September 20, 2017

HUYU NDIYE JAJI MKUU DAVID MARAGA

NA MARKUS MPANGALA

BAADA ya Mahakama ya Juu nchini Kenya kufuta matokeo ya uchaguzi, watu wengi wamejiuliza Jaji David Maraga ni nani? Swali hilo bila kujali Majaji wengine 6 walioungana naye kusikiliza shauri lililofunguliwa na mgombea wa upinzani, Raila Odinga dhidi ya Tume ya Uchaguzi, Chama cha Jubilee na Uhuru Kenyatta. Kabla ya kueleza David Maraga ni nani, ni vizuri kuwajua majaji wengine 6 walioungana na Jaji huyo kusikiliza na kutoa hukumu ya kesi hiyo.


MAJAJI 7
Hawa ndio waliosikiliza kesi ya NASA dhidi ya IEBC, Jubilee na Uhuru Kenyatta. David Maraga (Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu). Philomena Mbete Mwilu ni Naibu Jaji Mkuu, ambaye amekuwa nafasi jaji kwa miaka 32.

Jaji Mohamed Khadhar Ibrahim, alikuwa wakili na aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu mnamo Juni 16, mwaka 2016. Jaji Profesa Jackton Boma Ojwang, ni wa kwanza anayehudumu kuwa na hadhi ya Uprofesa.

Jaji Dk. Smokin Wanjala, amesomea sheria vyuo tofauti nchini Kenya na nje ya nchi. Jaji Njoki Susanna Ndung'u, ni jaji wa pili mwanamke katika Mahakama ya Juu na mtetezi wa haki za kina mama na kijamii.

Jaji Isaac Lenaola, ambaye alijiunga na Mahakama ya Juu mwaka 2016 kuchukua mahali ya Jaji mstaafu Philip Tunoi na Jaji mstaafu Kalpana Rawal. Aidha, Jaji Lenaola alikuwa jaji wa Mahakama Kuu kitengo cha Katiba na Haki za Binadamu kabla ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu.

DAVID MARAGA NI NANI?
JINA lake kamili ni David Kenani Maraga, ndiye Jaji Mkuu na rais wa Mahakama ya Juu ya Kenya. Maraga alizaliwa Januari 12 mwaka 1951 na ana umri wa miaka 65. Maraga ni mzaliwa wa Bonyamatuta katika Kaunti ya Nyamira nchini Kenya.  

Jaji Maraga
Mwaka 1977 alipata shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi na baadaye alipata shahada ya uzamili katika chuo hicho. Mwaka 2003 Maraga aliteuliwa kuwa rais mstaafu Mwai kibaki kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Mwaka 2012 Tume ya Huduma za Kimahakama ilimteua kuwa Jaji wa Mahakama ya rufaa. Tangu uteuzi huo Bodi ya Uchunguzi ya Majaji na Mahakimu ilikuwa ikimchunguza kabla ya kumthibitisha kuendelea na kazi yake baada ya mgongano mkali ambapo alitaka kula kiapo kwa kutumia biblia pamoja na kusisitiza kuwa hajawahi kupokea rushwa katika kazi yake.

Mwaka mmoja baada ya kuwa jaji wa Mahakama ya rufaa, aliwania nafasi ya urais wa mahakama hiyo lakini alishindwa na nafasi hiyo kuchukuliwa na Jaji Kihara Kariuki. Mei mwaka 2012 Jaji Maraga aliteuliwa na Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kimahakama ya maandalizi ya uchaguzi wa Kenya (JWCEP). Madhumuni ya kamati hiyo ilikuwa kujiandaa na migogoro yoyote au mapingamizi ya uchaguzi mkuu wa Machi mwaka 2013.

Mwaka 2013 rais Uhuru Kenyatta alimteua Jaji Maraga kuwa mwenyekiti wa tume ya kimahakama ya uchunguzi dhidi ya Jaji wa mahakama kuu, Joseph Mutava baada ya kuibuka malalamiko katika hukumu aliyotoa kwa Kamlesh Pattni kuhusiana na kashfa ya Goldenberg. Tume hiyo ilitoa ripoti yake Septemba 2016 na kupendekeza kwa rais Kenyatta kumwondoa Jaji Mutava.

JAJI MKUU
Kabla ya uteuzi wa Jaji Mkuu, David Maraga alikuwa rais wa Mahakama ya rufani Kisumu. Aidha, kabla ya uteuzi wa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Kenya mwaka 2003, Maraga alikuwa Wakali wa kujitegemea kwa kipindi cha miaka 25. Jaji Maraga aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu kuchukua nafasi ya Jaji Willy Mutunga ambaye alistaafu Juni mwaka 2016.

Kwa mujibu wa Tume ya Huduma ya Mahakama, Jaji Maraga kabla ya uteuzi wake alikuwa miongoni mwa majaji 11 ya walioomba kuteuliwa kuwa Jaji mkuu.

Baadhi ya majaji ambao waliangushwa na Jaji Maraga katika kinyang’anyiro hicho ni Profesa wa sheria Makau Mutua, Jaji wa Mahakama ya Juu, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala, Jaji Aaron Ringera na Jaji Alnashir Visram.

Jaji Maraga amekuwa Jaji wa pili kuhudumu nchini Kenya tangu kuanza kutekelezwa kwa katiba ya sasa nchini Kenya, ambayo ilifanyia mabadiliko mfumo wa Mahakama mnamo mwaka 2010. Kama Jaji mkuu, David Maraga anakuwa pia Rais wa Mahakama ya Juu ambayo husikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi za matokeo ya uchaguzi wa urais. Maraga alikula kiapo cha kuwa Jaji Mkuu mnamo Oktoba 19, 2016, ambacho kilimaanisha kuwa ni jaji mkuu wa 14 katika historia ya Kenya, na wa pili baada ya mabadiliko ya mfumo w kimahakama.

MHAFIDHINA
Wakati wa kuhojiwa kwake na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), kabla ya jina lake kupendekezwa kwa rais, alikuwa amedokeza kwamba hawezi kufanya kazi siku ya Jumamosi ambayo ni siku ya kupumzika kwa mujibu wa dini yake ya Sabato.

KUTETA NA ODINGA NA KENYATTA
WIKI mbili baada ya kuapishwa kuwa Jaji Mkuu mnamo Oktoba mwaka 2016, David Maraga alifanya mazungumzo na kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika Mahakama ya Rufani kwa muda wa saa moja na nusu.

Mazungumzo hayo yalikuwa sehemu ya mpango wake kama rais mpya wa Mahakama ya Rufani kuzungumza na wanasiasa waandamizi, ambapo awali alianza kufanya kikao cha kwanza rais Uhuru Kenyatta kabla ya kukutana na Raila.

Katika kipindi hicho Jaji Maraga alikutana na wanasiasa wakubwa nchini humo na kuwahakikishia uwazi wa hukumu za kesi zote. Pia alisisitiza kusimamia heshima ya Mahakama ya Rufani.

“Napenda kuwahakikishia wananchi, Mahakama ipo tayari na inamudu kusikiliza mapingamizi yote yatakayotokea mwakani (uchaguzi wa mwaka 2017),” alisema Jaji Maraga alipokuwa akizungumza na Raila Odinga na wafuasi wake, ikiwa ni njia ya kujenga imani kwa mhimili huo.

Viongozi wengine walioambatana na Odinga walikuwa Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula. Kabla ya kikao hicho idara ya mahakama ilikuwa na uhusiano mbaya na wanasiasa wa upinzani hususani Raila Odinga baada ya uamuzi kuhusu uchaguzi wa urais wa mwaka 2013 ambapo Mahakama ya Juu ilitoa uamuzi uliothibitisha ushindi wa Uhuru Kenyatta.

©Nishani Media
4/9/2017

No comments:

Post a Comment

Maoni yako