August 24, 2013

OLE WENU WAJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA


Niseme mapema naungana na Jaji Warioba ambaye ameonya vyama vya siasa pamoja na wajumbe wa Mabaraza ya katiba kutumia ajenda za vyama hivyo badala ya kutoa mapendekezo kwa Tume.
Kuna mambo yanasikitisha juu ya tafsiri ya wajumbe wa Mabaraza ya Katiba, badala ya kufanya upembuzi yakinifu juu ya Katiba Mpya, baadhi ya wajumbe wamegueza vikao hivyo kuwa sehemu ya kulalamika, kutuhumu na kuhukumu.
Hivi karibuni tumemsikia Profesa Mwesiga Baregu akimuonya mjumbe mmoja aliyeshutumu kuwa eti wasomi wanaipeleka pabaya nchi hii bila kuchambua mapendekezo yaliyoko kwenye Rasimu ya katiba mpya.
Nitangulie kusema, ujumbe wangu wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba, wanapaswa kupendekeza mambo muhimu kwa niaba ya wananchi kwenda Tume ya Rasimu ya Katiba.
Acheni kubeba magunia ya malalamiko na kugeuzwa madaraja ya vyama bali ongezeni mapendekezo nyeti na kushauri marekebisho pale inapotakiwa. Lawama kwa Tume ya Jaji Warioba hazitasaidia.
Kwa mfano, baadhi ya Wajumbe, wanachangia maoni  kwa kutumia waraka ambao unaelezwa kusambazwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenda kwa wanachama.
Tunafahamu kuwa CCM haitaki muundo wa serikali tatu bali inaunga mkono serikali mbili. Mpaka wakati huu, waraka wa CCM umezusha rabsha kidogo miongoni mwa wananchi ambao wanadhani chama hicho ndicho kinastahili zaidi kusikilizwa ama kinabeba uamuzi wa kufikiri wa watanzania.
Nadhani muundo wa serikali mbili unatakiwa kutetewa kwa hoja, na sio hisia sababu hakuna sehemu nzuri ya kuwasilisha mapendekezo kama muda uliopangwa mpaka Tume ikakamilisha shughuli zake.
Kuna hatari moja inayoweza kutokea kwenye mchezo huu ambao umeasisiwa na CCM, kwamba katika kipindi hiki tunachotakiwa sio kwuaelekeza wajumbe wa Mabaraza ya katiba waseme nini, bali kuwapangia maeneo ya kuzungumzia bila kuathiriwa na ajenda ya chama chochote.
Kama CCM inadhani serikali tatu ni tatizo basi inayo haki ya kupinga kwa hoja sio vinginevyo. Onyo langu kwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ni hili, leo hii mnaweza kujisikia fahari sana kutumika kwa matakwa ya CCM ambacho ni chama cha siasa.
Lakini kuna kipindi tutafika mahali tutalazimika kufumua mambo mengi kutokana na mzaha unaofanywa sasa. Tume ya Katiba inaongozwa kwa taratibu ambazo zinaelekezwa kwenye kanuni ya Mabadiliko ya Katiba ambayo watu (wajumbe) wanatakiwa kutoa maoni yao sio kutumwa na chama chochote.
Kuna kelele nyingi nchini Misri, Rais Mohamed Mosri aligombana na raia wa nchi hiyo kwenye utungaji wa Katiba mpya kama tunavyofanya sisi hapa nchini.
Wakati chama chake kikipendekeza kuundwa kwa Jamhuri ya Kiislamu kama Katiba ya mwaka 1980 ilivyosema, wao wakataka kuwalazimisha wananchi wakubali hata kwa shuruti. Mpaka leo hakuna utulivu Misri.
Sasa, kwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba wanaodhani kuwa kuteuliwa wkao ni kama sehemu ya kucheza ndombolo ama kwasakwasa waache mara moja. Suala la katiba mpya sio kitu cha kuchezea hata kidogo.
Ni lazima wajumbe wa Mabaraza ya Katiba wafahamu kuwa wamekabidhiwa jukumu zito sana la kuimarisha na kusimika ujenzi wa taifa letu.
Leo hii tunaweza kuchekelea sana waraka wa CCM, ama hata ungekuwa wa chama chochote, lakini huko tuendako tutaanza kutafuta mchawi, na baadaye tutanyoosheana vidole na kumgeukia Jaji Joseph Warioba na timu yake iliyoketi na kutumia nguvu pamoja na akili zao kukusanya maoni ya watanzania wote kuunda Katiba.
Tukishatafuta mchawi kitakachofuata ni kukosa maelewano na kuanza kutwangana wenyewe. Tumeunda Mabaraza ya Katiba ili kufanikisha mchakato wa kupatikana Katiba Mpya sio sehemu ya kupiga porojo ama kuimba nyimbo za vyama vya siasa.
Kwenye mabaraza ya Katiba hatuzungumzii maslahi ya chama chochote bali tunaizungumzia Tanzania ambayo inahitaji uponyaji wetu.
Mabaraza ya Katiba sio sehemu ya kupenyeza sumu za kulalamika na kubebeshana tuhuma ambazo haizna msaada wowote kwa taifa. Hakuna nchi yoyote itakayotusaidia kukamilisha mchakato huu, na tusipokuwa makini leo basi tutalia na kusaga meno.
Onyo langu moja, Wajumbe msigeuze mikutano ya Mabaraza ya Katiba kama sehemu ya mikutano ya kisiasa. Nimemaliza.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako