December 27, 2017

IJUE ASILI YA LIKUNGU AU NGUNGA (LAKE NYASA FLIES)

NA PROF. MARK MWANDOSYA, MATEMA BEACH, KYELA.
UKIKAA ufukweni Matema wakati Ziwa Nyasa likiwa limetulia, kwenye upeo, kwa mbali kabisa unaweza kuona umbile kama vile moshi unaobaki nyuma kama meli imepita. Mara ya kwanza nilibishana na wenyeji wangu nikiwaambia meli ya MV Songea ilikuwa ikipita kwa mbali kutoka bandari ndogo zilizo mwambao wa Ziwa. 

Wenyeji wakanicheka kama vile sijui kitu. Na hakika sikuwa najua. Kwani ule ulikuwa sio moshi bali makundi makubwa ya wadudu wenye umbo la mbu ambao huletwa mwambao na upepo mkali unaotoka ziwani. 

Ngunga (Chaoburus edulis) utokana na mabuu (Larvae) ambao huzaliana juu ya maji. Baada ya kukua hubadilika kuwa kama mbu au inzi wazima na huelea katika makundi makubwa ambayo huonekana kwa mbali kama moshi.

Mabuu ni chakula cha muhimu cha samaki na Ngunga wenyewe ni chakula cha ndege na binadamu. Makundi ya ngunga yanapofika ufukweni wenyeji hujitokeza na ndoo na vikapu ili kuwakusanya.

Ngunga walioletwa pwani na upepo kutoka Ziwa Nyasa. Kwa taarifa za wenyeji wa hapa, baada ya kuwatengeneza kama keki, Ngunga huwa chakula kutamu sana na chanzo muhimu cha protini kwa ajili ya mwili. 

Chakula kinachotengenezwa kutokana na Ngunga. Wenyeji huku hawakosi maelezo kuhusu asili ya Ngunga. Ukiongea na baadhi yao watakwambia Ngunga wanatoka kwenye miamba iliyo chini ya Ziwa. Wakifika ufukweni, baada ya siku moja hurudi majini na hukua na kuwa samaki wadogo, dagaa au usipa, kama dagaa wanavyojulikana huku. Wengine watakwambia Ngunga wanatokana na Nyifwila (Zimwi) anapofuka moshi.

2 comments:

  1. Asante sana kuna sehem nataka nifahamishwe sana mabuu wakike

    ReplyDelete
  2. Alafu huzaliwaje na wapi kwenye ziwa sehem gani asante sana mpangala

    ReplyDelete

Maoni yako