December 11, 2017

WAZIRI MKUU ATAMBUE NYASA IMEJAA UTAJIRI-2

Na MARKUS MPANGALA
SEHEMU ya kwanza ya makala haya katika safu hii tulichagiza kuwa agizo lililotolewa na Waziri mkuu katika hotuba yake akimwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala kuanzisha Mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza utalii na kuendeleza fukwe ambazo hazina shughuli kwa madhumuni ya kukuza utalii Kanda ya Kusini na mengineyo. Endelea kusoma….

Madhali linalozungumzwa ni kuhakikisha fukwe zinakuwa na tija ni muhimu pia kuikumbusha mamlaka husika kuwa wilaya ya Nyasa inao utajiri mkubwa sana wenye tija kupitia sekta ya utalii ambayo kihistoria maeneo mengi bado ni mbegu bora n zenye kuvutia. 

Si hilo, wilaya hiyo inao uwezo wa kuwa na viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali lakini kwa sharti moja muhimu; iwapo changamoto zinazoikabili Halmashauri zitattuliwa kwani zitakuwa chachu ya kukuza mapato ya ndani. Hatuimwagii sifa hizo za bure bali yapo mambo ya kuyaangalia kwa kina. Leo ninatoa mifano mingine ambayo kwa namna moja au nyingine itawafumbua macho wasomaji na watu mbalimbali wanaofuatilia mfululizo huu. 

FUKWE
Sifa kubwa ya Ziwa Nyasa ni kuwa fukwe bora na zisizo na uchafu wowote. Kama tulivyoona wiki iliyopita sifa zilizotajwa na rafiki yangu Ilan kutoka Israel, ndivyo ukweli ulivyo. Katika Kijiji cha Mtupale kilichopo Kata ya Chiwanda kuna fukwe za mawe ambazo ni kivutio adimu cha utalii. Ukitembelea mwambao mwa ziwa Nyasa kuna maeneo mengi yenye fukwe za mchanga unaovutia, lakini katika mwambao mwa Kata ya Chiwanda kuna fukwe za mawe ambazo bado wawekezaji hawajafungua milango ya Utalii kanda ya Kusini. 
Ufukwe wa Mchanga katika forodha ya Chivanga iliyopo kijijiji cha Lundu



Ikumbukwe Kijiji hicho kinapakana na kingine cha Chiwindi ambacho ndicho cha mwisho kabla ya kuingia mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji. Eneo hili linao ubora wa hali ya juu. Zipo fukwe zingine zenye kuwavutia watu ni Ndengere, Ngindo, Lundo, Lipingo, Mkali, Hongi,Liuli,Kihagara,Mkili, Lundu,Mbaha, na Ndumbi kwa kuzitaja chache ni sehemu ambazo zinahitaji nguvu kidogo sana za uwekezaji kabla ya kuleta tija kwa wawekezaji. Ikumbukwe kijiji cha Ndumbi ndicho chenye bandari ambayo Makaa ya Mawe yanayochimbwa na Kampuni ya TanCoal. Ni mahali ambapo unaweza kutumia darubini kuitazama nchi jirani ya Malawi kwa ufasaha. 


Fukwe za miji iliyozoeleka kupokea wageni kutoka ng’ambo ni Mbamba Bay, Kilosa, Liuli, Lundu na ufukwe bora kabisa wa Mhalo (Mhalo Beach) ni miongoni mwa maajabu yaliyopo katika wilaya ya Nyasa. Baadhi ya fukwe hususani zilizopo Mbamba Bay kuna hoteli za uhakika ambazo zinawapa nafasi watalii kuishi kwa utulivu. Mji wa Liuli umemuwa mkongwe kwa kupokea watalii, nao umekuwa na hoteli zenye uhakika. 

HIFADHI ZA ASILI
Mosi, Miongoni mwa mambo ambayo yanaipatia sifa Wilaya ya Nyasa ni hifadhi za asili.  Mkoa wa Ruvuma umepata hifadhi ya wanyamapori ya pili ya asili inayoitwa ‘Mbamba Bay Hill’ ambayo ipo mjini Mbamba Bay makao makuu ya wilaya ya Nyasa.
Hifadhi hiyo ni ya kipekee hapa Tanzania ya kwanza ya asili iliyopo mjini inaitwa Luhira iliyopo kilometa saba toka mjini Songea mkoani Ruvuma iliyoanzishwa mwaka 1974. Hivyo basi mkoa wa Ruvuma umepata hifadhi ya pili ya asili mjini. 

Kwa mujibu wa Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Chale anasema mchakato wa kuendeleza Mbamba Hill unaendelea vizuri na kwamba ya tayari bajeti ilipitishwa.  Eneo la hifadhi hiyo limeshapimwa na lina ukubwa wa ekari 420, ndani ya hifadhi hiyo kuna wanyama kama Nyani, Nyoka, Pimbi, Chui na ndege wa aina mbalimbali.

Aidha, bajeti ya kujenga uzio kuzunguka Mbamba Bay Hill imepitishwa na kwamba ujenzi unatarajia kuanza wakati wowote fedha zitakapoletwa na kwamba mara baada ya ujenzi wa uzio kukamilika wanyamapori wa aina mbalimbali wanatarajia kuongezwa, kwa mfano, Swala, Fisimaji, mbuzi Mawe, Digidigi, Mbawala na kwamba wanyama watakaongezwa ni wale ambao wanaweza kuishi katika mazingira ya hifadhi hiyo ambayo imeungana na ziwa Nyasa.
Ufukwe wa Mawe
Hifadhi nyingine itakuwa ni kisiwa cha Mbamba Bay maarufu kwa jina la Kisiwa cha Zambia, kina ukubwa wa ekari 27. Kisiwa hicho kimependekezwa kuwa hifadhi ya wanyamapori, kimejaliwa kuwa na uoto unaovutia wa misitu ya miombo ambao ni maarufu duniani ambapo mawe yanayozunguka katika kisiwa hicho ni mazalia ya samaki wa mapambano aina zaidi ya 400 wanaopatikana katika ziwa Nyasa pekee. 

Kutokana na udogo wa kisiwa cha Mbamba Bay Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anashauri katika kisiwa hicho kusijengwe makazi ya kudumu kwa ajili ya wafanyakazi wa kuhudumia watalii ili kuendelea kutunza uoto wa asili uliopo hivi sasa.

Hifadhi ninyingine ni msitu wa asili wa Chiwindi yenye ukubwa wa ekari  3000 ambao upo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.  Nyingine ni hifadhi ya misitu ya asili ya tarafa ya Ruhekei yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 2000 ambayo iliyoanzishwa mwaka 1938 na serikali ya Kikoloni.

Kisiwa cha Lundo ni miongoni mwa visiwa vilivyopo katika Ziwa Nyasa, kikiwemo cha Lundo kilichopo kata ya Lipingo na Tarafa ya Ruhekei wilayani Nyasa. Kisiwa hicho kina jumla ya ekari 20 kimepewa jina la Lundo kwa sababu watu wa kwanza waliovuka kisiwa hicho kwenda ng’ambo ya pili walifikia kijiji cha Lundo.

Taarifa za Maliasili ya mkoa wa Ruvuma inaonyesha kuwa kisiwa hicho tangu zamani kilikuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa vijiji vya Lundo, Ngindo na Chinula kwa sababu wakati wa vita ya Majimaji vilivyotokea kati ya mwaka 1905 hadi 1907 watu walikuwa wanakimbilia katika kisiwa hicho ambacho kina maeneo ya maficho.

Baada ya vita ya Majimaji kuanzia mwaka 1908 kisiwa hiki kilitumika na wakoloni wa kijerumani kuwahifadhi watu waliopata ulemavu kutokana na ugonjwa wa ukoma ambao baada ya uhuru walihamishiwa katika makazi ya Ngehe wilayani Nyasa. Serikali imependekeza visiwa vya Lundo na Mbamba Bay kuwa hifadhi za wanyamapori. 

Visiwa hivyo vitakuwa ni hifadhi ya pekee ya wanyamapori pamoja na samaki wa mapambo wanaozaliana katika visiwa hivyo ndani ya ziwa Nyasa. Ndiyo kusema vitavutia watalii kufika kusini na kutekeleza Sera ya nchi ya kufungua biashara ya utalii Kusini.  Usikose sehemu ya tatu ambayo nitakupa simulizi za kushangaza kuhusu wilaya ya Nyasa. Tuwe sote.

ITAENDELEA….

No comments:

Post a Comment

Maoni yako