July 06, 2013

FILAMU ZETU NA UTATA WA MAJINA-2


WIKI iliyopita tulijadili juu ya matatizo ya filamu zetu katika uteuzi wa majina na matumizi ya lugha. Jambo la pili tuliona namna filamu hizo zilivyotongolewa kutoka kwa filamu za nje. Tulitaja filamu mbalimbali, na sasa tuendelea zaidi ya tulipokomea. Kwa mfano filamu za ‘Deception’, imechezwa na marehemu Steven Kanumba na Rose Ndauka. 

Lakini jina la filamu kama hiyo lilishawahi kutolewa na waigizaji Michelle Williams, Hugh Jackman, na Owen Macgregory. Kwenye hadithi ya filamu ya Bongo tunaambiwa mke anatoka nje ya ndoa yake na kupata bwana wa pembeni, lakini wakiwa kwenye matembezi yao mwanamke anauwa. 

Upelelezi unafanyika kisha muuaji ni mume halali wa mke. Lipo funzo kwenye filamu ya Kanumba na Ndauka, lakini itoshe kusema kwenye Deception ya Owen Macgregory na wenzake, tunaambiwa kulikuwa na danguro wanaliita The List, ambalo lilianzishwa na marafiki wawili.
Baadaye mwanamke mmoja anatoweka na kiasi kikubwa cha pesa. Hata hivyo ni mpango ambao unagundulika vilevile ambavyo muuaji anayetajwa na filamu ya Kanumba na Ndauka. Filamu nyingine ni ‘The Bestman’. 
Kwenye filamu hii tunakutana na masuala ya ndoa na mapenzi kati ya Robin na Lance, pamoja na Jordan. Mapenzi yanayosimuliwa kwenye filamu hii hakuna tofauti na The Bestman ilitotolewa hapa Bongo ikiwa na maudhui yaleyale ya ‘bestman’ wa harusi anampindua bwana harusi na kumchukua bibi harusi. 

Mwishowe filamu hiyo inaonyesha kuwa mauaji yanatokea, vivyo hivyo kwa filamu yetu ya Bongo, ambapo Gabriel (Mlela) anarejea kutoka masomoni nje ya nchi kwa ajili ya kuwa Best Man, siku mbili kabla ya ndoa hiyo ya rafiki yake Morris (Hemed) na Noreen (Mariam) lakini siri iliyofichwa na Gabriel & Noreen kwa muda mrefu inafichuka. 

Ni kisa kilekile kichosanifiwa kwa kusema Gabriel alikuwa masomoni ughaibuni, lakini filamu yenyewe fani na maudhui yake haykuna tofauti na The Bestman ya akina Lance na Jordan. Kuna filamu nyingine ya What Is It ambayo iliingia sokoni hapa Bongo muda mrefu kidogo. Lakini maudhui ya filamu hii yanashabihiana na visa alivyotengeneza Crispin Glover. 

Tofauti yenyewe ni kwamba Glover ameongeza suala la visa vya kishetani, lakini mikasa inayotokea inalingana nay ale yaliyoko kwenye filamu ya Bongo. Pengine watetezi watasema ni mgongano wa mawazo. 

Lakini kuna jambo la kujiuliza zaidi kwamba huu mgongano wa mawazo unatokea kila siku hadi fani na maudhui yake yakilingana kwa kila jambo? Ni vema wasanii wetu waamke na kufahamu kuwa wapo wanaofuatilia filamu kila siku, ndani na nje ili kujua ulimwengu huo ukoje na kipi kinaingia sokoni. 

Tukikumbusha uteuzi wa majina ya filamu ni vema kuangalia matumizi sahihi ya lugha. Haiwezekani filamu ikapewa jina ambalo linaleta utata. Lazima wasanii wetu waangalie mfano bora uliopo kwenye filamu ya Ulimi ya Jackline Wolper Masawe. 

Kwanza ni jina la filamu kujenga udadisi kulikoni ‘Ulimi’, kisha humfanya mteja awe na shauku zaidi hasa anapoona kitu kilichozoeleka lakini anapaswa kujihadhari nacho. 

Hakuna filamu inayoweza kupigiwa kelele iwapo itazingaitia ujuzi au utunzi ambao una fani na maudhui tofauti na nyinginezo za ughaibuni. Lakini kwa wasanii wenyewe wanatakiwa kutazama filamu nyingi ili kuepuka migongano huku hadhira ikiwaona kama hawana jambo jipya. 
 
Hakuna njia nyingine hapo zaidi ya kuzingatia matumizi ya lugha, maana ya maneno, kuacha kutongoa filamu za nje, kuwa wabunifu zaidi, kutengeneza fani na maudhui yanayorandana na mandhari yetu. Haya yatawafanya wasanii wawe bora zaidi kwa kazi zao ili kuepusha utata huo.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako