October 09, 2017

MIAKA 50 TANGU CHE GUEVARA AUAWE, BADO ANAISHI

NA ZITTO KABWE
 
MIAKA 50 imetimia tangu Komredi Che Guevara auwawe huko Bolivia mnamo tarehe 9/10/1967. Che, mwanamapinduzi mzaliwa wa Argentina na mkombozi wa Cuba ni mmoja wa wanadamu waliojitoa mhanga kupambana dhidi ya ubeberu kote duniani. Katika maisha yake aliwahi kupita Tanzania na kushiriki kwenye vikao na vyama vya ukombozi kusini Mwa Afrika. 

Tanzania iliunganishwa na Che kupitia Zanzibar. Vijana wa Zanzibar walipelekwa mafunzoni Cuba Kwa ajili ya ukombozi. Mwaka 1962 wakati wa mgogoro wa Oktoba 1962, vijana wa kizanzibari waliokuwa mafunzoni Cuba walijitolea kupigana bega Kwa bega na waCuba dhidi ya Marekani. Jambo hili liliwafungua macho wacuba kuhusu Afrika na Kwa hakika Afrika yao ilikuwa Zanzibar.


Vijana hao baadhi yao wapo hai wakiwa ni wazee Sasa. Mmoja ni Mzee Ali Sultan Issa na Komred Shaaban ( pichani nikiwa naye nyumbani Kwa balozi wa Cuba ). Pia Dkt. Salim Ahmed Salim akiwa Mkuu wa Ofisi ya Zanzibar kule Havana, Cuba. Mzee Ali Sultan Issa ndiye alikuwa mwenyeji wa Che huko Zanzibar mwaka 1965. Prof. AbdulRahman Mohamed Babu, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Zanzibar na baadaye Waziri wa zamani wa Uchumi wa Tanzania alikuwa mtu wa karibu wa Che Guevara. Pichani walipokuwa kwenye mkutano huko Geneva, Uswiss. 

Kwa sisi watu wa Kigoma Ujiji Che Guevara ana historia kubwa. Che alikwenda Congo mwaka 1965 kupigana dhidi ya mabeberu waliomwua Patrice Lumumba. Alikaa huko miezi 7. Alipokwenda Congo alipitia Kigoma na kulala nyumbani Kwa Mkuu wa Mkoa wakati huo akiitwa Semvua Msangi ( mtoto wa Semvua alikuwa Mwalimu wangu Shule ya Sekondari Kibohehe Moshi, akiitwa Zidikheri Semvua Msangi). 

Che alipanda Boti kutokea kijiji cha Bangwe kwenda Congo. Hata alipokuwa akifanya mikutano walifanyia Kigoma mjini akiwa pamoja na kina Mzee Laurent Kabila ambaye baadaye alikuja kuwa Rais wa DRC.
Che Guevara katika nyakati hizi aliitwa Tatu huku mwenzake Dreke akiitwa Moja ili kuficha majina yao ya asili. 

Moja bado yupo hai na Kwa kushirikiana na ubalozi wa Cuba tumemwalika kuja nchini na yeye pamoja na aliyekuwa Myeka wa Che wataambatana na baadhi ya Watanzania kwenda Kigoma Kwa kufuata njia aliyopita Che.
Manispaa ya Kigoma Ujiji imeamua kutunza historia Hii Kwa kuiita Che Guevara Barabara inayoanzia Stesheni ya Reli mpaka mji wa Bangwe. Pia mazungumzo yanaendelea na Meya wa Mji wa Cadiz katika Nchi ya Spain ili kujenga jengo la makumbusho mjini Kigoma Kwa ajili ya kuenzi nafasi ya Kigoma katika juhudi za ukombozi dhidi ya ubeberu barani Afrika. 

Che Guevara ni alama halisi ya mwanamapinduzi wa kimataifa aliyepinga dhuluma kokote duniani. Maneno yake ya mwisho Kwa mkewe na wanawe yalidhihirisha hilo. Aliwaambia uzuri wa uanamapinduzi ni kuchukia dhuluma inayofanyika dhidi ya yeyote popote duniani. Kwa kimombo alisema;
"Above all, always be capable of feeling deeply any injustice committed against anyone, anywhere in the world. This is the most beautiful quality in a revolutionary.”
Che bado anaishi.

Zitto Kabwe Ni mbunge wa Kigoma Mjini

No comments:

Post a Comment

Maoni yako