June 28, 2013

TAIFA STARS NA MASHINDANO YA CHAN


Timu ya Taifa, imeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha michuano ya kuwania kufuzu kwa kombe la dunia nchini Brazil mwakani baada ya kufungwa mabao 4-2 katika dimba la Taifa, jijini Dar es salaam. Wakati Stars ikipoteza nafasi hiyo, timu jirani za Uganda na Ethiopia zinakaribia kufuzu katika hatua ya mtoano ambayo itajumuisha timu kumi. 
 
Katika kundi C, Stars inashika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 7, huku Morocco ikiwa nafasi ya pili ikwia na pointi 8. Ethiopia na Uganda zipo kwenye nafasi nzuri kufuzu kwa hatua ya mtoano ambayo itafanikiwa kutoa timu tano zitakazofuzu michuano ya Kombe la dunia. 

Iwapo mambo hayatabadilika kwa Ethiopia basi itakuwa imepiga hatua kubwa sana katika michuano hiyo. Ethiopia imeingia matatani baada ya shirikisho la soka duniani (FIFA) kuanzisha uchunguzi dhidi yake kwa tuhuma za kumpanga mchezaji asiyeruhusiwa. 

Ethiopia ambayo iliichapa Afrika Kusini mabao 2-1 wiki iliyopita katika pambano la kuwania kufuzu inachunguzwa na Kamati ya Maadili ya FIFA, huku ikiwa imebakiza mchezo mmoja katika kundi lake. 

Ethiopia inachunguzwa kutokana na mechi yake dhidi ya  Botswana iliyofanyika Juni 8 mwaka huu.  FIFA pia inazichunguza Togo kwa kosa la kumchezesha mchezaji asiyeruhusiwa kwenye mechi yake ya Juni 9 mwaka huu.
Nayo Guinea ya Ikweta inakabiliwa na adhabu kutokana na kosa kama hilo kwenye mechi yake dhidi ya Cape Verde iliyofanyika Machi 24.
Naam, tukirejea pambano la Stars na Ivory Coast tuliona tofauti fulani kati ya wachezaji wetu na wale wa Ivory Coast. Stars ilijaribu kulitia msukosuko lango la Ivory Coast na kwa hakika kikosi cha Kim Poulsen kinastahili pongezi kwa juhudi zao. 

Hata hivyo kueondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho sio mwisho wa mashindano. Stars inakabiliwa na mashindano ya CHAN ambayo yatafanyika nchini Morocco mwaka huu, hivyo pambano letu dhidi ya Gambia nalo lina umuhimu mkubwa kama tulivyoanza mechi zingine za Kundi C.

Michuano ya CHAN inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani itakwua fursa nyingine ya kuweza kujipa uzoefu wa mashindano ya kimataifa. Katika michuano hii Stars italazimika kuongeza wachezaji wengine, badala ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengi wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC). 

Mashindano ya CHAN yana umuhimu mkubwa sababu yanafanikisha kuibua vipaji vipya vya soka. Tulishiriki mashindano hayo nchini Sudan tulipokuwa chini ya Marcio Maximo, na tulionyesha kila aina ya ujuzi mashindanoni. 

Kim Poulsen ameonyesha mwelekeo wake katika kukijenga kikosi cha Stars, na uhakika wa kuwa washiriki wazuri wa CHAN ni mkubwa mno. Hebu tujikumbushe ni kitu gani kilichotokea kwenye pambano letu dhidi ya Ivory Coast. Stars ilifungwa bao la kwanza na Ivory Coast kwa sababu kubwa moja tu, kuzubaa. 

Wakati safu ya ulinzi ikianza kuekelea mbele huku tukitegemea kucheza ‘offside’, Yaya Toure aliingia eneo la hatari haraka sana na kuvunja mtego wa kuotea. 

Bao la nne la Ivory Coast ni somo jingine kwetu. Wakati tukiwa tumeshampoteza Shomari Kapombe, Kocha Kim Poulsen alijua hakuna sababu ya kujilinda, akamwingiza kiungo mshambuliaji, kisha safu ya ulinzi ikabadilika na kucheza mabeki watatu. 

Hii ilikuwa na maana Erasto Nyoni alitakiwa kwenda kushoto, kisha Nadir Haroub na Kevin Yondani wakigawana majukumu ya ulinzi. Cannavaro akilinda kutoka eneo lake kwenda kulia huku Yondani akilinda kuelekea katiti hali ambayo ilimfanya Frank Domayo arudi eneo hilo mara kwa mara kusaidia ulinzi katika 3-4-2-1. 

Kwa mfumo wa mabeki watatu ulikuwa mzuri, na Ivory Coast walituzidi jambo moja, uzoefu katika mbinu husika. Walifahamu kuwa watacheza mashambilizi ya kushtukiza, na hilo lilionekana tangu mwanzo wa kipindi cha pili. 

Bila shaka Kocha wao Sabri Lamouchi alifahamu ukali wa Stars.Wachezaji wote Stars walipigania ushindi, walitaka timu yetu iibuke na pointi tatu, lakini mambo hayakwenda vile ilivyotakiwa na tumeshidnwa kwenda Brazil. Kwa sasa hatuna sababu ya kuendelea kulia machozi, bali ni kuangalia mashindano ya CHAN. Na huo ndio mpango mzima.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako