June 13, 2013

ULINZI NA USALAMA WETU:


Na Edgar Mwandemani

Leo naomba nijitumbukize katika mjadala mgumu kidogo. Ni hili suala la ulinzi na usalama wa watanzania na mali zao. Natambua kuwa hapa nchini tunavyo vyombo vilivyokasimiwa majukumu ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao upo, unadumishwa na kuondoa aina yoyote ya tishio dhidi ya raia.

Tunalo Jeshi la Polisi, JWTZ, JKT, Magereza, Uhamiaji, Usalama wa Taifa kwa kutaja vichache. Vyombo hivi pamoja na mambo mengine vinahudumiwa na kodi za raia ili vitulinde lakini vyote pia vinaundwa na raia wa nchi hii. Kwahiyo, usalama wa raia ndio usalama wa vyombo hivi.

Nijielekeze kwenye lile nililotaka tujihoji. Siku za hivi karibuni kumeibuka mlolongo wa matukio ambayo yanatuingiza shakani kama nchi, japo inaonekana ni matukio yanayolenga kundi fulani tusipongalia yatasambaa na kumhusu kila raia.

Ukiondoa matukio ya vifo na majeraha yanayotokana na vurugu za raia, mapigano baina ya makundi kama wakulima na wafugaji, vifo vilivyotokana maandamano na migomo. Ni dhahiri kwamba katika maeneo fulani majeraha na vifo ni matokeo ya mikakati madhubuti inayopangwa ama na watu binafsi, vikundi au taasisi zetu rasmi ambazo kwa upande mwingine zilipaswa kuhakisha hayo hayatokei.

Matukio ya kuumizwa na kuuwawa kwa raia wasio na hatia wakiwa katika himaya za vyombo vyetu vya ulinzi na usalama yameongezeka nitakumbusha machache tu. Wale wafanyabiashara wa vito "kesi ya Zombe", yuko dereva teksi pale Kimara, kijana mwingine aliwawa kule Chunya akiwa kituo cha polisi. 

Unyama dhidi ya waandishi Saed Kubenea na Ndimara Tigambwage, Dr. Stephen Ulimboka, Daudi Mwangosi kule Iringa, na hivi karibuni mwandishi Absolom Kibanda. Huyu wa mwisho ameweza kutoka hadhani na kutuambia "haya yote ni matukio ya kupanga kutokana na namna yanavyojitokeza" na akahoji kuwa pamoja na ahadi nyingi kwamba "tutahakikisha wahusika wanakamatwa mara moja na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria" hakuna lililokwisha kufanyika akichukulia mfano wa tukio lililomkumba yeye binafsi.

Inawezekana tukaona matukio haya yote hayatuhusu, lakini nina hakika kuwa iko siku sisi sote tutahusika kwa sababu tumekubali utaratibu huu ndio uongoze maisha yetu. Hatuwezi kudumu katika vurugu hizi harafu siku moja zisiiangamize jamii nzima!

Kwanini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kushindwa kushughulikia wahalifu hawa wanaoumiza, kutesa na kuua wasio na hatia. Je, vinataka tuamini kuwa navyo vinahusika na uchafu huu unaondoa hali ya amani na utulivu. Hali inayokaribisha ile dhana ya "survival for the fittest". Tujiulize itakuwaje pindi kila raia atakapochukua jukumu la kujilinda mwenyewe?

Mbaya ya jambo hili ni kuwa hivi sasa limefanywa ni silaha ya kisiasa. Hivi sasa pande zinazohusika katika siasa za nchi hii zimekuwa haziishi kutuhumiana kwa mauaji na utesaji. Kila upande umekuwa ukieleza kuwa una ushahidi na unawajua watekelezaji wa unyama huu. Na wengine wamekuwa wakiwatumia wahanga wa matukio haya ili kuendeleza agenda za kisiasa ikiwemo kuonyesha ubaya wa upande wa pili.

Muda wote huo sisi kama raia tumekuwa tukichekelea na wengine kushabikia upuuzi huu, huku upande wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ukiwa hauonekani kushtushwa na hali ya mambo. Ni kutokana na hali hii wahanga wa matukio haya wameanza kujilinda kwa makundi yao: waandishi wanalia kivyao, viongozi wa dini nao wanabaki kulalama; raia kule mtaani nao hivi sasa wameanza hata kuvamia na kuchoma vituo vyetu vya polisi kwa hisia kwamba vimepoteza maana. Wakati wa matukio ya kule Mtwara inaelezwa kuwa gari la Afisa usalama lilitekezwa kwa moto.

Naomba tushirikiane katika tafakuri hii juu ya hali ya ulinzi na usalama wetu, huku tukiendelea kudadisi yaliyomo katika rasimu ya Katiba iliyotoka hivi karibuni

No comments:

Post a Comment

Maoni yako