April 20, 2008

Ziwa Limechafuka,Wanyasa na Ngalawa Tu

Nilikaa juu ya jiwe nikiangaza huku na huko kuwatazama wanyasa wanavyohaha katika shughuli zao za maisha ya hapa na pale.Nikaona ngalawa zinaumiza vifua vya wanyasa kwani hali siyo nzuri katika ziwa kwa sasa.Hakika ziwa nyasa limechafuka namaanisha dhoruba kali sana wiki hili,kila myasa/mvuvi unayemuona kanuna,kafura kama chatu ghadhabu imejaza vibaba wala haimithiriki zaidi ya hapo,hawacheki.Ziwa linanguruma mawimbi makali makali,nyavu zinapotea nyakati hizi shauri maboya yanazama kwa kushindwa kuhimili nguvu ya mawimbi.Lakini pamoja na kuchafuka kwa ziwa hilo hakuna hata mvuvi anayethubutu kusema atabaki nyumbani kujipumzisha au kurejesha zana za uvuvi nyumbani ili kupisha dhoruba hiyo,wapi bwana sahau kabisa habari ya wanyasa kuogopa dhoruba nyakati hizi au kuacha ngalawa ili kukosa kitoweo,hakuna mnyasa anayefikiri kula nyama za kuku wasiokomaa,wanaotafunika hata mifupi,wanaokuzwa kwa kudungwa sindano,wanatia kinyaa kuwala,au chipsi za huko mijini.Wanyasa wanaelewa uzuri wa kuwa wajuzi wa ziwa hili ambalo wenyewe wanasadiki kuwa hakuna ziwa lenye dhoruba kali ulimwenguni zaidi ya hili.Hakuna aliyeka chini kuacha ngalawa au kuacha kupanda mitumbwi.Yaani uvuvi unaendelea kana kwamba ziwa lipo shwari wakati "limekasirika" utafikiri limedungwa sindano ya kukasirika.Yote hao ni kitoweo cha asili hiki utamu adimu huu.

No comments:

Post a Comment

Maoni yako