January 01, 2018

HERI YA MWAKA MPYA 2018! NGUVU YA HABARI


“Kama habari zozote ziwe nzuri au mbaya za sehemu yoyote hazisemwi au kutangazwa maana yake ni upenyo kwa wenye mamlaka “kutojali” kwasababu watasema, “nani atajua”. Kama habari mbaya zikisemwa maana yake inawazindua wenye mamlaka au watu wengine kufahamu kinachoendelea sehemu hiyo. 

"Kama habari nzuri zikisemwa maana yake zinavutia wengine kama fursa na mwelekeo mpya wa kijamii au kiuchumi. Tumia nyenzo yoyote kuhabarisha hata ikiwafikia marafiki zako watano tu inatosha sana kwasababu nguvu zake kubwa kuliko kubaki na fikra duni kuwa "nani anazitaka". 

"Kanda ya kusini ingali na nguvu ndogo sana katika habari. Mkondo wa habari Kanda ya kusini umekuwa duni kwasababu zifuatazo: wapashaji habari wachache wenye nguvu katika taasisi, wapashaji habari binafsi hawaoni umuhimu (sawa na kusema nina mambo yangu nyeti), miundombinu hafifu, kutojali au baadhi kukosa nyenzo. Lakini suluhisho lipo; hizi ni zama za Uandishi wa raia (Citizen Journalism), ambapo mitandao ya kijamii (Blog, Facebook, Instagram, Twitter, Tagged, Badoo, LinkedIn, Vk, Connect, YouTube, Vimeo, Skype, Tumblr,Flickr, WhatsApp, inachukua mkondo mkubwa wa habari kama ilivyokuwa Blogu miaka ya mwanzoni mwa 2000.

"Nyenzo hii ya mitandao ya kijamii inatakiwa kutumika kuziba nakisi ya uhaba wa wapashaji wa habari (ambapo wanahabari watatumia mitandao hiyo kupata ‘tips’ za habari). Nguvu hii ya habari ndiyo kiini cha wenye mamlaka kufuatilia nani anatoa habari zaidi za eneo lake la kazi (wakinuia kuepusha habari hasi/mbaya).  Hizi ni zama Mpya, tuzikusanye habari zote! Lazima wakubali na watimize wajibu wao. Mabadiliko yanaanzia hapo hapo ulipo (mtaani kwako) kabla ya kufika sehemu nyingine (mitaa mingine/miji).

Wanazuoni wanasema habari ni uchumi na biashara. Habari ni jamii. Habari ni diplomasia. Habari ni maendeleo. Habari ni siasa. Habari ni utamaduni. Habari ni michezo. Habari ni kununua na kuuziana. Nguvu ya Habari ni kubwa.”-Markus Mpangala. 
Kwa niaba ya wenzangu Honorius Mpangala na Kizito Mpangala, tunawatakieni HERI YA MWAKA MPYA.

Wasalaamu!

©MARKUS MPANGALA
Mwandishi&Mhariri: New Habari(2006) Ltd (eg.Mtanzania, Bingwa, Rai& Dimba). Mwanablogu (2007-2018); lundunyasa.blogspot.com. Mhariri wa Vitabu; Nishani Media Co. Ltd.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako