September 14, 2017

HUYU NDIYE MUHINGO RWEYEMAMU

NA MARKUS MPANGALA

Ninajaribu kuweka wasifu wa ndugu Muhingo Rweyemamu. Baadhi ya wasomaji wetu hapa wanasema hawakuwahi kumfahamu kwa kina.
KIFO: Muhingo alifariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kifo chake kimemkuta huko akiwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa Myelofibrosis (hudhoofisha uwezo wa kinga za mwili kutengeneza damu) hivyo kusababisha kuwekewa damu mara kwa mara.
 TAALUMU: Ni mwalimu kwanza. Baadaye mwaka 1993 alijiunga na tasnia ya uandishi wa habari (hapo ndipo nilipokutana naye kwa mara ya kwanza mwaka 2006 akiwa kampuni ya New Habari (2006) Limited wamiliki wa magazeti ya MTANZANIA, DIMBA, RAI, THE AFRICAN, na BINGWA.

 
KAZINI: Ni mmoja wa wahariri waanzilishi wa gazeti la Mwananchi na The Express. Alianza kama mwandishi wa kawaida na kupanda ngazi hadi Mwandishi Mwandamizi, baadaye Mhariri wa Makala, kisha Mhariri, Mkuu wa Kitengo cha Picha (Gazeti la Mtanzania). Kisha amewahi kupanda ngazi zaidi kuwa Mhariri wa Rai, Naibu Mhariri mtendaji, na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited (2008-2010).
Mwaka 1984-1985 alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Igwata, Geita.
Mwaka 1985-1987 alikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makongo, Dar es Salaam.
Mwaka 1989 alikuwa Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Morogoro.
Mwaka 1989-1992 alikuwa Katibu Uenezi Taifa wa Chama cha Wanataaluma ya Uenezi.
Mwaka 1993-1995 alikuwa mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na The Express.
Mwaka 1995-1998 alikuwa Mwandishi Mwandamizi , Mhariri wa Makala, Mhariri na Mkuu wa Kitengo cha Picha katika Gazeti la Mtanzania .
Mwaka 1999 alikuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la “Wiki hii”.
Mwaka 1999-2001, alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi.
Mwaka 2003, alikuwa Mwakilishi wa Jarida la habari za mazingira la ENS la nchini Marekani.
Mwaka 2004-2005, alikuwa Mhariri Mshiriki akihusika na mambo ya kisiasa katika Gazeti la Citizen.
Mwaka 2006-2008 alikuwa Mhariri wa Gazeti la Rai.
Mwaka 2008-2010, alikuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.

NJE YA FANI: Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni (Tanga), ambako alianzisha programu ya “NIACHE NISOME” kama njia ya kupambana na mimba kwa wanafunzi wa kike. Baadaye alihamishiwa Wilaya ya Makete mkoani Njombe, kabla ya mwaka 2015 kuwa mkuu wa wilaya ya Morogoro Mjini.
KUFANANA: Muhingo Rweyemamu na Elisa Muhingo (rafiki yangu pia hapa mtandaoni) ni watu wenye waliobahatika kuwa na “Fikra Pevu”. Wawili hawa nimewasoma sana kazi zao, kama zilivyo za Jenerali Ulimwengu na Ezekiel Kamwaga. Hawa wamekuwa sehemu ya “kuchonga” staili zangu katika siasa za ndani na nje, michezo,utamaduni na jamii.
ELIMU: Mwaka 2004 alihitimu masomo ya Shahada ya Kwanza ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa.
Mwaka 1993 alihitimu Stashahada ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha TSJ.
Mwaka 1989 alihitimu Stashahada ya Elimu katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dar es Salaam.
Mwaka 1983 alihitimu Astashahada ya Elimu katika Chuo cha Ualimu cha Tukuyu, Mbeya.
Mwaka 1977 alihitimu Elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Nyakato.


No comments:

Post a Comment

Maoni yako