambo mawili ya kufanya kama tiba, nami nitayaeleza:

1. Waungame kuwa kweli walihusika
2. Watubu (waache kutumia udini kutafuta uhalali wa kutawala, kwa sababu madhara yake ni kwetu sisi tusio watawala.
Noeni panga, chongeni mawe, andaeni silaha zote kama mnadhani kuusema ukweli huu kutanistahili adhabu, lakini nasisitiza CCM ITUBU DHAMBI HII AMBAYO WATANZANIA SASA WANAYAONA MADHARA YAKE!

Kwa mkono wangu mwenyewe
Daniel Gingo
Dar es Salaam - Tanzania.

1 comment:

  1. Karibu Nyasa kazi yako nzuri saaana, kaza buti Mpangala. Jukumu ni moja tu, kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi inayoridhisha. Vichua uozo, elekeza na bashiri mazuri kwa kutumia yale yaliyopita na halihalisi ya sasa. Nduguyo Juma Nyumayo, Songea

    ReplyDelete

Maoni yako