December 28, 2017

AKAMATWA NA VITAMBULISHO 65 VYA KUPIGIA KURA

NA MWANDISHI WETU, SONGEA
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limemkamata Rajab Seleman (27) mkazi wa mkazi wa Nakawale Halmashauri ya wilaya ya Songea akiwa na vitambulisho 65 vya kupigia kura vya wakazi wa kijiji cha Nakawale.
Kamanda wa Polisi wa Ruvuma, SAPC Mushy
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma SACP Gemini Mushy amesema mtuhumiwa Seleman ambaye pia ni mpigapicha na amefuzu mafunzo ya ualimu alikamatwa Desemba 26 mwaka huu majira ya saa saba mchana katika stendi ndogo ya mabasi ya abiria.


Kwa mujibu wa Kamanda Mushy mtuhumiwa alidai alipewa na wananchi wa kijiji cha Nakawale ili kuwasaidia kutoa nakala kwa ajili ya maandalizi ya vitambulisho vya utaifa yaani NIDA.
Hata hivyo anasema polisi waliwasiliana na uongozi wa kijiji hicho ambao walithibitisha kuwa walifanya mkutano wa hadhara wa maandalizi ya vitambulisho vya NIDA na kwamba walimuomba kijana huyo kutoa nakala za vitambulisho hivyo mjini Songea kwa kuwa katika kijiji hicho hakuna huduma hiyo.
“Tumefuatilia NIDA ili watujulishe kama utaratibu huo unaruhusiwa,lakini pia Jeshi la Polisi tunaendelea kufanya uchunguzi,ikiwa atabainika na hatia ya kumiliki vitambulisho kinyume cha sheria,taratibu za kisheria zitafuatwa’’,anasisitiza Kamanda Mushy.

HAKI: RUVUMA MULTMEDIA.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako